×

Hadithi ya Shigongo: Dimbwi la Damu-13

Shabir alimpiga Victoria kwa  
mateke na ngumi bila 
huruma, akilalamika kitendo cha  Victoria kuitoa mimba ya mtoto wake! Victoria alilia akiomba msaada lakini hakuna mtu aliyejitokeza kumsaidia. Baadaye alimvuta kwenda bafuni ambako alimwonyesha  kama kipande cha nyama   na kitoto kidogo kilichokuwa katika sinki la choo! “Wee kenge! Umeua mtoto wangu kweli? Nikupe adhabu gani?”

“Nisamehe baba sikuwa na jinsi  nimefanya hivi kwa sababu sikutaka kumuudhi Leah, amenisaidia sana katika maisha yangu!”

“Leah? Ndio nani unayemwogopa  kiasi cha  kufikia kuua mtoto wangu? Leo utanikoma na humu ndani hulali, huli mpaka utakufa kwa mateso!”  Alisema Shabir  kwa sauti nzito ya kukwaruza na kuanza kumvuta     hadi nje ya nyumba  alimtupa na kufunga mlango nyuma yake na  kurudi  hadi chumbani ambako alichukua mzinga wa pombe kali na kuumimina wote mdomoni! Alitaka alewe alale bila kusikia kilio cha Victroria nje ya nyumba.

Victoria alilala ardhini akilia huku damu zikiendelea kumtoka, hakupata msaada wowote hadi asubuhi mlango ulipofunguliwa na Shabir kutoka nje! Hakumsaidia kitu chochote zaidi ya kumwangalia kwa jicho la dharau  kisha mlango wa  nyumba na kuingia ndani ya gari lake  kuondoka kwenda kazini.

“Wewe kipofu! Leo utashinda  hapo  na kifo chako kitakukuta hapohapo!”

“Baba nisamehe!” Victoria aliendelea kuomba msamaha.

Kweli siku hiyo Victori alishinda nje bila kula chakula na  Shabir  aliporudi kutoka kazini jioni hakumruhusu kuingia ndani ya nyumba yake wala kumpa chakula, alilala nje   akinyeshewa na mvua na kuumwa na mbu wengi! Kwa siku tatu mfululizo alilala nje bila kula  na Shabir hakujali kila siku alimwambia kikatili kuwa alisubiri kifo chake ili amfukie nyuma ya nyumba.

Tumbo  lilimuuma sana na  joto la mwili wake lilipanda kupita kiasi  alitetemeka  kwa baridi, maumivu ya tumbo aliyokuwa nayo hakuwahi kufikiria kama yapo duniani!  Mara nyingi aliumwa tumbo akiwa mtoto lakini hata siku moja hakuugua tumbo la mateso kama  hilo.

Hakuwa na la kufanya aliamini kweli kifo chake kilikuwa kimefika, alishangaa ni kwanini Shabir alikuwa na roho mbaya kiasi hicho! Pamoja na kumlilia ampeleke hospitali bado Shabir hakujali akidai Victoria aliua hivyo ilikuwa ni lazima na yeye afe.

*************************

Nicholaus Hospitali:

Hali yake ilikuwa nzuri kidogo ingawa usoni alikuwa ameungua sana! Uso wote  na sehemu ya mbele ya tumbo ulibabuka lakini macho yake yalikuwa salama kabisa, kwa hilo alimshukuru Mungu! Mzee Mohamed alikuwa amekaa pembeni mwa kitanda chake, ni siku hiyo ndiyo walipata muda mrefu zaidi wa kuongea.

“Tafadhali nieleze ni kitu gani kilikupata kijana!”Mzee Mohamed alimuuliza Nicholaus.

“Ni habari ndefu sana, itachukua muda mrefu sana kuielezea!”

“Nieleze tu nielewe!”

“Nilizaliwa nchini Tanzania, katika familia ya mfanyabiashara aliyeitwa Patrick, tulizaliwa mapacha yaani mimi na dada yangu  niliyemwacha Tanzania. Tukiwa watoto wazazi wetu walifariki kwa ajali ya gari  lao kugongwa na treni,  pacha wangu pia alikuwemo katika ajali hiyo na kuambulia upofu!” Nicholaus alisimulia kila kitu mpaka jinsi alivyojikuta akibambikiwa madawa ya kulevya sababu ya kutamani kwenda nje ya nchi.

“Baada ya kukamatwa ulifanywa nini?”

“Nilipelekwa kwenye kiwanja cha wazi ambako nilifungwa kwenye mti ili nipigwe risasi maana sheria ya nchi yenu wafanyabiashara wa madawa hupigwa risasi mbele ya halaiki ya watu!”

“Sasa ilikuwaje ukaokoka?”

“Tetemeko!”

‘Tetemeko lilifanya nini?”

“Kabla hawajanipiga risasi lilitokea tetemeko la ajabu na ardhi ilipasuka, maaskari wote waliingiwa na woga na kujikuta wakitupa bunduki zao na kuniacha nikiwa nimefungwa katika mti ili nife kwa tetemeko!”

“Uliokokaje?”

“Msichana mmoja wa Kitanzania aliyefanya kazi katika  ubalozi wa Tanzania nchini Iran, alikuja na kunifungua kutoka mtini wakati tetemeko likiendelea, baada ya kufunguliwa   tulikimbia  tukijaribu kujiokoa lakini mbele    ardhi ilipasuka na sote tukadumbukia shimoni na kufunikwa  na udongo kwa juu! Tukiwa ndani ya shimo hilo jiwe kubwa lilimkandamiza msichana aliyeniokoa na kufa, nilikaa kwa siku  chini ya ardhi kwa siku nne ndipo nikaokolewa.

Nicholaus alipofika sehemu hiyo mzee Mohamed alifumba macho yake na kuonekana kuvuta kumbukumbu zake na alipofumbua macho yake alimwangalia Nicholaus usoni kwa  makini.

“Nimekukumbuka!”

“Uliniona Tehran wakati nataka kupigwa risasi siyo?”

“Hapana nilikuona siku ulipookolewa  kutoka katika udongo!”

“Ulikuwepo siku hiyo?”

“Ni mimi niliyefanya kazi ya kukuokoa baada ya serikali kusitisha zoezi hilo siku ya tatu!”

“Nisaidie baba sitaki kufa!”

“Usiwe na shaka  nitakusaidia!”Alisema mzee Mohamed na kuichomoa simu yake ya mkononi kutoka katika kanzu yake na kuponyea namba fulani dakika kama kumi baada ya kupiga simu hiyo kijana mmoja aliingia mbio hadi chumbani.

“Inuka twende kijana!”

“Wapi?”

“Wewe nifuate tu!”

Nje waliingia ndani ya gari dogo jeupe liliondoka kwa kasi  ya ajabu kama lilikuwa likitorosha kitu na aliyetoa amri ya kwenda kwa kasi alikuwa mzee Mohamed mwenyewe. Moyoni kwa Nicholaus kulijawa na wasiwasi mwingi, alihofia sana biashara ya kuchunwa ngozi! Hakumfahamu vizuri mzee Mohamed na hakuelewa alikokuwa akipelekwa.

“Baba mnanipeleka wapi?”

“Ninajaribu kukuokoa kwani ninajua wazi kuwa utatafutwa!”

Kilomita kama tano hivi mbele gari lilisimama  mbele ya ngome kubwa na ndefu na nje ya ngome hiyo kulikuwa na   idadi kubwa ya walinzi   waliovaa magwanda ya kijeshi wote  wakiwa na bunduki mikononi mwao!  Walilipigia saluti mbele ya gari na lango lilifunguliwa, Nicholaus alishangazwa  na heshima ambayo mzee Mohamed alipewa!

“Karibu Nicholaus hapa ndipo nyumbani kwangu nikiwa  visimani!”

“Ahsante mzee!” Alijibu Nicholaus na wote waliingia ndani wakifuatana,  ndani  walikuta walinzi  wengine wasiopungua hamsini wakiwa mbele ya lango la ukuta mwingine!  Walilipiga saluti gari na mzee Mohamed alitingisha kichwa! Walipita  kuta kubwa   tatu ndio wakalifikia    jumba la kifahari aliloishi mzee huyo tajiri!

“Unaishi hapa na nani?”

“Nilikuwa niikiishi  hapa na mke wangu lakini haitakuwa hivyo tena!”

****************

Mzee Mohamed alimtafutia daktari wa kumtibu mpaka   vidonda vyake vyote vikapona  na kuacha  hali  ya kubabuka   usoni ambayo daktari alisema angebaki nayo maisha yake yote na pia kulikuwa na makovu makubwa.

Alipopona mzee Mohamed alimpa kazi  ya umesenja, akawa anafuata barua za kampuni posta na kuzisambaza!  Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake ya kwanza katika kampuni ya  Gulf gas  limited iliyomilikiwa na mzee Mohamed mwenyewe!

Hali ya kubabuka usoni ilimfanya Nicholaus ajulikane sana miongoni mwa wafanyakazi wenzake kwa sababu hapakuwa na mtu mwingine mwenye sura ya aina hiyo, lakini si sura  peke yake iliyompa umaarufu bali pia uchapakazi! Nicholaus alifanya kazi yake  vizuri na kwa uaminifu kiasi kwamba baada ya miezi sita ya kazi hiyo mzee Mohamed aligundua juhudi yake na  kumpandisha cheo.

Alimfanya  ajifunze udereva wa magari na alipohitimu miezi mitatu baadaye  akawa dereva wake  mwenyewe, alimpenda kupita kiasi na  alizunguka naye kila mahali na waliishi  wawili ndani ya nyumba yao. Maisha ya Nicholaus tayari yalishakuwa mazuri lakini siku zote hakumsahau dada yake! Bado alikitunza kipande cha noti  walichogawana  akiamini ipo siku   wangekutana wakiwa hai na kukiunganisha kama walivyokubaliana!

“Ipo siku nitakuja kwenda Tanzania kumfuata dada yangu najua anateseka sana na roho inaniuma kupita kiasi!”

Visima vya mzee Mohamed  vilikuwa  ndio visima vilivyoongoza kwa kutoa mafuta mengi zaidi katika nchi   za Ghuba na mafanikio hayo yote yalikuja  kutokana na uchapaji kazi aliokuwa nao mzee Mohamed mwenyewe!  Pamoja na kuwa na umri wa miaka 65  bado alifanya kazi  kwa nguvu kupita kiasi jambo lililowatia morali wafanyakazi wake.

 

**********************

Ilikuwa ni siku ya Jumapili ya 
mwisho wa mwezi wa tisa! Mzee Mohamed na Nicholaus walikuwa ndani ya  gari 
wakitoka visimani   kurejea nyumbani  baada ya kazi ngumu, siku hiyo mzee Mohamed alikuwa akiendesha  gari mwenyewe na Nicholaus alikaa upande wa abiria.

Ndani ya gari kulijaa vicheko wakiongea hili na lile, kifupi walikuwa marafiki wakubwa! Ghafla Nicholaus alishtuka kuona gari linaacha njia kuelekea porini, alipomwangalia mzee Mohamed  aliona ametupa shingo yake pembeni!   Kwa haraka kabla gari halijadumbukia mtaroni Nicholaus aliudaka usukani.

“ Baba! Baba! Baba! Vipi?” Aliita Nicholaus na baadaye kuuliza lakini mzee  Mohamed alikuwa kimya kabisa akikoroma na  kutoa mapovu mdomoni! Nicholaus akielewa hiyo ilikuwa ni hatari alimsukuma  mzee Mohamed pembeni na   kuukalia usukani, akafanikiwa kulirejesha gari barabarani kabla halijapinduka.

Aliliendesha  gari  hilo kwa kasi   kwenda moja kwa moja hadi mjini Baghdad kwenye hospitali ya AgaKhan ambako  mzee Mohamed alipokelewa akiwa mgonjwa mahututi! Madaktari walipompima waligundua  kuwa alipatwa na kiharusi sababu ya kupanda kwa shinikizo la damu!  Upande  mmoja wa mwili wake ulionekana kupooza,  mdomo na jicho lake  upande  wa kulia vilipinda!

Alilazwa hospitalini kwa muda wa miezi miwili  akipata matibabu ndipo hali yake ikabadilika na kuwa nzuri kiasi ingawa mkono wake wa kulia na mguu  bado viliendelea kupooza.

Hakuna hata ndugu mmoja wa mzee Mohamed aliyekuja hospitali kumwona wala kuulizia hali yake katika kipindi chote alicholazwa hospitali, kwa utajiri aliokuwa nao halikuwa jambo la kawaida.  Jambo hilo lilimshangaza sana Nicholaus  kiasi  cha kushindwa kujizuia kuuliza.

“Hawawezi kuja!”

“Kwanini?”

“Wao hudai mimi naringa  sababu  ni tajiri, binafsi nakushukuru sana Nicholaus kwa msaada ulionipa wewe ni ndugu yangu wa dhati na  Mungu atakulipia! Kuna wakati  nawaza hivi  kama  nisingekufahamu ingekuwa vipi leo?”

“Usijali baba!”

“Vipi maendeleo visimani, ni nani anasimamia?”

“Kazi inaendelea vizuri   wafanyakazi wa visima A,B,C wote nimewachagulia  kiongozi wao na wale wa  visima D,F,E na G  pia nimewawekea viongozi  wao na mimi ndiye  nashikilia nafasi yako, napokea  taarifa za kazi zao  kila siku!   Uzalishaji umeongezeka maradufu! Wiki iliyopita visima vyote vilitoa mapima 150,000 badala ya 100,000 kama ilivyokuwa zamani!

“Kweli?” Mzee Mohamed aliuliza kwa mshangao hakutegemea mtoto mdogo kama Nicholaus angeweza kuisimamia kazi yake vizuri kiasi hicho.

“Ndiyo baba!”

“Nicholaus umekua! Nalazimika kuamini  utaendesha vizuri kazi katika kipindi chote  cha ugonjwa  wangu mpaka nitakapopona?”

“Hakuna tatizo baba  kaa upumzike na uwe na amani mimi mwanao nipo!”

*****************

Fikra za mzee Mohamed zilikuwa tofauti na  mipango ya Mungu kwani hakupona wala kurejea katika afya yake ya zamani! Hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi katika miezi sita  iliyofuata hatimaye alifariki dunia! Siku chache kabla ya kifo chake aliandika wosia mbele ya wanasheria kuwa   mali zake zote aliziacha mikononi mwa Nicholaus akimwita mtoto wake katika wosia huo.

Visima vyote pamoja na majengo aliyokuwa nayo katika nchi za Ghuba yakawa ya Nicholaus, hakuacha kitu hata kimoja mikononi mwa ndugu zake!  Kufumba na kufumbua Nicholaus akawa  miongoni mwa matajiri akiwa katika umri mdogo kupita kiasi!  Hakuna aliyekuwa tayari kuliamini jambo hilo!

Wakati akiwa masikini wasichana wengi walikataa uhusiano na Nicholaus kimapenzi kwa sababu ya makovu aliyokuwa nayo usoni! Lakini  alipoamka tajiri  wasichana wengi walianza kujigonga kwake na miezi mitatu tu baada ya mzee Mohamed kufariki alimwoa  Suraia, binti mzuri na   mjukuu wa mfalme wa Kuwait!

Baada ya ndoa yao Nicholaus alibadili jina  na kuitwa Abdulwakil, Alimshukuru  sana Mungu kwa utajiri aliokuwa  ameupata. Mwaka mmoja baada ya ndoa yao walizaa mtoto wa kiume waliyemwita Patrick kama kumbukumbu ya baba yake mzazi.

Ni mwaka huo huo alisafiri na familia yake kuja hadi Arusha kwa lengo la kumfuata dada yake, alikutana na  taarifa kuwa nyumba ya  Shabir  aliyoishi na Victoria pamoja na Leah  iliungua kwa moto usiku na iliaminika kuwa wote waliteketea ndani ya moto huo!

Kilikuwa kilio kikubwa mno kwa Nicholaus kugundua kuwa  pacha wake hakuwa duniani,tena alikufa katika mateso makali ya kuungua na moto. Alirudi Iraq akiwa na simanzi kubwa moyoni  na  aliuahidi moyo wake kutorudi tena Tanzania.

“Pamoja na kuwa amekufa nitakitunza kipande hiki cha noti kama kumbukumbu yake!”

***********************

Maumivu ya tumbo:

Siku ya nne tumbo lilivimba  kupita kiasi na homa iliongezeka zaidi! Victoria alijua anakufa, hilo kwake halikuwa na mjadala tena! Kwa maumivu aliyokuwa nayo aliona ilikuwa ni bora kufa kuliko kuendelea kuishi lakini kitu pekee kilichomuumiza moyo ni kaka yake Nicholaus, hakupenda kabisa kufa kabla ya kukutana naye na kuunganisha noti zao.

Ghafla muunguro wa gari ulisikika nje ya ngome yao na mara kengele ilianza kulia!  Ilikuwa ni ishara nje kulikuwa na mtu aliyetaka kufunguliwa! Aliposikiliza vizuri ingawa  kwa mbali alisikia sauti ya Leah pamoja na Manjit! Akajua mkombozi amefika  alijaribu kunyanyuka  kwa lengo la kwenda langoni kufungua, lakini hatua tatu   mbele alishindwa na kuanguka chini!

Leah alikishuhudia tukio hilo kupitia katika tundu lililokuwepo katika lango hilo, hapakuwa na njia nyingine ya kufanya ziadi ya kumwomba dereva wa teksi iliyowaleta aparamie ukuta na kuingia hadi ndani na kulifungua lango,  Leah alikimbia hadi mahali alipoanguka Victoria, alishangazwa na hali aliyomkuta nayo, machozi yalimdondoka kwa uchungu.

“Vicky! Vicky! Vicky!”Aliita Leah.

“Mh!”Victoria aliitika kwa kuguna!’

“Imekuwaje? Baba yuko wapi?”

“Na….umwa! Sana nipeleke hospitali Leah!”

Hapakuwa na sababu ya Leah kuendelea kuuliza  ingawa alijua kulikuwa na tatizo, kilichokuwa muhimu wakati huo ni Victoria kupelekwa hospitali haraka iwezekanavyo! Walimbeba na kumpakia ndani ya teksi na kwa haraka walimkimbiza hospitali ya Canadian Fellowships Consultant hospita ambako daktari waliyemkuta alishangazwa na hali aliyokuwa nayo mgonjwa!

“I cant deal with this case it needs a specialist in Gaenocology!”(Siwezi kumshughulikia mgonjwa huyu anahitaji bingwa wa magonjwa ya wanawake) alisema daktari huyo na palepale bila kupoteza muda alinyanyua simu na kupiga namba fulani dakika chache tu baadaye mzee wa makamo aliingia.

“Can I have a per vaginal examination tray?”(Unaweza kunipa vifaa vya kupimia sehemu za siri?)

“Yes doctor!”(Ndiyo daktari)

“And gloves too!”(Na glovusi pia)

Nesi alimpa daktari vifaa vyote  alivyoomba na daktari alianza kumpima Victoria sehemu za siri, alichukua usaha katika pamba kwa  lengo la  kuupima.

“This is a septic incompete abortion, to be accurate we need to do an Ultra sound  urgently and take pus for culture and sensitivity ok?”(Hii ni mimba iliyotoka nusu halafu ikaingiliwa na wadudu  ili kuwa na uhakika zaidi tunahitaji kupiga picha tumboni na kuwakuza wadudu waliomo  katika usaha ili tujue ni dawa gani itawaua!)

“Sawa daktari!” aliitikia nesi na vipimo vyote vilichukuliwa majibu yalipotoka yalionyesha kila kitu alichokisema daktari kilikuwa sawa  mfuko wa uzazi wa Victoria ulikuwa umeoza   na haukufaa tena!

“Nothing can be done to save her life except doing histerectomy!”( Hakuna kinachoweza kufanyika ili kuokoa maisha yake isipokuwa kuutoa kabisa mfuko wake wa uzazi!) daktari alimwambia Leah.

Mpaka muda huo Shabir alikuwa hajafika hospitalini   pamoja na kupewa taarifa kuwa mke wake alirudi  kutoka Bombay kumpeleka Victoria hospitali, Leah alishindwa kuelewa ni kitu gani hasa kilitokea   akiwa safarini.

“What are the results for culture and sensitivity?”(Majibu ya wadudu waliokuzwa katika usaha  yanasemaje?) Madaktari waliulizana katika mkutano wao.

“There are lots and lots of gram negative bacilli!”(Kuna wadudu wengi sana waitwao bacilli!)

“To which antibiotics are they sensitive?”(Wanakubali kutibiwa na dawa gani?)

“Avelox alone!”(Avelox peke yake)

“Sure?”(Kweli?)

“Then prescribe Avelox!(Basi mwandikie Avelox)

Pamoja na matibabu yote hayo bado hali ya Victoria haikuwa nzuri na  Leah  aliendelea kuishi naye wodini kwa siku saba akitibiwa  yeye na mtoto wake Manjit walikuwa hospitalini siku ya nane madaktari waliamua kumpeleka Victoria chumba cha upasuaji ambako mfuko wake  wa uzazi ulitolewa.

“So, she will never bear children?”(Kwa hiyo hatazaa kabisa maishani mwake?)

“That’s the truth, but her life is also very important!”(Huo ndio ukweli lakini maisha yake pia ni muhimu sana)

“Kweli!”

Siku hiyo jioni baada ya Victoria kuletwa wodini kutoka chumba cha upasuaji, Leah alipewa ankara za matibabu yote aliyopewa Victoria tangu alazwe  hospitali, kwa sababu hakuwa na pesa aliondoka na  Manjit kwenda nyumbani kumwomba pesa Shabir.

“Ningekuwa na mtu mwingine wa kunisaidia nisingekwenda kwa Shabir!” aliwaza Leah wakati akitembea kutoka hospitali.

Walikuta mlango wa nyumba ukiwa wazi hiyo halikuwa jambo la kawaida kwa mlango wa nyumba yao kuachwa wazi! Hilo liliwashtua kidogo lakini hawakujali waliingia hadi ndani.

“Mh mama kuna harufu ya kitu gani?”Manjit aliumuuliza mama yake.

“Sijui ni kitu gani lakini ni mnyama ameoza!”

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano hapahapa.