Jiwe hilo kubwa lilizidi kushuka na kumkandamiza Neema kifuani, alilia akimwomba Nicholaus msaada lakini alishindwa afanye nini kumsaidia Neema matokeo yake alianza kulia!
Neema hakusema kitu tena baada ya jiwe hilo kumgandamiza kifuani, tayari alikuwa amekufa! Nicholaus alimpapasa mdomoni na kugundua alikuwa hahemi tena, ingawa hata yeye alijua angekufa muda si mrefu sababu ya kukosa hewa au njaa bado aliumia moyoni kuona mtu aliyejitolea kuokoa maisha yake akifa! Alimshika kichwani na kuanza kumuombea akimshukuru Mungu kwa kazi aliyoifanya na bado alimuomba Mungu amnusuru na kifo kilichokuwa mbele yake ili siku moja aonane na dada yake Victoria.
Pamoja na kumuomba Mungu amuokoe na kifo kichwani mwake bado wazo la kusakwa liliendelea kuwemo! Alijua mpaka wakati huo bado alikuwa akitafutwa na ingawa alinusurika kifo cha risasi kimiujiza bado adhabu hiyo ilikuwa ikimsubiri kama tu angetiwa mikononi na serikali ya Iran iliyopiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zote.
Lawama zake nyingi alizitupa kwa Samwel na AbdulAzizi waliomdanganya na kutaka kumtumia kusafirisha madawa ya kulevya kwenda katika nchi hatari kama Iran, mpaka wakati huo hakuamini kama aliondoka Tanzania kumkimbia dada yake bali kwenda kutafuta maisha bora zaidi baada ya yeye na dada yake kudhulumiwa na ndugu mali zote walizoachiwa na marehemu wazazi wao.
“Kama si tetemeko la ardhi kutokea hivi sasa ningekuwa maiti, sijui Victoria angefahamu vipi kuwa nilikufa!” Aliwaza Nicholaus
Ghafla mawazo ya kijasiri yalimwijia kichwani mwake na kujikuta akipata nguvu za ajabu, hakuwa tayari kufa katika shimo hilo tena, alitaka kutoka nje lakini alishindwa angetoka vipi! Mawazo hayo yalimfanya ajikute akipiga kelele kwa nguvu kuomba msaada lakini sauti yake haikufika mbali kwa sababu ya kuzungukwa na udongo sehemu zote!
Hakuchoka kufanya hivyo bali aliendelea kupiga kelele zaidi na zaidi akiamini hatimaye sauti yake ingesikiwa na labda angejitokeza mtu akachimba juu na kumtoa ndani ya shimo alilokuwemo!
*************
Hakuna msaada uliojitokeza na kwa siku nne mfululizo Nicholaus aliendelea kukaa ndani ya shimo hilo akisubiri kifo chake! Maiti ya ilikuwa pembeni mwake ikiendelea kuharibika! Ilivimba na kutoa harufu kali kupita kiasi, hewa yote iliyokuwemo ndani ya kishimo kidogo alichojificha ilijaa harufu lakini Nicholaus aliizoea harufu hiyo na kuna wakati hakuisikia kabisa.Ilikuwa si rahisi hata kidogo kuamini maiti iliyokuwa imevimba kiasi hicho ilikuwa ya msichana mrembo Neema.
Ilikuwa si rahisi kufahamu upi ulikuwa mchana na upi ulikuwa usiku ndani ya shimo alilokuwa, kwa siku zote nne aliendelea kupiga kelele bila kukoma akijua msaada ungepatikana, njaa kali pamoja na kiu ya maji ilimsumbua kiasi kwamba hadi siku ya tano ilipofika bila kunywa maji wala kula hakuweza tena kupiga kelele, nguvu zilimwishia akalala pembeni ya maiti ya Neema iliyovimba na kusubiri kifo chake! Alikuwa na uhakika asilimia mia moja angekufa.
Nicholaus aliendelea kukishika kipande cha noti mkononi mwake kilimkumbusha mengi kuhusu dada yake na hata nchi yake Tanzania! Ni fikra juu ya dada yake na pacha wake Victoria zilizomfanya azidi kulia machozi ya huzuni, Nicholaus alisikitika kufa akiwa mbali na Tanzania, kilichomuumiza zaidi ni kuwa dada yake asingeiona wala kuigusa maiti yake na angeendelea kuamini alikuwa hai!
Alitamani mambo yabadilike na arudi tena Tanzania kama ingetokea hivyo aliuahidi moyo wake kutofanya makosa kama aliyoyafanya maishani mwake, angeishi na dada yake siku zote za maisha yake. Mawazo juu ya dada yake yalimtia huzuni kupita kiasi na alijilaumu kwa kitendo cha kuondoka na kumwacha!
Kila kumbukumbu za siku ya mwisho uwanja wa ndege wa Kilimanjaro zilipomwijia alimwona dada yake akilia na kumwomba lakini alimpuuza akimwona ni msichana asiyejua kitu kumbe Mungu alishamuonyesha kila kitu kilichokuwa mbele ya kaka yake, Nicholaus alilia zaidi.
Mpaka wakati huo Nicholaus hakuwa jinsi yoyote ya kujiokoa zaidi ya kusubiri kifo chake mwili wake ulizidi kupoteza nguvu sababu ya njaa kali aliyokuwa nayo mpaka kiasi cha kushindwa hata kufungua macho na mdomo wake.
*********************
Nchi ya Iran ilikuwa imekumbwa na pigo kubwa, hapakuwahi kuwepo na tetemeko kubwa la ardhi kiasi hicho katika muda wa miaka ishirini kabla, idadi ya watu wasiopungua elfu moja waliaminika kufa na wengine zaidi ya elfu tatu walikuwa majeruhi.
Serikali ya nchi hiyo ilitangaza siku tatu za maombolezo wakati shughuli za uokoaji zikiendelea kwa nguvu zote. Hali ilishatulia na tetemeko halikuwepo tena, mashirika mbalimbali ya kupambana na majanga yalikuwa yakifukua ardhini kuondoa udongo na kuwaokoa watu waliofunikwa na udongo. Maiti nyingi zilitolewa na watu wachache walikuwa hai.
Shughuli ya uokoaji iliendelea usiku na mchana kwa siku nne, siku ya tano serikali iliamua kusitisha zoezi hilo kutoa nafasi kwa mazishi ya kitaifa kufanyika! Maiti nyingi zilizikwa katika makaburi ya pamoja, mamia kwa maelfu ya wananchi wa Iran walihudhuria mazishi hayo, watu ambao hawakuokolea katika siku hizo tano walihesabika kama wafu na kuhesabika wamezikwa hukohuko ardhini!
*************
“Hawa hapaaaaa!” Alipiga kelele mmoja wa watu waliokuwa wakifukua chini ya ardhi kwa kutumia vijiko vya katapila baada ya kuona miili miwili ya watu! Mmoja ukiwa umevimba sana na uligandamizwa na jiwe kubwa. Watu wote wakiwemo mzee Mohamed walikimbia mbio hadi mahali kelele hizo zilipotokea.
“Sio wenyewe lakini hebu watoeni tu, huyo mmoja anaonekana amekufa lakini huyu mtoto bado hajafa mkimbizeni hospitali haraka ikiwezekanavyo!” Alisema mzee Mohamed na jambo hilo lilifanyika kwa haraka.
Maiti ilichukuliwa na kupelekwa chumba cha maiti cha hospitali ya Tehran Muslim Agency na mwili wa kijana ulipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa matibabu!
“Huyu kijana hana tatizo jingine zaidi ya njaa! Lakini amewezaje kuishi huko chini bila hewa kwa siku zote hizi?”
“Hata mimi nashangaa sana au kulikuwa na matundu yaliyopitisha hewa?”
“Inawezekana!”
Waliendelea kuongea madaktari huku wakimwekea kijana huyo dripu za maji ya chakula katika mishipa yake na baada ya kugundua alikuwa ameishiwa sukari mwilini mwake pia aliwekewa mashine ya hewa safi ya oxygen li kumsaidia katika kupumua. Ngozi yake ilikuwa bluu kwa sababu ya kukosa hewa safi!
“Yuko cynotic kabisa!” Alisema daktari mmoja akimaanisha kuwa ngozi ya kijana huyo ilikuwa ya bluu sababu ya kukosa oxygen.
“Lakini hii oxygen anayopata itamsaidia!”
“Sijui huyo mtoto mwenyewe ni raia wa wapi? Anaonekana kama kuwa raia wa nchi ya Kiafrika!”
“Au ndiye alikuwa apigwe risasi sababu ya madawa ya kulevya kabla ya tetemeko?” alisema daktari mmoja huku akimwangalia kijana huyo usoni kwa makini!”
“Hapana si huyu!” Alisema daktari mwingine huku akimgusagusa kijana huyo usoni.
“Lakini anaonekana ni yeye subiri uvimbe ukipungua usoni kwake tutagundua sura tofauti na hii!”
“Inawezekana lakini sidhani kama ni huyu!”
“Hivi ingekuwa vipi kama mzee Mohamed asingejitolea kutafuta maiti za mke na mtoto wake?”
“Angekufa nasikia hata maiti ya mke na mtoto wake hajazipata ilikuwa bahati ya kijana peke yake!”
****************
Kwa siku saba kamili kijana huyu aliendelea kulala kitandani bila kujitambua, maji ya dripu yaliendelea kuingia katika mishipa yake na kumtia nguvu mwilini taratibu, kila mtu alikuwa na matumaini angepona na kurejewa na fahamu lakini haikujulikana ni lini, madaktari walishasahau kumchunguza sura tena walibanwa na kazi nyingine.
Siku ya nane usiku wa manane kama namba yenyewe ilivyo kijana huyo alishtuka na kufumbua macho yake, alijikuta yu peke yake kitandani. Alikuwa ndani ya chumba ambacho hakukielewa, aliangaza macho yake huku na kule na kugundua mahali alipokuwa palikuwa ni hospitalini.
Alishindwa kuelewa alikuwa pale kwa sababu gani, dakika thelathini baadaye alipojaribu kuvuta kumbukumbu zake vizuri alikumbuka kila kitu kilichotokea na kufumba macho kwa woga! Kimbukumbu zilizomwijia zilionyesha picha yake akiwa amefunga kwa kamba kwenye mti na watu wenye bunduki walisimama mbele yake wakisubiri amri kutoka kwa mkuu wao ili wammalize kwa risasi.
Kumbukumbu zilizidi kumiminika akalikumbuka hata jina lake kuwa aliitwa Nicholaus na kumwona mkuu wao akihesabu namba na wenye bunduki walisubiri namba tatu itajwe ndipo wakamilishe kazi yao, kabla mkuu hajaifikia namba hiyo ardhini ilianza kutetemeka na maghorofa yalianza kuyumba na mengine kuanguka yakiwagandamiza watu.
Watu walikimbia huku na kule na kumwacha Nicholaus peke yake, baadae alimwona msichana mwafrika akija mbio na kufungua kamba walianza kukimbia naye lakini mbele ardhi ilipasuka na wakatumbukia!
“Wasalimie Tanzania ukiokolewa” Aliyakumbuka maneno ya mwisho ya msichana huyo kwake.
Nicholaus alilia machozi hapo hapo kitandani hakukumbuka ni namna gani alitolewa katika shimo alikokuwa amebanwa na kujikuta hospitali. Huo ulikuwau ni kama muujiza na alipousikiliza vizuri mwili wake aligundua ulikuwa na nguvu nyingi kuliko kawaida! Alikuwa na uwezo wa kujiokoa.
“Wakinikuta hapa ni lazima watanikamata na kunipiga risasi tena! Ni lazima niondoke!” aliwaza Nicholaus na kuanza kuangalia kila pembe ya chumba, watu wote ndani ya chumba hicho walikuwa wamelala fofofo! Hata muuguzi ofisini alikuwa amelala juu ya meza!
Aliuona huo kuwa wakati muafaka wa kuondoka na kuokoa maisha yake! Alipoangalia saa ya ukutani iliyokuwemo wodini ilionyesha saa tisa na nusu ya usiku ulikuwa ni usiku mkubwa mno kwake kutoroka kwani hakufahamu sehemu yoyote katika nchi ya Iran lakini hakuogopa.
Asingeweza kusubiri hadi asubuhi huku akijua angeingia mikononi mwa polisi na kuuawa kikatili! Alizichomoa sindano zilizokuwa katika mishipa yake na akaufyatua mfuniko wa mashine ya oxygen uliokuwa mdomoni mwake na taratibu alishuka na kuanza kutambaa chini kwa chini kuelekea mlangoni hakuna mtu aliyemwona alikuwa ameamua kuondoka hospitalini kwenda kusikojulikana.
Nje ya wodi alinyanyuka na kuanza kutembea akiiacha wodi na kupita chini ya miti mingi ya Misonobari iliyokuwepo katika mazingira ya hospitali hiyo, hali ilikuwa kimya na ya kiza! Katika muda huo wa usiku karibu kila mtu alikuwa usingizini, Nicholaus alimwomba Mungu asionekana mtu yoyote kwani kama jambo hilo lingetokea angekuwa amechungulia kaburi tena!
“Lakini kama Mungu ameniokoa na matatizo yote yaliyopita kwanini asininusuru na leo?” aliwaza Nicholaus huku akiingiza mkono mfukoni mwa suruali aliyovaa lengo likiwa ni kukitafuta kipande cha noti alichokwenda nacho kila mahali lakini hakukiona!
Hakutaka kupoteza muda wala kufikiria mara mbili, kwake kupoteza kipande hicho cha noti ilikuwa ni sawa na kifo cha dada yake, alianza kukimbia mbio kurudi wodini bila kuwaza angekamatwa au la! Alijua angeweza kukamatwa lakini hakujali, alipoikaribia wodi alianza kutambaa tena.
“Haiwezekani, siwezi kuondoka hapa bila Victoria wangu!” Alisema kwa sauti ya chini kwake kipande hicho cha noti kilikuwa ni sawa na dada yake mpendwa kukiona ilikuwa ni sawa na kumwona Victoria.
Nicholaus aliingia wodini na kuendelea kutambaa hadi kitandani kwake ingawa hakuwa na uhakika kama nguo zake zilikuwepo alijikuta akifungua kabati lililokuwepo pembeni mwa kitanda chake! Hakuamini alipoona suruali pamoja na shati lake vikiwa vimefungwa pamoja kwa kamba!
“Alhamdullilah” Alijikuta akitamka neno la Kiarabu bila kutegemea kwa furaha aliyoipata, alichukua nguo zake na kutambaa tena hadi nje bila kugundulika ambako alivua nguo za hospitali na kuvaa nguo zake.
Alipoingiza mkono ndani ya mfuko wa kulia ya suruali yake alikikuta kipande cha noti! Furaha aliyoipata ilikuwa haielezeki, ilikuwa ni kama kukutana na Victoria ana kwa ana, Nicholaus tayari kupoteza chochote katika maisha yake lakini si kipande hicho cha noti! Alikipiga busu na kuendelea na safari yake kutoka nje ya eneo la hospitali.
Hospitali ya Tehran Muslin Agency ilimilikiwa na shirika la Kiislam na ilikuwa na chuo kikuu cha mifugo na ilijishughulisha na utafiti mbalimbali wa wanyama, hasa mamba, ilikuwa na bwawa kubwa lililofuga mamba wengi pembeni mwa chuo hicho, watu walizuiliwa kupita katika maeneo hayo sababu ya usalama wao, watu zaidi ya kumi walishadumbukia katika bwawa hilo na kuliwa na Mamba katika kipindi cha miaka kumi na tano kabla! Nicholaus alitembea taratibu kuelekea lilikokuwa bwawa hilo kwa sababu ya giza hakukiona kibao kilichozuia watu kupita maeneo hayo!
Mita kama hamsini kulifikia bwawa alishtukia kundi kubwa la mbwa wakija huku wakibweka nyuma yake, walikuwa wakimfukuza yeye, aliogopa na kuanza kukimbia kwenda mbele bila kujua kulikuwa na bwawa la Mamba! Ghafla alishangaa mguu yake wa kulia ulibodumbukia ndani ya bwawa na kuanguka majini! Alisikia mlio wa maji ukija mbio kuelekea mahali alipokuwa, ni kama kitu kilikuwa kikimfuata lakini hakikutoa sauti! Suruali na shati lake vilikuwa kama vimenasa kwenye kitu kwa nyuma.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.