
Mwili wa Mwenyekiti Mstaafu wa hama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Dkt.Walid Amani Kaburu umezikwa leo nyumbani kwake Kigoma na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa serikali, vyama na siasa.
Kaburu alifariki usiku wa kuamkia juzi tarehe 07 Machi, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dkt. Kaburu ambaye alizaliwa Mei 23, 1949, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini (CHADEMA) kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.
Aidha, Dkt. Kaburu amewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki akiiwakilisha Tanzania kuanzia Juni 05, 2007 hadi Juni 04, 2012.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa sasa wa Kigoma Mjini amesema kwao huo ni msiba mkubwa, na umewaacha na majonzi tele.
“Tumeamka asubuhi na habari za kusikitisha kuwa Dkt. Amani Walid Kabourou, Mbunge Mstaafu wa Kigoma Mjini ametangulia mbele ya haki. Hakika ni msiba mkubwa kwetu. Mola ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” ameandika Zitto.
