Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo Aprili 04, 2018, katika mkutano wa 11 wa Bunge la 11, amewasilisha hotuba yake inayoelezea mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali.
Hapa chini tumekuwekea baadhi ya mambo aliyoyasema katika hotuba yake:-
“Wananchi wanashuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi cha takribani miaka miwili na nusu tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani.
Mwaka 2018/19 ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake inaliomba Bunge liridhie jumla ya shilingi bilioni 124.95, kati ya fedha hizo, bilioni 66.16 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Bilioni 58.7 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Naliomba Bunge liidhinishe jumla ya bilioni 125.5 kwa ajili ya mfuko wa Bunge, kati ya fedha hizo, bilioni 117.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Bilioni 8.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Ili kufikia malengo ya bajeti, Serikali pamoja na mambo mengine, itaweka mkazo katika kudhibiti upotevu wa mapato, kuimarisha mfumo wa kukusanya mapato hususani kwenye mamlaka ya Serikali za mitaa.
Msukumo utawekwa katika kuhimiza uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.
Rais aliweka wazi dhamira ya Serikali ya awamu ya tano kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kutengeneza ajira nyingi. Ili kufikia azma hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha amani, utulivu na mshkamano wa Kitaifa uliopo kuleta maendeleo endelevu.
Serikali imerahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima baada ya kuanza kuagiza mbolea kwa mfumo wa ununuzi wa pamoja. Hadi Machi 2018, upatikanaji wa mbolea nchini ulikuwa tani 310,674 sawa na 64% ya mahitaji yote ya tani 485,000 kwa mwaka.
Idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2017 imeongezeka hadi kufikikia watalii milioni 1.33 ikilinganishwa na watalii milioni 1.28 mwaka 2016. Mapato yamefikia dola bilioni 2.19 mwaka 2017 ikilinganishwa na bilioni 2.13 mwaka 2016 sawa na ongezeko la 6%.
Takwimu zinabainisha sekta ya utalii ina nafasi kubwa kulipatia Taifa fedha za kigeni na kuzalisha ajira kwa wingi. Tutaendelea kuimarisha sekta hii kwa kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha miundombinu ya maeneo ya utalii pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani.
Kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ni kujenga uchumi wa Taifa unaotegemea viwanda, Hadi Februari 2018, viwanda vipya 3,306 vimeanzishwa.”