×

IMEFICHUKA! Mzungu Aliyehukumiwa Miaka 26 Jela Atorokea Tanzania

 

SIRI imefichuka kuwa, Gareth Johnson (pichani) ni Mzungu anayesakwa kwa udi na uvumba na Serikali ya Uingereza, Kitengo cha Mamlaka ya Kodi na Mapato (HMRC), anadaiwa kutorokea Bongo baada ya awali kujificha nchini Kenya kwa muda mrefu.

 

Gareth, mzaliwa wa Forfar, Angus nchini Scotland anatafutwa kwa makosa ya ukwepaji mkubwa wa mabilioni ya fedha za kodi ambapo kwa kushirikiana na baba yake mzazi, Geoffrey Johnson walifun­guliwa kesi kabla ya kufanikiwa kutoroka nchini Uingereza.

Taarifa za awali zilionesha kwamba baada ya kutoroka nchini Uingereza, wawili hao walikwenda kujichimbia nchini Kenya katika eneo la Muthaiga lililopo umbali wa kilometa nne, Kaskazini mwa Jiji la Nairobi.

 

 

Awali, mwaka 2013, wawili hao walihukumiwa bila uwepo wao mahaka­mani ambapo Gareth alihu­kumiwa kifungo cha miaka 12 na baba yake miaka 10 jela huku wakitakiwa kulipa deni la pauni milioni 109 (zaidi ya bilioni 340).

Baada ya kushindwa kulipa deni hilo la mamil­ioni, wawili hao wal­iongezewa hukumu ya miaka 14 kila mmoja, hivyo kumfanya Gareth kutakiwa kutumikia kifungo cha miaka 26 na baba yake kutu­mikia kifungo cha miaka 24.

 

BABA YAKE ANASWA

Julai, 2017, baba yake aitwaye Geof­frey Johnson, alinaswa kwenye Uwanja wa Ndege Dubai, muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Mombasa nchini Kenya kwa ushirikiano wa HMRC na askari wa Kenya na Dubai, akitumia hati bandia ya kusafiria.

 

Baada ya kukamatwa, haraka al­isafirishwa chini ya ulinzi mkali hadi nchini Uingereza ambako tayari mashtaka dhidi yake na mwanaye yalikuwa yamesomwa na kutolewa hukumu bila wao kuwepo, hivyo akaanza kutumikia kifungo cha miaka 24 jela.

Gareth na baba yake, walikuwa wami­liki wa Kampuni za Tectonics Holdings na Coast Logistics, ambazo licha ya wenyewe kuzisajili kwamba zinafanya biashara ya simu nchini za Uingereza na Hispania, zinatuhumiwa kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu na ukwepaji mkubwa wa kodi nchini humo.

 

WALIKUWA NA KUNDI LA WAHALIFU

Taarifa zaidi zilieleza kwamba, Gareth na baba yake, walikuwa na kundi la wahalifu wapatao 18, ambao kazi yao ilikuwa ni kupora mamilioni ya fedha kwenye benki mbalimbali na baadaye kuzitakatisha kupi­tia kampuni zao sambamba na kufanya udalali wa kitapeli wa kodi za ongezeko la thamani kwenye simu kabla ya baadaye kutoroka nchini humo baada ya kushtukiwa.

Wanachama wao na kundi lao la ki­halifu, wote walishakamatwa ambapo kwa pamoja, wamehukumiwa kifungo cha miaka 135 jela, huku mshirika wao wa karibu ambaye wanatokea sehemu moja, Albert Amri­tanand akitumikia kifungo cha miaka mitano jela.

 

GARETH YUPO BONGO

Taarifa zilidai kwamba, Gareth kwa sasa, kabla ya kutolewa kwa tangazo la kutafutwa kwake kwenye magazeti ya Kiswahili hapa nchini, anamiliki kiwanda maeneo ya Kipawa jijini Dar kiitwacho Johnson International Group kina­choshughulika na kuko­disha mitambo ya viwandani na mashine za ujenzi yakiwemo magreda, ambako hata hivyo, inatajwa kwamba huwa haonekani kirahisi kwa sababu haishi jijini Dar bali makazi yake yapo mkoani Iringa.

Mbali na shughuli hizo, inadaiwa pia kwamba Gareth anamiliki vitega uchumi vingine mkoani Iringa yakiwemo mashamba na ardhi kubwa ambapo ndipo yalipo maka­zi yake ya kudumu na sehemu nyingine nchini Tanzania, yakiwemo mahotelini na klabu za usiku.

Inaelezwa kwamba, Kampuni ya Johnson International Group, mwaka 2014 iliwahi kuingia kwenye mgogoro mkubwa baada ya wafanyakazi wake zaidi ya 125 kutishia kugoma kutokana na kutolipwa malimbikizo ya mishahara yao.

MALI ZAO NYINGI ZIMEFILISIWA

Mwendesha mashtaka wa serikali nchini Uingereza kupitia Kitengo cha The Crown Prosecution Service, Nick Price amewahi kunukuliwa na gazeti moja la nchini Uinge­reza, akisema: “Hukumu ya mahakama imetupa mamlaka ya kushirikiana na wadau wengine, kutafuta mali za watuhumiwa na kuzishikilia kwa mujibu wa sheria na hicho ndicho tunachokifanya kwa sasa.

“Tutaendelea kuzitafuta na kuzishikilia mali zao nchini Uingereza na kwingineko duniani.”

 

MAISHA YA KIFAHARI USIPIME

Kabla ya kutoroka nchini Uingereza, wawili hao wanatajwa kuponzwa na utajiri mkubwa wa ghafla waliokuwa nao huku wakiishi maisha ya kifahari mno ambapo kwa mujibu wa Gazeti la Daily Report, polisi walipokwenda kupekua kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, walishangazwa na jinsi walivyokuwa wakiishi maisha ya anasa.

“Kulikuwa na magari yenye hadhi ya juu ndani ya nyumba yao, yakiwemo Bent­ley, Ferrari, Porsch na magari mengine yenye thamani ya mamilioni ya fedha, iliwashangaza wengi kwa jinsi walivyokuwa na utajiri mkubwa.

 

“Muda mwingine walikuwa wakitumia helikopta binafsi kwenye matembezi yao, walikuwa wakiishi kwenye dunia ya kipekee kabisa,” kilinukuliwa chanzo na gazeti hilo.

Familia hiyo ilikuwa ikiishi kwenye jengo la kifahari, Turin House, likiwa limejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa takriban ekari 21, likiwa na bwawa la kuogelea ‘swimming pool’ na vitu vingine vingi vya kifahari.

Tangu walipotoroka nchini humo, jumba hilo hivi sasa limegeuzwa kuwa hoteli ya nyota tano ambayo haimilikiwi tena na familia hiyo.

 

Akizungumza na Uwazi juu ya sakata hilo juzi, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP Barnabas Mwakalukwa alisema kuwa, hana mamlaka ya kulizungumzia hilo badala yake watafutwe Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba au Polisi wa Kimataifa (Interpol).

Juhudi za kumpata Waziri Nchemba juzi Jumapili hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutokuwa hewani kila ilipopigwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha In­terpol nchini, Gustav Babile, ofisi yake haina taarifa rasmi kutoka Uingereza kuhusu watu hao.