
POLISI nchini Guinea wamemkamata mganga wa kienyeji, N’na Fanta Camara kwa tuhuma za kuwalaghai mamia ya wanawake ambao ni wagumba na kuwapa ujauzito feki.
Imeelezwa amekuwa akiwapa dawa ya kienyeji wagumba na kusababisha matumbo yao kufura (kujaa) na kuonekana kuwa ni wajawazito ambapo wagonjwa hulipia dola 33.
Polisi wanaamini kuwa Bi Camara alipata maelfu ya dola kila mwezi licha ya yeye kusema kuwa alijaribu tu kusaidia. Zaidi ya wanawake 200 waliandamana Jumanne, nje ya kituo cha polisi kwenye Mji Mkuu wa Guinea Conakry ambapo Bi Camara alikuwa anashikiliwa.

Zaidi ya wanawake 700 walio na kati ya umri wa miaka 17 na 45 wanaamiwa kuathiriwa na matibabu ya Bi Camara huku idadi hiyo kubwa ikiashiria jinsi Guinea na nchi zingine za Afrika zinawategemea madaktari wa kienyeji. Mwaka 2006 shirika la afya duniani lilisema kuwa asilimia 80 ya Waafrika walitumia matibabu ya kienyeji.
Wanawake hao walisema kuwa Bi Camara aliwashauri wasimuone daktari, na mara alipothibitisha kuwa wamekuwa wajawazito walistahili kumpa kuku na vitambaa kama njia ya kumshukuru na baadhi yao walisema kuwa walionekana kuwa wajawazito kwa kati ya miezi 12 na 16.
Daktari aliyewachunguza amebaini 47 kati ya wanawake walioathiriwa alisema wako kwenye hatari ya kukumbwa na matatizo ya kiafya ya muda mrefu kutokana na matibabu hayo.
Bi Camara hata hivyo anasema kuwa hajafanya lolote baya.
“Ninafanya kazi ngumu sana kuwasaidia wanawake kuweza kutimiza ndoto zao lakini mengine yako mikononi mwa Mungu, aliwambia waandishi wa habari mjini Conakry.