×

 Meya Mwita: Mafuriko Jiji la Dar es Salaam Kuwa Historia

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, akizungumza wakati akiwa na ugeni wa taasisi inayoshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi duniani (C40 CITIES) ofisini kwake leo.
Wakati wa majadiliano kati ya pande hizo mbili.

 

 

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, amesema mipango thabiti iko mbioni ili kuboresha miundombinu yenye changamoto dhidi ya mafuriko na majanga mbalimbali yanayoweza kulikumba jiji hilo.

 

Meya Mwita aliyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na ugeni kutoka taasisi inayoshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi duniani (C40 CITIES) ofisini kwake Karimjee jijini hapa.

Ugeni huo uliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa C40 CITIES Kanda ya Afrika, Hastings Chikoko na Mkurugenzi Mkuu wa C40 CITIES kanda zote duniani kutoka London, Uingereza.

Amefafanua kuwa katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuleta mtalaamu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambaye atafanya kazi ya kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mabadiliko hayo jijini hapa.

 

Amesema pia wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yanakumbwa na mafuriko mara kwa mara likiwemo bonde la Mto Msimbazi, Jangwani na maeneo mengine.

 

“Leo nimekutana na marafiki zetu hawa wa C40 CITIES, tumeongea mambo mengi ya kujenga na kuliletea jiji letu maendeleo katika sekta ya miundombinu ambayo imekuwa ni changamoto katika jiji letu.

“Jiji letu linakua kwa kasi kubwa, tunatakiwa kujipanga mapema, maeneo mengi yanakumbwa na mafuriko wakati wa mvua, wananchi wetu wanahangaika, sasa imefika kipindi ambacho tunapaswa kulipatia ufumbuzi jambo hili,” amesema Meya Mwita.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa C40 CITIES, Hastings Chikoko, amesema kuwa wamekuja jijini hapa kwa ajili ya kusaidiana katika maeneo matatu ambayo ni usafiri jijini, kukabili mafuriko na ukame ili kuwezesha kilimo cha mijini.

 

Alisema taasisi hiyo itatoa mtaalamu/mshauri mmoja ambaye atafanya kazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa muda wa miaka mitatu ili kutoa mapendekezo ya namna watakavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ili jiji liwe salama.

 

 

NA DENIS MTIMA/GPL

Leave a Comment