
MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
DROO ya pili ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba awamu ya pili itafanyika Machi 17 mwaka huu ambapo kama ilivyokuwa ile ya kwanza, itatawaliwa na zawadi kibao zitakazobadili maisha ya washindi.
Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, alisema juzi kuwa zoezi hilo la kufanya droo ndogo litaendelea kila mwezi ili kuhakikisha wasomaji wengi wa magazeti ya Ijumaa, Championi, Uwazi, Risasi, Amani na Ijumaa Wikienda wanapata zawadi.
“Huu ni mwendelezo wa droo ndogo za Shinda Nyumba kama tulivyoahidi hapo awali, tutazifanya kila mwezi na tumeboresha aina za zawadi pamoja na thamani zake, sasa wasomaji wetu watajikuta wakiondoka na zawadi nzuri zaidi tofauti na Bahati Nasibu iliyopita, niwasisitize tu wasomaji wetu waendelee kujaza na kutuma kuponi zao kwetu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuweza kuibuka mshindi,” alisema Mrisho.
Droo ndogo ya kwanza ilifanyika Februari 8 mwaka huu katika ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakheem ambako washindi watano walijishindia zawadi za pikipiki, televisheni, simu za kisasa, vyombo vya jikoni na vitu vingine vingi. Washindi hao walikuwa ni Andrew Mtunguja wa Muheza mkoani Tanga, Ambrosi Ligonja wa Mang’ula, Morogoro, Evans Stanley wa Kunduchi, Said Mohamed na Gasto Peter wote wa Kimara jijini Dar es Salaam. Naye Afisa Usambazaji wa Global Publishers, Davis Mwaipaya, alisema:
“Ndani ya magazeti yetu kwenye ukurasa wa pili kuna kuponi ambayo unaijaza na kuileta kuponi hiyo kwenye ofisi zetu zilizopo Bamaga, Mwenge jijini Dar au unaweza kupeleka kwa mawakala au wauza magazeti wenye ndoo maalumu za Shinda Nyumba, ambao wako nchi nzima.”
Bahati Nasibu hiyo kubwa kabisa kuwahi kuchezwa na kampuni ya magazeti, inadhaminiwa na Kilimanjaro Institute of Technology and Management na British School.