Desemba 9, mwaka huu, Tanzania ilikuwa iliadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 56 ya Uhuru wake. Lakini kama kuna nyongeza ya shangwe hizo ambayo iliwakonga mamilioni ya Watanzania, ni kuachiliwa kutoka kifungo cha maisha jela kwa wanamuziki mahiri wa muziki wa dansi Bongo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.
Wawili hawa walikaa gerezani kwa takriban miaka 13 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuwanajisi watoto 10 wa Shule ya Msingi ya Mashujaa iliyopo Sinza, Dar, mwanzoni mwa miaka ya 2,000.
Kuachiliwa kwao kuliwezekana baada ya kupata msamaha kutoka kwa Rais Dk John Pombe Magufuli ambaye alitumia vifungu vya katiba vinavyompa mamlaka hiyo.
Katika kipindi ambacho wawili hao walikuwa gerezani, baadhi ya wanamuziki ambao walifanya nao kazi wakiwa na bendi mbalimbali walifariki dunia.
Baadhi yao, ambao wangejisikia furaha ya ajabu kukutana tena ana kwa ana na wawili hao uraiani ni kama wafuatao;
MCD
Masoud Mohamed ‘MCD’, alikuwa ni mpiga tumba wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ ambaye alifariki dunia Januari 2014, akiwa mjini Moshi, Kilimanjaro alikokwenda kwa ajili ya matibabu.
Kabla ya kifo chake, MCD alifanya kazi kipindi ambacho wawili hao walikuwa wakikamua jukwaani na hakuna shaka kwamba leo angejawa na furaha kubwa kumuona Babu Seya na Papii wakiwa uraiani.
AMINA NGALUMA ‘JAPANESE’
Japanese alikuwa ni mwimbaji gumzo katika kila bendi aliyopita, zikiwemo Double M Sound na African Revolution ‘Wana Tamtam’, kote aliacha jina na ‘legas’ ambayo inamfanya kukumbukwa mpaka leo katika muziki wa dansi.
Hata hivyo, wakati muziki huo ukiwa bado unamhitaji, Mei 2014, akiwa nchini Thailand, alifariki dunia baada ya kupatwa na uvimbe kichwani.
Mwanadada huyu alifariki dunia ikiwa ni miaka 11 tangu ‘kaka’ yake, Babu Seya afungwe. Miaka mitatu imepita akiwa hayupo duniani na kaka yake huyo ametoka jela. Hakika lilikuwa jambo la kufurahisha kama wawili hawa wangekutana, lakini kwa mapenzi ya Mungu haikuwezekana.
NDANDA KOSOVO
Asubuhi ya April 9, mwaka 2016, ilikuwa ni siku ya huzuni kwenye muziki wa dansi nchini baada ya nguli wa muziki huo na mkali wa Kibao cha Chozi la Mnyonge, Ndanda Kosovo kupoteza maisha kwenye Hospitali ya Muhimbili jijini Dar.
Ndanda ni miongoni mwa watu ambao wangefurahi sana kuliona tabasamu la Babu Seya baada ya kuliona jua akiwa huru. Babu Seya mwenyewe alikuwa akimuita Ndanda ‘kaka’! R.I.P Ndanda!
BANZA STONE
Bila shaka Banza angekuwepo hai angefurahi sana kumuona Babu Seya na mwanaye wakiwa uraiani. Kwa kushirikiana nao wakiwa makundi tofauti, wawili hawa wangemtoa machozi ya furaha Banza kwa jinsi ambavyo walijitoa kuupaisha muziki wa dansi hapa nchini.
Banza Stone alifariki dunia mchana wa Ijumaa ya Julai 17, mwaka 2016 katika Hospitali ya Mwananyamala ikiwa ni miezi miwili tu tangu Ndanda Kosovo afariki dunia.
AMIGOLAS
Enzi za uhai wake, Amigolas ambaye jina lake halisi ni Hamis Kayumbu, alifanya kazi kwa kushirikiana na Babu Seya kwenye matamasha ya dansi na sehemu tofautitofauti.
Alifariki dunia tangu Novemba 8, mwaka 2014 na hakika huyu pia angekuwa mwenye furaha kumuona Babu Seya akiwa uraiani kutokana na ukaribu wao.
Boniphace Ngumije.