
MSANII wa Bongo Fleva, Papaa Masai wiki iliyopita aliwaongoza mashabiki wa burudani kumkumbuka msanii, marehemu Mr Ebbo kwa kuimba wimbo wake wa Mimi Mmasai katika mkesha wa Mwaka Mpya 2018, uliofanyika katika Uwanja wa Burudani wa Dar Live, Mbagala, Zakhem jijini Dar es Salaam.
Papaa Masai alikuwa ni miongoni mwa wasanii waliotumbuiza katika Show ya Kibabe iliyowakutanisha wasanii wakali akiwemo MC Dalada, Jay Moe, Young Killer, Coyo, Q Boy Msafi, Stamina na wengineo.
Msanii Coyo aliwakamata mshabiki wake kwa kuimba nao kila nyimbo, huku msanii Q Boy Msafi aliyeibuka jukwaani akiwa amevaa ovalori na maski usoni akiwashangaza mashabiki kwa ubunifu wake. Kwa msanii Ice Boy yeye alipanda na kulisafisha jukwaa kwa kushangiliwa na mashabiki kisha kumuita jukwaani msanii Young Killer ambaye alikata kiu ya mshabiki wake kwa michano ya hatari.
Young Killer akiwa bado anaendelea kutamba na michano alimwalika mkali mwingine wa Hip Hop, Stamina ambaye naye aliwanyanyua mshabiki kwenye viti vyao. Huku nguli wa kurap Jay Moe akiwaomba mshabiki wake wamsaidie kushare shoo hiyo ya mwaka mpya kwenye mitandao wa kijamii.
Host wa Show ya Kibabe alikuwa ni MC Shebby akishirikiana na mchekeshaji Dullvan ambao walifanya poa katika kuongoza burudani hiyo. Mashabiki wa burudani walipata nafasi ya kula keki iliyokatwa na mtangazaji mkongwe nchini, Maimatha wa Jesse. “Nimeikubali sana shoo ya leo kwani kila msanii aliyepanda jukwaani alitoa burudani nzuri na ya kipekee, kwa kifupi nimeupokea mwaka mpya 2018 kwa shangwe sana,” alisema mmoja wa mashabiki