
UNAPOZUNGUMZIA muziki kwa nchi ya Afrika Kusini upo tofauti, kila msanii anakubalika kutokana na jiji analotoka tofauti kabisa na Tanzania ambapo wanamuziki wanaokubalika nchi nzima ni Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Alikiba huku wengine wakikubalika kawaida.
Katika gazeti ndugu na hili la Ijumaa Wikienda kwenye upande wa burudani ‘Over Ze Weekend’ nilielezea safari yangu ya Johannesburg nchini Afrika Kusini mapema wiki hii hususan kwa upande wa burudani.
Nilielezea jinsi muziki kwao ulivyo na mashabiki wanavyowakubali wasanii kutoka katika majiji yao. Nilielezea Jiji la Cape Town ambalo kimuziki lina mkali wao anaokubalika ‘top’ ambaye ni mwanadada, Shekhinah Thandi Donnell ‘Shekhinah’ na ukizungumzia shoo mbalimbali mwanadada huyu amekuwa akisepa na kijiji.
Pia nilielezea Jiji la Durban, ambalo nalo mkali wao ni DJ Tira ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Kwaito akiwa na ngoma yake ya Woza Durban iliogeuka na kuwa wimbo wa taifa katika jiji hilo.
Leo tutaangalia Jiji la Johannesburg ukipenda waweza kuliita Jozi ambalo ni kubwa kuliko majiji yote Afrika Kusini likiwa pia miongoni mwa majiji 50 makubwa duniani.
Jiji hili pia linaloongoza kuwa na wasanii wengi kwa nchi nzima, hapo wapo wanaofanya Muziki wa Injili, Kwaito, Afro Pop na Hip Hop.Katika makala haya nachambua baadhi ya wasanii hao.

CASSPER NYOVEST
Wengi wanamuita mwanamuziki wa Hip Hop milionea Afrika Kusini. Ni mzaliwa wa nje kidogo ya Johannesburg akiwa amekulia maisha ya uswahilini hadi anafanikiwa.
Kama ulikuwa hujui, Cassper ndiye kinara wa wanamuziki wanaopendwa zaidi katika jiji hili akiwa na rekodi kibao za kujaza mashabiki zaidi ya 20,000 katika uwanja wa mpira wa miguu wa Dome na kuuza zaidi ya tiketi 60,000 katika tamasha lake ndani ya Uwanja wa Mpira wa FNB na kuwa msanii wa kwanza Afrika Kusini kujaza katika shoo kuliko yeyote kuwahi kutokea ndani na nje ya jiji hili.

AKA
Rapa huyu anashikilia nafasi ya pili miongoni mwa wakali wa Hip Hop wanaopendwa katika Jiji la Johannesburg. Kama ilivyo kwa Cassper, mara nyingi AKA amekuwa akifashindanishwa na Cassper kutokana na kuwateka mashabiki sambamba na kujitengenezea mashabiki wengi lakini ukweli unabaki kuwa Cassper yupo juu yake.

BLACK COFFEE
Wakazi wa jiji hili, wanampa nafasi ya tatu miongoni mwa wakali wanaopendwa katika akiwa ni mzaliwa wa Durban. Black siyo Mwanahip Hop bali anafanya Muziki wa Afro Pop na Afro House ambao umetokea kumpatia mafanikio ya kufanya shoo nyingi za kuimba na kupiga kama DJ ndani na nje ya jiji hili.
Jamaa huyu anayetumia mkono mmoja kutokana na mwingine kupata matatizo, anaheshimika sana kutokana na mchango wake katika kuliwakilisha jiji hili nje ya nchi. Ameshawahi kualikwa na kufanya shoo katika matamasha makubwa duniani kama vile Coachella ya 2017 na 2018 nchini Marekani akipanda jukwaa moja na Kundi la Migos, wakali kama Card B, Beyonce, Justin Bieber na wengine kibao.

DJ MAPHORISA
Jamaa huyu ambaye ni mzaliwa wa Pretoria kipaji chake cha kuimba ni cha kipekee ukiachilia mbali kazi yake ya U-dj.
Anapendwa zaidi na mashabiki wa jiji hili kutokana na kupenda kutumia staili ya kuchanganya lugha mbili ya Zulu na Xhosa katika nyimbo zake kiasi cha kubatizwa jina la mfalme wa staili ya Gqom ambayo huimbwa kwa kuchanganya lugha hizo.
Historia ya mkali huyu naambiwa kuwa ni mtu wa kutafuta sana ‘chaneli’, hadi sasa ameshafanikiwa kufanya kolabo na wakali kibao nje na ndani ya jiji hili akiwemo Wizkid (Nigeria), Chegge na Temba (Tanzania), Rayvanny (Tanzania), Drake (Marekani) na Runtown (Nigeria).
MAKALA: ANDREW CARLOS ALIYEKUWA AFRIKA KUSINI