
HAKUNA mpenzi wa filamu za Kibongo ambaye hamjui Jacqueline Wolper, hii ni kwa sababu ya kujituma kwake kwenye kazi, hasa kuanzia kipindi kile tasnia ya Bongo Movie ilipokuwa juu, enzi za akina marehemu Kanumba mpaka leo.
Binafsi si shabiki sana wa filamu za Kibongo lakini mara chache ninazotazama kazi za hapa nyumbani, huwa navutiwa na uwezo wa huyu binti. Ukimtazama kwa makini, utagundua kwamba Wolper anacho kipaji kikubwa cha uigizaji na ndani ya moyo wake anayo matamanio ya kufika mbali.
Ndiyo maana utamuona kuanzia kwenye filamu za wakongwe, filamu za wasanii wachanga mpaka kwenye video za muziki za wasanii wa muziki wa kizazi kipya. Kwa hilo sina tatizo naye.
Upande wa pili wa maisha yake ya kimapenzi ndiko kwenye tatizo, Wolper hana historia ya kuvutia na matendo yake ya kuwaanika hovyo mitandaoni watu anaovunja nao amri ya sita kabla ya kuingia kwenye ndoa, huwa yanawafanya wengi wasiyaone mafanikio yake kisanaa zaidi ya ‘skendo’ za kila kukicha.

Maisha ya kimapenzi ni faragha na kila mtu anayo haki ya msingi kabisa ya faragha, hilo linafahamika lakini inapotokea mhusika mwenyewe kutojua maana ya faragha na kumwaga mambo yake ya ndani hadharani, tena kwa viapo na nadhiri, hapo ndipo penye tatizo.
Inafahamika wazi kwamba kwa mila za Kitanzania, tunategemea binti akishafikia umri wa kuolewa, muoaji atafuata hatua zinazotakiwa, ikiwa ni pamoja na kujitambulisha ukweni, kutoa posa na kuchumbia kisha baadaye ndoa inafuata.

Hakuna anayetegemea kuona mwanamke wa Kitanzania, akiwa anabadilibadili wanaume huku akileta maigizo hata katika suala nyeti kama ndoa! Kuvalishana pete za uchumba si jambo la kufanyia mzaha kwa sababu hapo safari ya kuelekea kwenye unganiko takatifu kwa maana ya ndoa huwa umeanza.
Hivi karibuni kulizuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii, zikimhusisha mwanadada huyu, Wolper kwamba anaenda kuchumbiwa nyumbani kwa wazazi wake, Moshi mkoani Kilimanjaro na Kibaha mkoani Pwani na mwanaume ambaye mpaka sasa bado hajulikani.

Ukifuatilia kwa makini sarakasi za kimapenzi za Wolper, wakati akitoa taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii, zilikuwa ni siku chache tu tangu amwagane na aliyekuwa mpenzi wake, Brown.
Ukijiongeza kidogo, utagundua kwamba kitendo cha Wolper kutangaza kwamba anaenda kuchumbiwa, kinatoa tafsiri zaidi ya moja.
Kiuhalisia haiwezekani kwa muda mfupi tu ambao Wolper na Brown wamemwagana, tayari mwanadada huyo awe amekutana na mwanaume ambaye kweli yupo ‘serious’ anataka kwenda kumchumbia na kujitambulisha ukweni! HAIWEZEKANI.
Kwa wadadisi wa mambo, ni rahisi kugundua kwamba, aidha Wolper alifanya hivyo kwa sababu ya kumrusha roho mpenzi wake waliyeachana naye, Brown, au alifanya hivyo kwa lengo la kutaka umaarufu, wenyewe wanaita ‘kiki’.
Pia inawezekana kama ni kweli huyo mwanaume yupo na ameenda kumchumbia kama mwenyewe anavyodai, basi alikuwa akitoka na Brown kimapenzi lakini wakati huohuo akawa na mwanaume mwingine.
Kwa jinsi ninavyowajua wasanii wa Bongo Movie, kati ya hayo mambo matatu, moja linaweza kuwa kweli kwa Wolper na uwezekano mkubwa ni kwamba hakuna ndoa wala mchumba, bali ni KIKI!
Anataka azungumziwe, awe kwenye midomo ya watu, mitandao ya kijamii itawaliwe na stori zake, umaarufu wake uendelee kupaa! Unaweza kuona aina ya wasanii tulionao kwenye tasnia ya filamu Bongo. Yaani yupo tayari kujidhalilisha, tena hata kuwahusisha mpaka wazazi wake wakati anajua kabisa kwamba anachokizungumza ni uongo.
Nizungumze na wewe Wolper! Kama ulichokisema ni kweli, nakutakia kila la heri katika safari yako ya ndoa unayoelekea kuianza, lakini kama ni kiki kama mlivyozoea kucheza na akili za watu, basi utakuwa umejishushia sana heshima yako, kimsingi huo ni ushamba.
Historia yako katika mapenzi inakuhukumu, kuanzia kipindi ulipokuwa na Abdallah Mtoro ‘Dallas’, Putin, Mkongo, Harmonize, Brown na wengine ambao hatuwajui (kama wapo), hata kama wao ndiyo wanakutenda ni rahisi watu kukutafsiri kwamba wewe si wife material! Hebu jaribu kuwa msiri kwa mambo yako ya ndani, acha watu waone vitendo tu.
Za chembe Lazima Ukae Na Haziz Hashim