×

LORI LA MAFUTA LILILOLIPUKA SEKENKE, KIFO CHA DEREVA YAANIKWA – VIDEO

NYUMA ya mlipuko wa lori la mafuta lililoteketea kwenye Mlima Sekenke mkoani Singida, kuna mapya yamefichuka juu ya kifo cha dereva wa lori hilo, Erasto Abed Zemba (25), Uwazi lina simulizi yenye kukutoa machozi.

WALITEKETEA PAPOHAPO

Erasto na utingo wake, Ramadhan Hash­im Ramadhan waliteketea papohapo kwenye ajali hiyo mbaya ya kuungua kwa moto na kubaki majivu, tukio ambalo lilijiri Machi 23, mwaka huu kwenye mlima huo wenye historia ya ajali za kutisha.

Marehemu.

UWAZI KWENYE MAZISHI

Mazishi ya Erasto yaliyohudhuriwa na Uwazi yalifan­yika juzi Jumapili kwenye Makaburi ya Kanisa Kato­liki Parokia ya Mtakatifu Monica almaarufu Maka­buri ya Mangweha yaliyopo Kihonda mkoani hapa.

Uwazi lilishiriki mazishi hayo yaliyoongozwa na Padri Msimbe wa Parokia ya Mtakatifu Monica iliyopo Kihonda.

Misa ya kumuombea marehemu huyo ilifanyika ny­umbani kwao, Kihonda Mazimbu Road kabla ya kwenda kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele kwenye makaburi hayo.

Mjomba wa marehemu.

 

MJOMBA, MKE WAFICHUA MAPYA

Baada ya mazishi hayo, Uwazi lilizun­gumza na msemaji wa familia ya mare­hemu ambaye ni mjomba wa Erasto, Eniceth Severini na mke wa marehemu, Nuru Ramadhan.

Wawili hao ndiyo waliofichua mapya juu ya dereva huyo (Erasto) ambayo hayakufahamika kwenye eneo la ajali Sekenke kwa kuwa mwili wake uliteketea kabisa na kubaki majivu.

Mjomba wa marehemu Erasto alifun­guka“Erasto alizaliwa Desemba 15, 1993 hapahapa Morogoro.

 

“Alisoma darasa la kwanza hadi la saba katika Shule ya Msingi ya Kihonda na alipomaliza elimu hiyo mwaka 2010, alikwenda Dar kusoma Chuo cha Veta ambapo alihitimu mwaka 2012.

“Baada ya kumaliza Veta alijishughuli­sha na kazi za gereji na baadaye alikuwa utingo kwenye malori hadi mwaka 2018.

JIPYA LA KWANZA

“Jambo ambalo wengi wanaweza wakawa hawalijui ni kwamba Erasto alipata ajira ya kuendesha lori hilo mwezi huuhuu na ukweli ni kwamba alikuwa hata hajapokea mshahara wake wa kwanza. Kiukweli hakuonja hata matunda ya mshahara wake.

“Tarehe 22, mwezi huu wa tatu alipata safari ya kutoka Dar kwenda Uganda kupeleka mzigo wa mafuta na tarehe 23, alilala Singida.

“Alipoamka aliendelea na sa­fari yake na alipofika Mlima Sekenke, wakati anashuka mlima, lori alilokuwa akiendesha lilifeli breki, likamshinda na kupinduka kisha kulipuka moto na yeye na utingo wake wakiwa humo ndani.

“Siyo siri, ukivuta picha walikufa vibaya mno kwani waliungua na kubaki majivu na sehemu chache ya mwili hadi tumeshindwa kuaga maana hatazamiki.”

JIPYA LA PILI

Mjomba huyo alipoulizwa kama mare­hemu alikuwa na familia, alijibu:

“Ndiyo, ana mwanamke, anaitwa Nuru, tunaweza kusema ni mke maana ameishi naye kwa muda mrefu na amezaa naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Elisha.

“Mbali na hilo pia alitarajia kufunga naye ndoa hivyo walikuwa kwenye maandalizi, lakini ndiyo hivyo Mungu amempenda zaidi.”

 

NURU ASHINDWA KUVUMILIA

Kwa upande wake, Nuru alizun­gumza na Uwazi kwa uchungu, lakini alishindwa kuvumilia maumivu ya kumpoteza mwenza wake na kujikuta akiangua kilio kilichosababisha msiba huo kuzizima kwa simanzi na baadhi ya waombolezaji wakajikuta akitokwa na machozi.

“Jamani roho inauma sana, aliniaga kwamba amepata mzigo anakwenda Uganda.

JIPYA LA TATU

“Hakika nilipoteza fahamu nilipopigiwa simu ya kuelezwa kwamba amepata ajali na ameungua vibaya. Kiukweli mume wangu amekufa kifo kibaya sana,” alisema Nuru ambaye alipoteza fahamu baada ya kung’ang’ania kuuona mwili wa mumewe, la­kini aliooneshwa namna uli­yoteketea na kubaki kidogo, aliishia kupoteza fahamu.

 

PADRI AONYA

Naye Padri Msimbe, kwenye mahubiri yake, aliwaonya watu kuacha tabia za kwenda kuc­hunguza kwa waganga ni kitu gani kilichomuua ndugu yao.

“Huko ni kukufuru, haya umeenda kwa huyo mganga, akakwambia aliyemuua ndugu yako ni yule mzee mwenye upara pale mtaani kwako, sasa uk­ishaambiwa hivyo ndiyo ndugu yako atarudi zaidi ya huyo mganga kukuongezea matatizo ya kugombana na watu?” Alihoji Padri huyo ambapo waombolezaji walibaki kimya wakitafakari.

 

 

JIPYA LA NNE

Mwakilishi wa Serikali ya Mtaa, Hilali Hilu, baada ya kutoa salamu na rambi­rambi za mtaa, alisema:

“Erasto alikuwa kijana mwenzetu ali­yekulia hapa mtaani kabla ya kuhamia Dar kwa shughuli za utafutaji. Kama mnavyojua, mtaa wetu uko kandokan­do ya Barabara Kuu ya Dodoma, kila alipopita barabara hii ilikuwa ni lazima asimamishe lori kisha aje kijiweni na kutusalimia.

“Hata wakati akisafiri kwenda Ugan­da alisimamisha lori, akaja kutusalimia kisha akaendelea na safari, kesho yake ndipo tukapata taarifa ya kifo. Kiuk­weli tumeumia sana sisi kama vijana wenzake, kumbe alikuwa akituaga!” alisema Hilali.

 

BREAKING NEWS: Mbowe, Viongozi wa Chadema Wapandishwa Mahakamani