×

KAFULILA: TRIL 1.5 SIYO KITU KIPYA, MWAKA 2012/13 ILIKUWA TRIL 3.48

Na David Kafulila
Kumekuwa na uvumi unaosambazwa na baadhi ya wanasiasa kwamba kuna ufisadi wa 1.5 trn kufuatia ripoti ya CAG kwa ukuguzi wa hesabu za 2016/17. Na hata baada ya majibu ya Serikali kutolewa kupitia Naibu Waziri kumekuwepo baadhi wakipinga ufafanuzi huo bila hoja mahususi;
1. Ieleweke kwamba msingi wa hoja hii ni ukurasa wa 34 ripoti ya CAG alipoandika kwamba matumizi yote yalikuwa trilioni 25.3 wakati mapato ni trilioni 23.8.
2. Ifahamike kwamba katika ripoti hizo, CAG hakuhoji tofauti hiyo ya 1.5 trilioni kwa sababu ni kawaida katika mfumo wa ripoti zao kwani nimekagua ripoti za CAG kuanzia mwaka 2012 mpaka 2018, hakuna mwaka ambao mapato na matumizi vimelingana kama inavyoshinikizwa leo kwa nia ya kupotosha wasio jua.
3. Watanzania wajiulize kama hesabu za ripoti zipo hivyo miaka yote kwann leo aje mtu kufanya tofauti hiyo kuwa hoja kama sio kucheza na akili za Watanzania? Muulizeni huyo aliyetengeneza hoja hiyo, kwa nini mwaka Jana ripoti ya CAG ukurasa wa 46 ulionesha mapato ilikuwa trilioni 21.108 huku matumizi yakiwa trilioni 20.020 sawa na tofauti ya Trilioni 1.088, lakini hawakuhoji?
Au muulizeni Ripoti ya CAG kwa hesabu za 2012/13, Mapato yaliandikwa Trilioni 15.018 wakati matumizi yakiwa Trilioni 11.531(ukurasa 115-120) sawa na tofauti ya Trilioni 3.486, kwa nini haikuwa hoja?
4. Hoja ya Naibu waziri fedha kwamba kwenye mfumo wa IPSAS ambao Tanzania ilianza kutumia mwaka 2011, kwamba katika mfumo huo kuna baadhi ya takwimu ni mapato tarajiwa mtu hawezi kuzipinga kizembe kwa hoja kuwa ameongoza Kamati ya PAC kwa miaka 8.
“Kwahiyo ana mamlaka ya kuaminika anachosema, hoja ya Naibu Waziri inathibitishwa na Ripoti ya bodi ya shirikisho la wahasibu dunia ya – ACCA ( Association of Chartered Certified Accountants,) ndani ya ripoti yao ya Oktoba2017, ukurasa15. Unaeleza changamoto hiyo, ninukuu”…
More over the financial reporting frame work used IPSAS accrual accountings , while the budget was compiled under cash basis , so some entries based on accruals and other on cash”, hii ni sehemu ya ripoti hiyo ya ACCA ikithibitisha alichosema Naibu Waziri fedha bungeni kwamba wakati bajeti inatengenezwa katika mfumo wa cash lakini ripoti za fedha zinatengenezwa katika mfumo wa acrual ambapo mapato au matumizi tarajiwa yanaingizwa.
5. Yote haya yanafanyika kucheza na akili za watu, ndio maan a Zitto anathubutu kusema Serikali kupata hati isiyoridhisha nisawa na kupata hati chafu, huu ni upotoshaji wa maksudi kwani hati isiyoridhisha inaitwa ” qualified audit opinion” wakati hati chafu inaitwa ” Adverse audit opinion”. Sasa wahasibu duniani wanashangaa mwanasiasa Tanzania anaposema qualified audit opinion nisawa na adverse audit opinion.
6. Ukweli nikwamba hesabu jumuifu ( consolidated accounts) zina hati isiyoridhisha, kwa maana ya qualified audit opinion na sio hati chafu kwa maana ya adverse audit opinion. Na suala la hesabu jumuifu kuwa na hati isiyoridhisha halijaanza Leo na Rais Magufuli, Zitto amekuwa Mwenyekiti wa PAC miaka8, awambie watanzania ni lini hesabu jumuifu zilipata hati safi ya CAG.
Ni ngumu kwani hata kwenye nchi zenye mifumo madhubuti kama Uingereza, hesabu jumuifu zina hati isiyoridhisha kwa miaka6 sasa kuanzia 2011/12, sasa itakuwa Tanzania ambayo bado kimifumo ndio inakua na sasa hesabu jumuifu ( consolidated accounts) ni pamoja na hesabu za vyama vya siasa, ambavyo 7 vimepata hati chafu?
7. Jambo la msingi tukubaliane kwamba baada ya majibu ya Serikali hakuna mwenye uwezo wala upeo wa kutwambia ukweli wa mwisho zaidi ya CAG kupitia Kamati ya PAC kama kutatokea mjumbe wa kamati kuhoji tofauti hiyo, nasema kama kutatokea mjumbe wa Kamati kuhoji kwasababu jambo hili halimo wala sio miongoni mwa hoja za CAG katika ripoti yake ya ukaguzi wa 2016/17.
Wabunge wana haki hiyo na Serikali inawajibu huo na bila shaka CAG ikikagua na kukuta kasoro yoyote JPM ni Kiongozi thabiti kuchukua hatua hasa inapohusu Mali ya Umma, lakini hawezi kuchukua hatua yoyote malalamiko ya jumlajumla. Tusubiri PAC/ CAG, hakuna njia ya mkato. Ndio utaratibu!