ILIPOISHIA
Watu wale wakanitaka kuteremka, tukafanya hivyo na kuanza kulisogelea jumba lile kubwa lililoandikwa Illumiterant, yaani wenyewe wakiwa na maana ya KANISA LA SHETANI.
ENDELEA NAYO
Nilibaki nikishangaa, sikuamini kama mwisho wa siku nilitakiwa kuingia kanisani. Lilikuwa jengo kubwa, zuri, lililokuwa na urembo fulani wa dhahabu mlangoni, lilivutia kwa kuliangalia.
Mlango ukafunguliwa, kabla ya kuingia ndani kabisa, tukatakiwa kwenda sehemu fulani, hapo, tukaambiwa tuvue nguo, wenzangu niliokwenda nao waliufahamu utaratibu huo hivyo wakavua na mimi kufuata.
Ngoja nikwambie kitu kimoja ambacho watu huwa hawakifahamu. Kuna wengi niliwahi kuwasikia kwamba unapoingia katika makanisa kama hayo ambapo watu mnavua nguo na kusali miwa watupu, basi ni lazima mtatamaniana tu, haipo hivyo, ile hali ya kutamaniana kufanya ngono inaondoka kabisa.
Tuliingia mpaka ndani, hatukuingia tukiangalia mbele, tuliambiwa tugeuke na tuingie kinyumenyume, tukafanya hivyo. Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikishangaa, hilo lilikuwa kanisa la aina gani? Mbona lilikuwa tofauti na yale ambayo ninayafahamu mimi?
Tuliingia ndani kabisa, kulikuwa na viti kadhaa, hakukuwa na idadi kubwa ya watu ila niliambiwa kwamba watu wangeongezeka kadiri muda unavyozidi kwenda mbele.
Tulikaa katika viti vile tukiwa watupu kabisa ila baada ya dakika chache tukaletewa mavazi, yalikuwa mesui tu, ya moja kwa moja kama kanzu, mavazi hayo yalikuwa na alama ya msalaba kwa nyuma, msalaba ule ulikuwa tofauti kabisa, si kama ule aliosulubiwa Yesu, ulikuwa umegeuka, yaani kichwa chini miguu juu.
Nilipolivaa vazi hilo, nilihisi mwili wangu ukipata nguvu za ajabu, hofu ambayo ilianza kuutawala moyo wangu ikapotea na kuhisi nikipata nguvu mpya.
Ndani ya kanisa hilo watu walisimama mistari miwili, waliziba nyuso zao, tulikuwa kama watu ishirini hivi. Nakumbuka wote walikuwa wakiimba wimbo kwa sauti za chini, ilikuwa ni vigumu kufahamu ni wimbo upi waliokuwa wakiimba.
Mbele kabisa ya kanisa lile alisimama mwanaume mmoja, naye alikuwa ndani ya vazi hilo, alisimama imara huku mkononi akiwa na fimbo moja ya chuma iliyonakshiwa na dhahabu, yeye ndiye alikuwa kiongozi na watu wote walitakiwa kumsikiliza yeye.
“Kaeni chini,” alisema mwanaume huyo, wote wakakaa chini, na mimi nikafanya hivyo.
Kila mmoja alibaki kimya, ilikuwa ni kama wanamsikilizia mtu fulani afike mahali hapo, hakukuwa na mtu aliyezungumza kitu chochote na hata yule kiongozi aliyekuwa amesimama pale mbele naye akaungana nasi na kutulia.
Baada ya dakika kama tatu, mwanaume mmoja akatokea mahali hapo, yeye alivaa vazi kama yetu lakini lake lilikuwa na rangi nyekundu. Mwanaume huyo alituangalia kisha kutuamuru wote tuvue vazi lile sehemu ya usoni na kumwangalia yeye.
Watu walipovua hapo ndipo niliposhangaa, sikuamini kile nilichokiona mbele yangu. Miongoni mwa watu waliokuwa mahali hapo, zaidi ya watu sita nilikuwa nikiwafahamu vilivyo.
Wa kwanza alikuwa bwana Saidi Abdulaziz, huyu alikuwa Mpemba mwenye mabasi mengi yaliyokuwa yakifanya safari za kutoka Dar es Salaam na kwenda Mwanza, alikuwa na kiwanda cha kutengenezea karatasi na pia alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na fedha nyingi, yaani kwa kifupi alikuwa bilionea.
Baada ya kushangaa kuhusu bwana Saidi, mtu wa pili alikuwa Simon Peter, huyu alikuwa kijana wa miaka ishrini na tatu, alikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa na mafanikio makubwa. Alikuwa akimiliki vitu vingi vya thamani kama magari huku biashara zake zikiwa tata na wengine kuhisi kwamba alikuwa muuzaji mzuri wa madawa ya kulevya.
Mtu wa tatu ambaye nilimfahamu alikuwa msichana Pamela Ndanshau. Huyu alikuwa msichana mrembo, aliwavutiwa watu wengi, alikuwa mwanamuziki mwenye jina, aliimba nyimbo zilizompa mafanikio makubwa mpaka wakati mwingine watu kuhisi kwamba alikuwa mmoja wa watu kutoka katika dini hiyo kitu ambacho alikipinga sana.
Uwezo wake wa kuimba na umaarufu wake ulikuwa tofauti kabisa, alipendwa japokuwa watu wengi walisema kwamba hakuwa muimbaji mzuri. Hakuwa mtu wa kutulia, alitembea huku na kule bila kuchoka, kumbe katika yote hayo, alikuwa na nguvu kubwa ya shetani iliyokuwa ikimuongoza na ndiyo maana alipewa mashabiki wengi japokuwa uwezo wake ulikuwa mdogo.
Mtu wa nne kumuona alikuwa Potifa Maliki. Huyu alikuwa mzee mwenye asili ya Kiarabu kutoka nchini Misri. Alipenda sana kuwafundisha watu kuhusu mafanikio, watu walimpenda kwa kuwa alikuwa kioo cha jamii, alisaidia watu wengi, kuna tetesi zilisema kwamba kutokana na utajiri wake, kuna baadhi ya serikali hapa Afrika ziliazimwa pesa na yeye mwenyewe, bila kujua, kumbe naye bwana Potifa alikuwa ndani ya dini hiyo.
Mtu wa tano kumgundua alikuwa muigizaji Rashida Abdul, msichana mrembo ambaye naye alipendwa sana nchini Tanzaniia kutokana na filamu kali alizokuwa akiigiza. Msichana huyu alikuwa bilionea, kila filamu aliyoitoa, ilipendwa, alijikusanyia mashabiki wengi, jina lake lilijulikana Afrika nzima, aliitetemesha Afrika kipindi hicho, hakukuwa na aliyejua kwamba naye alikuwa na nguvu kutoka katika dini hiyo iliyokuwa ikikusanya watu.
Mtu wa sita na wa mwisho kumgundua sikuweza kuamini kama alikuwa yeye, alikuwa mtu mwenye nguvu Tanzania, aliposema hili lifanyike, lilifanyika, alisikilizwa sana, alikuwa na cheo kikubwa mno. Mtu huyu alijulikana kwa jina la Mtazar.
****
Kwa jina aliitwa Gabriel Mtazar, huyu alikuwa waziri wa mambo ya ndani na nje nchini Tanzania kipindi hicho. Alikuwa miongoni mwa watu waliopendwa sana, katika uchaguzi ambao ulifanyika nchini humo kipindi hicho cha nyuma, aliongoza kwa kura nyingi zaidi ya wabunge wote nchini Tanzania.
Alikuwa kipenzi cha watu, alipendwa na alikuwa maarufu hata zaidi ya rais wa nchi hiyo. Kila siku katika maisha yake alikuwa mtu wa kuwasaidia watu wengiine, alikuwa bilionea mkubwa ambaye alijitangaza kabisa kwamba yeye alikuwa mtu wa watu, mali alizokuwa nazo hazikuwa zake bali alichangia na wananchi wote.
Naomba niseme kwamba, watu waliokuwa katika chama hiki hawakuwa kama wale watu waliochukua utajiri kutoka kwa waganga wa kienyeji, hakukuwa na masharti ambayo yalionyesha dhahiri kwamba wewe ulichukua utajiri kutoka kwa shetani, yaani si kwamba uwe tajiri lakini usile nyama, uwe tajiri halafu usivae viatu, watu wa dini hii ya kishetani ilikuwa tofauti kabisa, unapopata utajiri, kitu cha kwanza ni kusaidia watu.
Sikuamini kama ningemkuta mahali hapo, aliaminika sana, alipendwa, wakati nikiwa nikijiuliza maswali mengi, mara yule mkuu wetu akakohoa kidogo, macho yangu nikayarudisha kwake na kuanza kumwangalia.
“Nimesikia kwamba tuna mwanachama mpya,” alisema kiongozi yule huku akituangalia.
“Ndiyo mkuu!” aliitikia mwanaume mmoja.
“Aje hapa mbele!” alisema.
Nikabaki nikijiuliza kama nilikuwa mimi au alikuwa akizungumziwa mtu mwingine. Wakati nikijiuliza, ghafla nikajikuta nikisimama na kuanza kuelekea kule mbele.
Naweza kusema haikuwa amri yangu kwani bado niliendelea kujiuliza ila kuna hiyo nguvu iliyonitoa pale na kuelekea mbele. Nilipofika hapo, nikasimama na kuanza kumwangalia mtu huyo ambaye wote humo ndani walimuita mkuu.
“Unaitwa nani?”
“Zakia…”
“Ulishawahi kusikia kuhusu sisi?” aliniuliza.
“Hapana! Si mtu wa kukaa sana na watu, ila nilijikuta nikiletwa huku,” nilimjibu huku nikimwangalia kwa macho yaliyokuwa na hofu tele.
“Kwa nini upo hapa?” alinitupia swali.
“Nimeletwa tu.”
“Ulikuwa ukihitaji utajiri! Si ndiyo?” aliniuliza.
“Ndiyo!”
Mwanaume yule akabaki kimya, aliendelea kuniangalia kwa macho yaliyokuwa na shauku ya kutaka kufahamu mengi kutoka kwangu. Nilibaki nikimwangalia tu.
Kwa kweli nilijiona kama kuwa na nguvu mpya, nilijikuta nikipewa nguvu ambayo sikujua ilikuwa wapi. Nikiwa hapo, nikaanza kupata maono ya ajabu kabisa kwamba nilikuwa tajiri mkubwa mno, kila mtu alikuwa akiniangalia kwa heshima, utajiri ambao nilikuwa nao ulimtetemesha kila mtu.
Sikujua maana ya maono hayo, nikawaza kwamba labda ndivyo itakavyokuwa hapo baadaye, hivyo nikayapuuzia. Baada ya kuniangalia kwa sekunde chache, akachukua kitu fulani, kilikuwa kama chuma fulani, akaniwekea kifuati mwangu na kusema kwamba huo ulikuwa ni utambulisho kwangu kwamba nilikuwa mwanachama kamili wa hiyo dini.
“Utataka tukufanyie nini kingine?” aliniuliza.
“Niwe tajiri!”
“Wewe ni tajiri tayari!”
“Zaidi ya hivi nilivyo!”
“Hakuna tatizo! Kuna kingine?” aliniuliza.
“Ninataka heshima pia.”
“Umepata. Kingine?”
“Ninataka kulindwa, niwe na ulinzi mkubwa.”
“Umepata!”
Nilimwambia mahitaji yangu yote, baada ya kumaliza akaniambia kwamba nilitakiwa kujumuika na wenzangu, nikafanya hivyo na wote kunipongeza kwa uamuzi mzuri nilioufanya wa kujiunga nao.
Tulikaa huko kwa saa moja na ndipo tukaondoka, moyo wangu ulikuwa na furaha tele, sikuamini kama ningepata yote yale niliyoyaomba ndani ya kanisa lile, usiku huo, sikulala, nilibaki nikiwa na furaha tele.
Utajiri unachanganya, unapoushinda umasikini unajiona kuwa mshindi mkubwa, mshindi zaidi ya watu wote katika dunia hii. Nilibaki nikiyafikiria maisha yangu yaliyopita, niliendelea kuwa katika hali hiyo mpaka saa tisa alfajiri, manyunyu ya mvua yakaanza kusikika kutoka nje, nikachukua shuka na kujifunika.
“Ngo ngo ngo…” nilisikia geti likigongwa.
Kwanza nilishtuka, sikujua ni nani alikuwa akigonga, nikatoka kitandani na kuangalia nje kwa kutegemea kwamba mlinzi angesikia, cha ajabu, mlinzi hakusikia kabisa kwani alikuwa amelala.
Nikatoka na kwenda nje, ghafla, hata kabla sijalifikia geti na kulifungua, watu waliokuwa wakigonga, nikashtukia wakiwa wameingia ndani, mikononi walishika mfuko mkubwa mweusi, walisimama wima huku wakiniangalia, mvua kubwa ikaanza kunyesha lakini hawakutoka hapo kwenye mvua, wakanitaka na mimi niwafuate. Kwa kweli, niliogopa mno.
“Nyie ni wakina nani?” niliuliza huku nikiwa na hofu moyoni mwangu.
Watu wale ambao walikuwa wawili hawakujibu swali hilo, walikuwa kimya huku wakiendelea kuniangalia, nilibaki kuwa na maswali mengi, wale walikuwa wakina nani na walitoka wapi.
Walichokifanya ni kuanza kupiga hatua kunifuata, kwa kweli niliogopa mno hivyo kuanza kurudi nyuma na kuufunga mlango. Nilijua kwamba siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho wa maisha yangu, akili yangu iliniambia kwamba watu wale walikuwa majambazi ambao waliingia na kutaka kuniibia.
Sikuuona msaada wowote wa mlinzi kwani wakati watu hao wakiingia, yeye alikuwa amelala kitu kilichonifanya kukosa amani, wakati mwingine nikahisi kwamba hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya kufa.
“Ngo…ngo…ngo..” nilisikia mlango ukigongwa.
“Nyie ni wakina nani?” niliuliza huku nikitetemeka.
“Ngo…ngo…ngo..” nilisikia tena ukigongwa.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa mahali hapa.