
FUKUZAFUKUZA makocha katika Premier League imeendelea kushika kasi ambapo Klabu ya Swansea City imemfukuza kazi Paul Clement kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo.
Mara baada ya kutoka kwa tangazo hilo, tayari kocha wa zamani wa Manchester United, Louis van Gaal anatajwa kuwaniwa na timu hiyo huku majina ya makocha wengine yanayotajwa kupewa nafasi pia ni bosi wa zamani wa West Ham, Slaven Bilic na Ronald Koeman aliyekuwa akiinoa Everton.
Swansea kwa sasa ndiyo inayoshika mkia katika Premier ikiwa imeshinda michezo mitatu tu kati ya 18 ya msimu huu.
Pamoja na tetesi hizo, mapema wiki hii, Van Gaal, 66, alinukuliwa akisema kuwa bado anaamini atarejea katika soka kwa kuwa kuna kazi hakuimaliza baada ya kufukuzwa Man United mwaka 2016.