
MPENZI msomaji Risasi Mchanganyiko kila Jumatano huwa linakusogezea kwenye ukurasa huu wakongwe mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wamepotea kwenye gemu, hawasikiki kabisa au wanajaribu kufurukuta ili kurudi kule walipokuwa lakini bado wanashindwa.
Leo tuko na msanii mkongwe, Haruna Kahema ‘Inspector Haroun’, mkali wa michano ambaye aliwahi kutamba na ngoma nyingi zikiwemo Pamba Nyepesi, Bye Bye na Hapa Kazi Tu!
Lakini pia mbali na kazi nzuri ambazo Inspector alifanya, umaarufu wake aliuvuna pia akiwa ndani ya kundi liitwalo Gangwe Mobb, ambalo aliliunda na mshikaji mmoja aitwaye Luteni Karama.
Kwa pamoja Inspector na Luteni wakiwa ndani ya Gangwe Mobb, walifanikiwa kufanya albumu mbili ambazo ni Simulizi za Ufasaha na Nje Ndani.
Hata hivyo baadaye ni kama kundi hili liliparanganyika kwani kila mmoja wao alianza kufanya kazi kivyake. Na kwa upande wa Inspector, akiwa solo artist, amefanikiwa kufanya albumu tatu, ambazo ni Ndoa Ina Doa, Ndani ya Pamba Nyepesi na Ina Bamba.
Akipiga mzigo peke yake naye meli ilianza kupigwa na mawimbi. Akaanza kuyumbayumba na mwishowe akapotea. Na ngoma yake ya mwisho iliyopokelewa angalau vizuri kwenye media ni Sharubu za Babu, aliyoitoa takribani miaka mitano iliyopita.
Kutokana na ukimya huo, Risasi Mchanganyiko limeamua kumtafuta. Na katika makala haya anafunguka nini sababu ya ukimya wake, nini anafanya na mambo mengine kuhusu muziki.
Risasi: Inspector kimya sana kaka, vipi gemu ndiyo umepiga chini?
Inspector: Siwezi kuacha muziki, ni maisha yangu, kwa hiyo nitaufanya siku zote.
Risasi: Huo muziki unaufanyia wapi maana husikiki kabisa?
Inspector: Ni kweli sisikiki. Lakini kuna muda inabidi upime juu ya mashabiki wako kama wanakuhitaji au lah! Sasa ndiyo nilichokuwa ninakifanya na kwa sasa nimeweza kugundua watu wananihitaji sana ndiyo maana nimeamua kurudi.
Risasi: Kwa hiyo sasa umerudi?

Inspector: Ndiyo nimerudi na kazi mpya inaitwa Ofa Zimebaki Stori. Nimemshirikisha kijana aitwaye Dreazy. Huyu pia anapatikana kwenye Gangwe Foundation, ambayo inahusika na kukuza vipaji vya wasanii chipukizi.
Risasi: Sawa. Vipi kuhusu Kundi la Gangwe, bado lipo?
Inspector: Kundi bado lipo, lakini kutokana na mambo ya kimaisha mimi na Karama, kila mmoja anafanya mambo yake, lakini mtu akiwekeza Gangwe ipo na zaidi hivi karibuni tunatarajia kufanya ujio wa pamoja kuwakumbusha mashabiki wetu enzi zile tunashika kila kona.
Risasi: Wakati upo nje ya gemu, kabla ya ujio huu nini hasa ulikuwa unakimisi?
Inspector: Shoo, unajua mimi ninapenda sana kufanya shoo na kuimba pamoja na mashabiki zangu. Sasa nilipokuwa kimya sikuwa ninafanya shoo kabisa. Nakumbuka shoo ya mwisho nilifanya Dar Live, muda kidogo umepita, kwa hiyo shoo ni kitu nilichokuwa ninakimisi sana.
Risasi: Kama ulikuwa hufanyi shoo, studio huingii nini zaidi ulikuwa unajishughulisha nacho?
Inspector: Biashara. Nina biashara zangu kwa ajili ya kuendesha maisha yangu ya kila siku. Namiliki maduka ya nguo, shamba kwa ajili ya ufugaji wa kuku na mambo mengine. Lakini studio nilikuwa ninaingia. Kwa sababu ninamiliki studio iitwayo Saba Seven Records, kwa hiyo muda wowote huwa ninaingia studio na kurekodi nitakavyo, sema kuachia tu nyimbo kwenye media ndiyo nilikuwa sifanyi.
Risasi: Na wakati huo upo nje ya gemu kwa muda bila shaka ulikuwa unasikiliza muziki pia, ni mwanamuziki gani ulikuwa unamsikiliza na unamzimikia kutokana na kazi zake?
Inspector: Ninamsikiliza sana Maua Sama. Kiukweli huyu dada ananinyima usingizi na ninatamani siku moja niweze kufanya naye kazi.
Risasi: Tunaona wanamuziki wengi wanakomaa kufanya kolabo za nje ili kutanua ‘fun base’ yao, wewe vipi kuhusu hili?
Inspector: Sijafikiria bado kufanya kolabo nje. Naamini hata mimi binafsi ninaweza kujipeleka kimataifa. Lakini ikitokea nitafanya ila kwa sasa sifikirii.
Risasi: Una nini cha kuwaeleza wakongwe ambao wamepotea kabisa kwenye gemu?
Inspector: Wasiogope changamoto kikubwa ni kupambana. Ninafurahi kuona kina Jay Moe wamerudi, kina Nature na wanajaribu kila siku kuangalia ni namna gani watafika kule juu ambapo wapo wadogo zetu. Ndiyo ndoto zangu pia kwa hiyo wakongwe wasilale.
Maoni/Ushauri 0654 88070788
MAKALA: Boniphace Ngumije.