
WAKAZI wawili wa Dar es salaam, Ashura Ramadhan na Abbas Awadhi waliibuka kidedea baada ya kuwa washindi katika shindano la shika ndinga linaloendeshwa na kituo cha Redio cha Efm na Tv E.

Ashura Ramadhan mkazi wa Bunju alipiga simu na kupata nafasi hiyo kupitia kipindi cha uhondo ambapo mshindi mwingine ni Abbas Awadhi, ambaye ni mkazi wa Mwananyamala aliyeshiriki shindano hilo kupitia kipindi cha Genge kinachoendeshwa na kituo hicho cha redio. Hafla ya kuwapata washindi hao ilifanyika siku ya Jumamosi katika Viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi za washindi hao Meneja Mkuu wa Efm na Tv E, Dennis Busulwa alisema kuwa washindi hao wameshinda pikipiki na kupatiwa tiketi ya kushiriki fainali za shika ndinga zitakazo fanyika Dar es Salaam mara baada ya kuwapata washindi wa mikoani.

Busulwa akikabidhi pikipiki hizo alisesema kuwa siku ya jumatatu (jana) washindi hao watafika katika ofisi za Efm na Tv E kwa ajili ya kubadilisha majina ya kadi za pikipiki hizo kutoka jina la kampuni kwenda majina yao.

Washindi hao walipatikana siku ya jumamosi kupitia mchakato ulioanza asubuhi kwa mbio za kukimbia na vikombe vya maji kisha kufikia hatua ya pili ya kukimbia na mayai ambayo iliwapeleka kufika katika fainali na kuibuka kidedea.