
Pichani ni mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva.
KATIKA maisha kuna wakati binadamu anakuwa chini na wakati mwingine juu, unaweza ukamdharau mtu leo, kesho ukashangaa anakuwa tofauti kabisa na mategemeo yako.
Hivyo hivyo katika ulimwengu wa sanaa ya muziki kuna wasanii ambao hukaa kimya kwenye ‘game’ kwa muda lakini wanapokuja kuibuka wanatikisa na kuwa gumzo kila kona kutokana na kazi wanazotoa.
Leo tunakuletea listi ya wakongwe wa muziki ambao ndiyo habari ya mjini kwa sasa (wamerudi tena) kutokana na nyimbo zao kupata ‘airtime’ za kutosha kwenye redio na TV mbalimbali Bongo.

Ditto (Moyo Sukuma Damu)
Ni mmoja kati ya mhimili katika Jumba la Vipaji Tanzania (THT). Ditto ambaye pia aliwahi kuwa memba wa Kundi la La Familia na Watu Pori miaka ya nyuma kwa sasa ni habari ya mjini na wimbo wake wa Moyo Sukuma Damu.
Alikuwa kimya kwa kipindi kirefu, ikumbukwe kuwa 2011 aliachia mkwaju wa Tushukuru kwa Yote na baada ya hapo akawa kimya kwa muda hadi alipoibuka sasa.

Fid Q (Kemosabe)
Ukizungumzia kati ya wakongwe wa Hip Hop Bongo ni wazi jina la Fid Q hutaliacha kulitaja. Kuanzia miaka ya 2000 hadi sasa bado jamaa anakimbiza kwenye gemu.
Mwaka jana alisumbua na Ngoma ya Roho aliomshirikisha Christian Bella pamoja na Ngoma ya Sumu.
Amedhirisha kuwa amerudi tena baada ya kuachia Ngoma ya Kemosabe akiwa amechana mwanzo mwisho. Licha ya kupata shavu la kupigwa video yake mara kwa mara, ameonesha kitu cha kitofauti kutokana na kutumia mazingira ya ndani ya nyumba yake mwanzo mwisho.

Madee (Hela)
Anasimama katika listi hii kati ya wakongwe wasiochuja kwenye gemu. Mwaka jana alisumbua na Ngoma ya Migulu Pande.
Kwa sasa Ngoma ya Hela imemrudisha kwenye gemu ambapo ndani yake ameonesha kutumia staili f’lan ya kama ya kuuliza maswali hivi.

Chege (Kelele za Chura)
Mkongwe huyu ambaye kitambo anawakilisha Kundi la TMK Wanaume Family akiwa na Temba, kwa sasa anatingisha vilivyo na Ngoma ya Kelele za Chura akiwa amemshirikisha msanii kutoka THT, Nandy.
Mwaka jana pia alitingisha vilivyo na Ngoma ya Waache Waoane aliomshirikisha Diamond ambapo kideo chake kilifanyikia Sauz.

Dully (Yono)
Naye ni mmoja kati ya wakongwe waliotikisa mwanzoni mwa miaka ya 2000 akiwa na ngoma kibao kama vile Salome, Julietha, Nyambizi, Historia ya Kweli na nyingine kibao.
Dully ameonesha kuwa bado yumo baada ya kusumbua mwaka jana na Ngoma ya Inde aliomshirikisha mwanamuziki kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Harmonize.
Kwa sasa ameuanza mwaka vema baada ya kuachia kibao cha Yono ambapo amekiri kuwa kiitikio cha mkwaju huo kiliwahi kutumika katika moja kati ya nyimbo za Chameleone wa Uganda mwaka 2013.

Roma (Usimsahau Mchizi)
Ni kati ya wakali wa Hip Hop Bongo ambao hawashikiki katika muziki huo kila wakiibuka na ngoma mpya.
Roma ambaye pia anafahamika kwa kuchana ngoma nyingi zenye muelekeo wa kisiasa, kwa sasa anabamba vilivyo na Ngoma ya Usimsahau Mchizi akiwa amemshirikisha rapa kutoka Tongwe Records, Moni.
Gladness Mallya/GPL