ROBERTO Carlos ni mmoja wa wachezaji wenye historia kubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwanza, amebeba taji hilo mara tatu, pia aliwahi kufanikiwa kuwa beki bora wa klabuza Uefa al ipofanya maajabu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2002 na 2003.
Carlos, aliyezaliwa Aprili Mosi, 1973, ni Mbrazili ambaye jina lake kamili ni Roberto Carlos da Silva Rocha. Alianza maisha yake ya soka akiwa fowadi lakini baadaye alibadili namba, na maisha yake karibu yote ya soka alicheza kama beki wa kushoto.
Carlos, 44, amekuwa akitajwa kuwa katika historia ya soka, ni beki namba moja wa kushoto ambaye akili yake inawaza kushambulia zaidi.
Carlos alipewa jina la utani la “The Bullet Man” kutokana na kuwa na miguu yenye nguvu, iliyopiga mipira ya faulo kwa ustadi mkubwa, faulo zake zilipimwa kuwa zilikuwa na uwezo wa kwenda kilometa 169 kwa saa.
Gwiji huyu alijulikana kwa stamina, kasi ya kukimbia, uwezo wa kupiga krosi, kurusha mipira mirefu, na paja lake lilikuwa na ukubwa wa inchi 24 au sentimita 61.
Mwaka 1997, licha ya kuwa beki, Carlos alifanikiwa kuwa mchezaji bora namba mbili wa dunia. Huyu ni mmoja wa mabeki bora zaidi wa kushoto wal iowahi kutokea katika soka. Alipata umaarufu mkubwa akiwa na kikosi cha Real Madrid.
Katika ngazi ya kimataifa , Carlos alicheza kwenye michuano mitatu ya Kombe la Dunia, akaisaidia Brazil kufika fainali mwaka 1998 nchini Ufaransa, na kushinda taji hilo mwaka 2002 Korea/Japan.
Carlos aliichezea Real Madrid kwa misimu 11 ya mafanikio. Klabuni hapo, alishinda mataji manne ya La Liga, na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aprili 2013, alitajwa na Gazeti la Marca la nchini Hispania , kuwa mmoja wa “Kikosi cha Wachezaji 11 Bora wa Kigeni katika Historia ya Real Madrid.”
Pale Madrid, alipewa sifa ya kwamba akiwa upande wa kushoto anaweza kucheza mwenyewe namba tatu na 11, kwa maana ya kukaba na kushambulia. Kocha wa zamani wa Real Madrid, Vicente del Bosque, aliwahi kusema: “Ana uwezo mkubwa wa kulinda na kushambulia mwenyewe eneo lote la kushoto.”

Carlos, alikuwa beki wa kushoto wa kutumainiwa wa Real Madrid kwa misimu kumi mfululizo kuanzia 1996-97 hadi 2006-07. N d i y e mc h e zaji aliyezaliwa nje y a H i s pania, aliyeichezea Madrid mechi nyingi zaidi za La Liga kihistoria (370).
Enzi zake, Carlos alikuwa sambamba na gwiji wa AC Milan, Paolo Maldini, wakitajwa kuwa mabeki bora zaidi wa kushoto duniani.
Katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2002, Carlos anakumbukwa kwa kutoa pasi safi ya bao kwa Zinedine Zidane ambaye alifunga bao linalojulikana kama bao bora zaidi kufungwa katika historia ya michuano hiyo.
Ukiachana na ishu ya kutajwa kuwa beki bora wa Uefa 2002 na 2003, pia alijumuishwa katika timu bora ya Uefa miaka hiyo. Carlos pia alisifika kwa k u funga mabao makali.
Mbrazili mwenzake, Ronaldinho aliwahi kusema kwamba Carlos alikuwa muhimu katika kila ubingwa wa Ligi ya Mabingwa ambao Madrid iliupata akiwemo.
Siku ya mwisho ya msimu wa 2002-03, wakati Real Madrid ikitakiwa kuichapa Athletic Bilbao ili kutwaa ubingwa wao wa 29 wa La Liga, Carlos alifunga bonge la bao kwa faulo na kufanya matokeo kuwa 2-1, mwisho Madrid ilishinda 3-1 na kutwaa ubingwa.
Desemba 6, 2003, Carlos alifunga bao la kwanza walipoichapa Barcelona katika Uwanja wa Camp Nou, huo ulikuwa ushindi wa kwanza wa Real Madrid kwenye uwanja huo katika kipindi cha miaka 20.
Bao lake la mwisho Real Madrid lilikuwa la ushindi katika dakika za nyongeza dhidi ya Recreativo de Huelva msimu wa 2006–07. Bao hilo liliisaidia Madrid kubeba ubingwa wake wa 30 wa La Liga, ambapo walikuwa sawa kwa pointi na Barcelona lakini wakawa mabingwa kwa faida ya uwiano mzuri walipokutana ‘head to head’.
Carlos alistaafu soka rasmi Agosti 2012, akiwa na umri wa miaka 39. Alirejea dimbani katika kikosi cha Delhi Dynamos lakini alicheza mechi tatu tu.
MATAJI
Palmeiras:
Ligi Kuu ya Brazil (Campeonato Brasileiro Série A (2): 1993, 1994
Campeonato Paulista (2): 1993, 1994
Torneio Rio-São Paulo: 1993
REAL MADRID:
La Liga (4): 1996–97, 2000–01, 2002–03, 2006–07
Supercopa de España (3): 1997, 2001, 2003
Ligi ya Mabingwa Ulaya (3): 1997– 98, 1999–2000, 2001–02
Intercontinental Cup (2): 1998, 2002
Uefa Super Cup: 2002
FENERBAHÇE:
Turkish Super Cup (2): 2007, 2009
BRAZIL:
Kombe la Dunia: 2002
Copa América (2): 1997, 1999
Kombe la Mabara: 1997
MAISHA BINAFSI
Roberto Carlos amemuoa mwanamke mrembo wa Kibrazili, Mariana Luccon tangu 2009. Ana watoto nane, wa kiume wanne na wa kike wanne.
ANACHOKIFANYA KWA SASA
Baada ya kustaafu soka, Carlos alianza ukocha. Alikuwa kocha wa Sivasspor katika Ligi Kuu ya Uturuki kuanzia 2013, alijiuzulu Desemba 2014. Kuanzia Julai 2015, ni kocha wa Delhi Dynamos.