
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametembelea Hospitali ya Mwananyamala ambapo amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Salum Hapi, kwa kufanikiwa kuisimamia mipango ya maendeleo katika wilaya hiyo ikiwemo upatikanaji wa huduma bora ya afya kupitia hospitali hiyo huku akisisitiza suala la wananchi kukata bima ya afya.
Makonda amesema Serikali itaandaa mpango wa matibabu kwa kutumia kadi ya bima ya afya, kwa wakazi wa Dar, katika Hospitali zote za umma, Mwananchi ambaye hatakuwa na kadi ya bima, hataweza kupata huduma ya afya katika Hospitali za umma popote Dar es Salaam.
“Umuhimu wa kuwa na bima ya afya ni mkubwa,tuna bima ya mtoto na bima ya watu wazima, ni vyema tukakata bima zetu za afya mapema, tutazindua kampeni kubwa ya tiba kwa kadi ambayo tutaoa muda ili watu wakate bima hiyo, itafika wakati kama mtu hatakuwa na kadi hiyo hatoruhusiwa kutibiwa kwenye hospitali yoyote ya serikali Mkoa wa Dar es Salaam, isije ikafika hatua tukalazimishana kwa sababu jambo la afya ni la muhimu sana” alisema makonda.
Aidha, Makonda, ameelezea kuhusiana na ofisi aliyowajengea Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata), ambayo inatarajia kumalizika hivi karibuni.