×

Kapteni Komba Amuombea Lulu!

Komba enzi za uhai wake.

 

 

MAZUNGUMZO katika kolamu hii ni ya kiburudani si halisi, yameongezewa nakshi na mwandishi ili kuburudisha, ungana ndani yake kuna ujumbe pia:

Macho yanatoa machozi. Hii ni kutokana na ukali wa moshi mwingi uliotanda kila mahali. Moshi mweusi unaofuka mfululizo, unageuka karaha kwangu na hapohapo nalazimika kutafuta uwezekano wa kuondoka. Lakini ghafla naitwa na sauti ya kukwaruza lakini tamu kuisikiliza.

MIMI: Kapteni Komba shikamoo, habari za huku?

KOMBA: Marhaba, umekuja na nani na umefikaje huku wewe?

MIMI: Sijui nimefikaje lakini unaweza kuniambia hapa ni wapi?

 

KOMBA: Inakuhusu nini wewe? Tuzungumze yanayofaa, kwanza nini kinaendelea huko ulimwenguni hususan masuala ya kisiasa niliyokuwa nayapenda?

MIMI: Dk. John Magufuli ndiye rais wetu kwa sasa, Kassim Majaliwa ni Waziri Mkuu na Ndugai ndiye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KOMBA: Dah! Maisha yana mizunguko yake bwana. Juzi nilikutana na Banza Stone, sasa nani anatamba kwa muziki wa dansi sasa hivi?

MIMI: Muziki huo unasuasua sana kwa sasa. Yaani umepoteza kabisa mvuto na sijui nini kifanyike lakini hivi karibuni walikusanyika viongozi wote wa bendi hizo nadhani watakuja na mkakati mpya wa kurejesha heshima ya muziki huo.

KOMBA: Bora wafanye hivyo. Lowassa yupo? Aliposhindwa urais alifanyaje? Au ameshaachana na masuala ya siasa kabisa?

Lulu

MIMI: Lowassa bwana yupo, lakini alishahama chama. Kwa sasa ni mwanachama hai wa Chadema na hivi karibuni aliitwa Ikulu na Rais Magufuli lakini hajaacha siasa.

KOMBA: Hiyo dunia yenu nayo! Wasanii wa filamu wapo? Hivi yule Lulu bado anaigiza?

MIMI: Sanaa ya filamu nayo inapepesuka na kusimama lakini mvuto umepungua na tuliowategemea kutuwakilisha kwenye eneo la sanaa, hawafanyi hivyo na badala yake wanatuangusha, lakini sanaa ya filamu inaendelea na wapo wanaofanya vizuri.

KOMBA: Sawa. Nimekuuliza kuhusu Lulu mbona hujajibu?

MIMI: Aaah, nimesahau kidogo mzee, lakini habari mbaya ni kwamba Lulu yuko gerezani akitumikia miaka miwili baada ya kukutwa na hatia ya kuua bila kukusudia, nadhani unakumbuka sakata lake na marehemu Kanumba.

 

KOMBA: Ayaaa, kumbe ameshahukumiwa? Pole yake na kuanzia leo nitakuwa namuombea na nina imani atamaliza kifungo akiwa mwenye afya njema na maisha yataendelea. Ukipata nafasi ya kumtembelea mwambie namsalimia sana na sitaacha kumuombea kama nilivyosema.

MIMI: Nimekuelewa mzee, lakini zile tetesi kuhusu wewe na Lulu zilikuwa na ukweli?

KOMBA: Tetesi gani wewe bwana sitaki maswali ya kijinga na kama umeishiwa cha kuzungumza ondoka zako nisije nikafanya kitu kibaya hapa.

 

MIMI: Basi mzee naomba yaishe, nimechomekea tu. Kwa huku unafanya nini?

KOMBA: Naishi kama nilivyokuwa huko, tofauti ni kwamba huku maisha ni raha mustarehe na hakuna masumbuko na mahangaiko kama huko kwenu, niko huko na watu wengi maarufu na sioni tofauti yoyote na duniani. Kama namuona Mwalimu Nyerere, namuona Mandela, namuona Karume, namuona Deo Filikunjombe, Jeremiah Sumari, Cellina Kombani, Edward Sokoine na wengine wengi, hakuna tofauti kabisa.

MIMI: Kweli kabisa na mimi zamu yangu ikifika tutaungana ila siombei iwe hivi karibuni, kwa sababu kuna mambo sijayakamilisha huko duniani.

 

KOMBA: Mimi nilijua ndiyo umekuja moja kwa moja kumbe una mpango wa kurudi duniani.

MIMI: (namtazama kwa jicho kali), mzee acha mambo yako, unadhani huku ni kujakuja tu? Mimi zamu yangu bado, hadi nikamilishe na kutimiza ndoto zangu.

KOMBA: Basi naomba nikuruhusu uondoke na mimi niende kwenye mambo mengine, nataka nikamtembelee Nyerere na Karume, siku kama ya leo huwa wako kule kwenye bahari unayoiona kule, nataka nikapate busara zao.

MIMI: Sawa, lakini nyimbo zako bado zinaimbwa sana na huo ndiyo utambulisho wako mkubwa kwa taifa letu.

 

KOMBA: (anainama na kuanza kuimba), Sasa kumekuchaaa, sasa kumekuchaaaa, jogoo limekwishawika Chimwagaaaa, kada wa CCM, kada wa CCM apewe kura za ndiyoooo…yule paleee…yule paleee, mnamuonaaaa…sasa kumekuchaaa…. Jogoooo…

Hapohapo najikuta nikiimba wimbo huo nikiwa nimelala kitandani kwangu.

Ni asubuhi na kwa bahati nzuri ni Jumapili siku ya kupumzika kwangu hivyo naendelea kulala huku nikiitafakari ndoto yangu ya kufanya mazungumzo na Kapteni Komba, nabaki nasikitika na kuendelea kulala.

Kwa maoni na ushauri, wasiliana nami kupitia namba hizi; 0679-659 633.

Na Brighton Masalu  |  SAA TISA USIKU KITANDANI kwangu