
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuhakikisha kuwa askari polisi waliounguliwa nyumba zao mkoani Arusha, ndiyo wanaopaswa kuhamia kwenye nyumba mpya za polisi alizozindua leo mkoani humo.

Rais ameyasema hayo leo Jumamosi, Aprili 7, 2018 mara baada ya kuzindua kituo cha polisi cha Kidiplomasia na Utalii eneo la Naura Jijini Arusha na baadaye nyumba 31 za polisi zilizojengwa kwa ushirikiano wa serikali na wafanyabiashara baada ya zilizokuwepo kuungua moto Septemba mwaka jana.

“Ninataka polisi waliounguliwa nyumba zao ndiyo waingizwe kwenye hizi mpya nilizozindua leo, nafahamu mnaweza mkaleta wengine ambao hawakuuguliwa nyumba. Nataka polisi waliounguliwa tu, wahamie kesho.

“Nyumba za polisi ninazifahamu vizuri, ndiyo zilizonipa mke huyu ambaye baba yake alikuwa polisi, na mpaka amekufa wala hakuwa na cheo, alikuwa ‘staff sergeant’, kwa hiyo maisha ya polisi nayafahamu na yamenitunzia mke,” amesema Rais Magufuli.