
UNAWEZA kujiuliza alifikiria nini mwanamuziki mkongwe katika gemu la Muziki wa Bongo Fleva, Said Chigunda ‘Chegge’ mpaka kumshirikisha mkongwe mwenziye kwenye gemu la muziki wa asili Bongo, Saida Karoli kwenye ujio wake mpya wa ngoma iitwayo Kaitaba.
Wengine wanaweza kufikiri pengine ni kutokana na ‘idea’ ya wimbo wenyewe na jina lake la Kaitaba ndiyo ilikuwa sababu. Lakini wengine pia wanaweza kufikiri tofauti na kuwa na majibu mengine kichwani mwao. Ukweli ni kwamba, majibu sahihi ya Chegge kumshirikisha Saida anayo mwenyewe.
Katika makala haya, Chegge anafunguka kila kitu juu ya kolabo yake hiyo zaidi ni kuhusu muziki wake na mambo mengine.
Showbiz: Chegge niaje, hongera kwa kazi mpya, inaendaje sokoni?
Chegge: Kiukweli imepokelewa vizuri. Ukitazama kwenye Mtandao wa YouTube, umetazamwa na watu zaidi ya milioni moja na laki mbili. Lakini pia upo kwenye play list za redio zote nchini na umefanikiwa kuchukua Tuzo ya Jiwe la Wiki kutoa Clouds FM.
Showbiz: Hongera sana, lakini nini hasa sababu ya wewe kumshirikisha Saida Karoli kwenye ujio wako?
Chegge: Kisa kilikuwa mdundo. Baada ya kutengeneza mdundo kwa ajili ya kazi yangu mpya na kuusikiliza watu wangu wa karibu waliniambia kwamba ulikuwa ni ujio mzuri ambao una mahadhi ya kitamaduni. Kwa hiyo wakaniambia nimshirikishe Saida. Tukazungumza na meneja wake na kuweza kufanya kazi.
Showbiz: Ilichukua muda gani mpaka kuweza kukamilika?
Chegge: Ilichukua wiki mbili. Saida alikuwa mkoani, alipokuja hapa Dar alirekodi audio na baada ya muda mchache mambo yakaenda vizuri tukarekodi video.

Showbiz: Video umerekodi na nani?
Chegge: Hanscana na imefanyikia hapahapa Bongo.
Showbiz: Kipindi cha nyuma ulikuwa unakwenda nje sana kwa ajili ya video, lakini hivi karibuni unashutia ndani, nini kimebadilika?
Chegge: Wanamuziki tulikuwa hatupati kile ambacho tulitakiwa kukipata. Ubora wa video, ubunifu na mambo mazuri ambayo watu wangependa kuyapata kwenye video. Lakini siku hizi kila kitu tunakipata hapahapa ndani. Kwa hiyo hakuna haja ya kwenda huko nje.
Showbiz: Kuna tofauti gani ya kufanya kazi na mwana-muziki mkongwe na wanamuziki hawa walioibuka siku hizi?
Chegge: Hakuna tofauti sana, kipaji ni kipaji. Akiwa mkongwe ana kipaji anafanya vizuri na hata hawa wanamuziki wapya wenye vipaji nao wapo vizuri.
Showbiz: Kwa hawa wanamuziki wapya wa siku hizi wewe unamkubali nani zaidi?
Chegge: Sina mwanamuziki mmoja ninayemkubali. Wote wanaofanya vizuri ninawakubali.
Showbiz: Vipi kuhusu wewe na Temba, mna project yoyote mmepanga kuifanya hivi karibuni?
Chegge: Yah, lakini atatoa kwanza Temba halafu ndiyo tutakuja pamoja. Siyo muda mrefu kwa sababu muziki wa siku hizi umebadilika. Baada ya miezi miwili mitatu unatakiwa kutoa ngoma mpya.
Showbiz: Na vipi kuhusu wewe mwenyewe, kuna project yoyote baada ya hii umepanga kutoa?
Chegge: Ndiyo. Mwezi ujao, tarehe 20, kuna project nitatoa ikiwemo pia kumtambulisha mwanamuziki wangu mpya ambaye ninamsimamia kwenye gemu. Ni mwanamuziki mzuri sana ambaye anakuja kufanya mapinduzi kwa vijana hawa wapya kwenye gemu.
Showbiz: Tumeona wakongwe wakivuta majiko, vipi kwa upande wako?
Chegge: Bado, nikiwa tayari watu watafahamishwa.
Showbiz: Lolote kwa mashabiki wako?
Chegge: Waendelee tu kusapoti kazi zangu. Ninawapenda na sitowaangusha.
BONIPHACE NGUMIJE