KIGOMA-2000
Jina langu naitwa Vegasi Mbwana marafiki walipenda kuniita Vega, ni mzaliwa wa Kigoma Ujiji, nina miaka thelathini na tatu ni baba wa watoto wawili Hussein na Khadija, japo ni mwenyeji wa Kigoma ila kwa sasa naishi Jijini Dar wilaya ya Kinondoni eneo moja linaitwa Mwananyamala komakoma huko naishi mimi, mke wangu Latifa Binti Kassim Bakari pamoja na wanetu wawili.
Nilikuwa natoka katika familia yenye maisha ya kati yanii si maisha ya kimasikini wala siyo maisha ya kitajiri, mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne nikiwa ni mwanamume pekee wadogo zangu wote wakiwa ni wasichana naweza nikasema mimi ndio nilikuwa tegemeo kubwa la familia siku za usoni.
Nikililifahamu jambo hilo ilikuwa ni moja ya motisha kukazana katika masomo yangu nikielewa mimi ndio tegemeo la familia.
Juhudi zangu katika masomo zilinifanya niwe miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakitazamwa na uongozi wa shule hata wanafunzi wenzangu pia, kama miongoni mwa watu watakao faulu bila zengwe.
Uwezo mzuri kitaaluma ulinipatia marafiki wengi ukichangia na ule ukarimu wangu ukiachilia mbali kipaji changu cha usakataji kabumbu kipaji kilicho niongezea umaarufu mkubwa kabisa kila kona ya mji wa Kigoma.
Mfanano wa majina kati yangu na mchezaji mahili wa klabu ya Liverpool ya nchini Wingereza ajulikanaye kama Patric Vegas ilinifanya kuwa mpenzi mkubwa wa mchezaji huyo na kumfanya kuwa role model wangu, hatua iliyo pelekea kuwa mchezaji hatari ninaye chipukia, mwenye ndoto za soka la kimataifa.
Nathubutu kusema nilikuwa maarufu kule Kigoma kuliko hata mkuu wa wilaya ya Kigoma
Fauku ya hayo, masiku kadhaa nilifanya mtihani wangu wa mwisho wa kidato cha sita na kama ilivyo tarajiwa na watu wengi nilikuwa ni moja kati ya wahitimu wa kidato sita wa shule ya sekondari ya Newman, niliye faulu kwa alama za juu kabisa na kubahatika kuchaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salam nikitazamia kuanza masomo ya shahada ya kwanza ya ualimu.
Nakumbuka Ilikuwa ni majira ya saa moja kama na nusu hivi za jioni, mimi na marafiki wachache, tulikuwa katika hafla ndogo katika ukumbi maarufu pale Kigoma, kizota pub, ilikuwa ni sherehe ya kusherehekea ushindi wa timu yetu ya ‘Joy football club’ kupanda daraja na kuwa miongoni mwa timu zitakazo ingia katika ligi kuu ya hapa nchini, ligi iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Ilikuwa ni timu imilikiwayo na shirika moja la watu wa Marekani lijulikanalo kama joy the harvest, shirika ambalo linajihusisha na maendeleo ya jamii kiuchumi, afya na kiroho ambalo lilkuwa chini ya kanisa la katoliki,parokia ya Kigoma Ujiji, ilikuwa ni sherehe ndogo tu iliyo jumuisha wachezaji wa timu, makocha, viongozi wa timu, na mashabiki wachache.
Naikumbuka sana siku hiyo, siku iliyo badili dira nzima ya maisha yangu, siku isiyo weza kufutika akilini mwangu milele na milele, siku iliyo nibadili kutoka katika ubinadamu na kuwa kiumbe wa ajabu kabisa.
Sherehe ilienda mpaka majira ya saa saba usiku kisha hafla ile ikahitimishwa na mgeni rasmi Mheshimiwa Regina Olemunzu huyu ni Afsa ustawi wa jamii wa Manispaa ya mkoa wa Kigoma Ujiji.
Wachezaji wote tulitoka nje ya ukumbi kabla ya kurudishwa kambini ambako tulitakiwa kukaa tena kwa siku moja kabla ya kuvunjwa kwa kambi na askofu mkuu wa mkoa wa Kigoma Father Mathiasi Festo Mberekelwa na watu kurejea majumbani mwao.
Usiku ulikuwa umekuwa mkubwa, giza lilikuwa nene, miale ya radi ilikuwa ikimulika kila baada ya sekunde tano huku ikifuatiwa na ngurumo kali za radi. Dalili ya mvua kubwa ilionekana.
Pamoja na ukweli kwamba siku hii ilifurahiwa na kila mchezaji wa timu yetu hali ilikuwa tofauti kwangu mie!
Sikuwa katika hali ya kawaida na haikuwa wakati ule ambapo nipo ndani ya basi, rahasha! hali ile ya kutokuwa na raha nilikuwa nayo tangu mwanzo wa sherehe.
Sikuwa ni mwenye furaha kabisa kuna kitu nilikuwa napenda niwe nacho wakati ule lakini ajabu sikujua ni kitu gani.
Kuna wakati katika sherehe niliona kama sherehe ilikuwa ina mapungufu fulani, lakini ungeniuliza ni mapungufu gani bado nisingeweza kuwa na jibu kamili. Kwa lugha ya kueleweka naweza nikasema sikujua nini nahitaji.
‘Nahitaji nini mimi’ nilijuliza akilini huku mawazo yangu yakihamia kwa Nasra, mpenzi mwenye mwenekano wa mwanamke wa urembo.
Lakini wapi. Sikuwa nimemkosa binti huyo japo nilikuwa nampenda mno.
Sasa kumbe nahitaji nini mimi..? niliendelea kujiuliza mwenyewe bila kupata majibu.
Nilishia kuelekeza macho yangu huko nje ambako kulikuwa na giza nene huku anga yote ikimezwa na wingu jeusi la mvua, huku miale ya radi ikimweka kama mwanga wa flashi ya kamera, upepo ikiwa unakusanya takataka nyingi za mtaani na kuzisukuma hovyo kila mahali. Barabarani kukiwa hakuna gari lolote zaidi ya basi letu.
“Yakhee! vipi weye, wajionaje leo, mbona uko hivyo ati?,” nilistushwa na sauti ya Abduli Kareem Babu maarufu kwa jina la Mpemba, mwenyeji wa visiwani Pemba huko Zanzibar, rafiki mchezaji niliyependa kusikia lafudhi ya Kizenji kutoka kwake.
“Unasemaje Mpemba?” nilimuuliza huku nikitabasamu ilhali swali lake nililisikia vema.
“Ati, leo wapatwa na maswahibu gani weye? Mbona huna raha kabisaa? Aliuliza tena, nilijikuta nikitabasamu pasi na kufungua kinywa!
Nikaendelea kupata burudani kwa lafudhi tamu ya lugha adhimu ya Kiswahili.
Lakini kabla sijamjibu lolote Mpemba, mara kulitokea kishindo kikubwa kilichofanya watu wote tutoe sauti kali za kuogofya huku hali ya sintofahamu ikichukua hatamu mule ndani ya basi dogo aina ya la kosta.
Ndani ya nukta chache gari liliacha njia, likawa linaserereka kwa kasi, likijibamiza katika matuta na kuruka juu sentimita kadhaa na kujibamiza tena ardhini, ndani ya gari, kelele za kuogofya za kila aina zilililindima vibaya mno.
Moyo wangu ukalipuka, hofu ikatambaa kifuani mwagu, macho yakanitoka, nikakamatilia kwa nguvu zote mgongo wa siti ya mbele yangu, jasho likiwa linanichuruzika vibaya mno.
“Paaaaaaa” gari lilijibamiza katika tuta huku likizidi kuserereka kwa kasi nilitupa macho mbele kwa dereva nikaona jamaa akiwa anapiga makelele hovyo huku akiwa ameng’ang’ania usukani kwa nguvu.
Sasa tulikuwa katika mteremko mkali kutokea pale Mwanga kwa mchaga kuelekea katika Kituo cha treni Kigoma.
“Ooo! Mungu wangu uko wapi wewe Mungu wewe!..aagh” nilijikuta nikibwabwaja kibwege macho yamenitoka, hadi wakati huo yote hayo yanatokea, hakuna aliyekuwa anajua nini chanzo cha yote hayo!
Ingawa akili yangu ikakiri kuwa mwenye majibu ya yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya gari kwa muda huo ni dereva peke yake.
Gari lilienda mrama yule dereva mpiga makelele akiwa ameng’ang’ania usukani kwa nguvu na wakati huo tukawa usawa wa hoteli ya Mwaka Hill.
Eneo lile pembezoni mwa barabara kulikuwa na maporomoko marefu, ambayo licha ya urefu wake pia yalikuwa na upana mkubwa wa mita kama nne ama nne na nusu, ndani ya mtaro huo ambao pia nadhani siyo vizuri nikiuita mtaro labda ni sahihi kusema maporomoko.
Mara nyingi maporomoko hayo yalikuwa yakitumika kwa kutiririshia maji taka kutoka mitaa ya Mji Mwema.
Yule dereva aliyekuwa amepatwa na wazimu wa kupiga makelele hovyo huku mikono yake ikiwa imekamatilia kwa nguvu usukani wa gari, katika hali isiyo ya kawaida alilipeleka gari lile katika maporomoko yale.
“Hehe..hehe..hohooooh, huyu dereva ana wazimu nini,.sasa nini..hii..huku” nilitoa miguno yenye kitetemeshi huku watu wengine pia wakitoa mayowe ya kuogofya. “vuuuuuuu…paaaaaaaa” gari lilitumbukia vibaya na kujibamiza kwa nguvu ndani ya maporoko makubwa ya maji taka!.
Hakuna kilichosalia.
Macho yangu yaligubikwa na giza zito huku maumivu makali yakitambaa kichwani mwangu kwani nilijibamiza vibaya katika vyuma hapo sikujua tena kilichoendelea duniani..
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.