
HABARI hii inasikitisha sana! Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Mudrick Abdallah amedaiwa kumpa kipigo mwanamke aliyekuwa mkewe, Fatma Addy kiasi cha kumpofua jicho, baada ya kumkuta akizurura baa na mtoto aliyezaa naye, Risasi Mchanganyiko lina kisa na mkasa.
Abdallah na Fatuma walikuwa mume na mke kabla ya kuachana kwa talaka, lakini mtoto waliyemzaa pamoja alilazimika kubaki na mama yake kutokana na sheria inayotaka mtoto mwenye umri wa chini ya miaka saba kubaki na mzazi wa kike kwa ajili ya malezi ya karibu.
NINI KIMETOKEA?
Fatuma ambaye ni Mkazi wa Kigogo-Mbuyuni jijini Dar es Salaam, alikumbana na adha hiyo na kuporwa mtoto huyo wa mwaka mmoja na miezi
mitatu katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar.
Habari zilidai kuwa, Fatma alikutwa na mumewe huyo wa zamani akiwa anapiga kilevi huku akimnyonyesha mtoto huyo.

TUJIUNGE ENEO LA TUKIO
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, tukio hilo lilijiri Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Leaders Club ambapo Fatma na mtoto huyo walikwenda kuangalia bonanza lililoratibiwa na bia.
Baada ya kupata taarifa hiyo huku chanzo kikiishia hapo, gazeti hili lilisaga soli kumtafuta Fatma ambaye ilidaiwa kuwa alichezea kipondo cha hatari ambapo alipopatikana alisimulia mkasa mzima.
MKE ASIMULIA
“Mume wangu alikuwepo pale (Leaders) na mtoto wake ambaye mimi nilivyoondoka kwake nilimuacha naye.
“Tukawa wote, lakini baada ya muda kidogo, mimi nilitoka kwenda chooni, sasa kuna mwanaume mmoja alikuwa ananiulizia choo kilipo, nikawa ninamuelekeza.
“Mume wangu alipoona hivyo alikuja na kuanza kunitukana na kuniambia mimi ni Malaya.
“Basi kuanzia hapo alianza kunipiga makofi ya usoni, huku akinitishia kuniharibu sura ili nisipendwe na wanaume wengine. Mimi nilimshangaa na kumuuliza kwa nini anionee wivu wakati mimi siyo mke wake tena?
“Hapo ndipo alipozidisha kunipiga hadi akanipofua jicho na kuninyang’anya mtoto ambaye bado ananyonya.”

ATOKWA MACHOZI KWA JICHO MOJA
Mwanamke huyo alieleza kuwa, jamaa huyo alimnyang’anya mtoto kwa maelezo kuwa hawezi kumlea, hivyo aliamua kumwachisha kunyonya na kumchukua.
“Tukio hilo lilinifanya nikimbilie katika Kituo cha Polisi cha Magomeni kwa ajili ya kuchukua Fomu ya Matibabu (PF-3),” alisema Fatma akitokwa machozi kupitia jicho moja.
Alisema kuwa, Jumapili iliyopita alijaribu kumpigia simu mumewe huyo ili ampelekee mtoto, lakini bado aliendelea kumtukana.
“Mimi bado nina maumivu makali mno na siwezi kutoka nje matiti yanauma tu kwa kuwa nilikuwa ninanyonyesha, ninachomuomba aniletee mtoto maana atakuwa anateseka na hayo mambo mengine ya kunipiga nitahakikisha sheria inachukua mkondo wake,” alisema Fatma.
KAULI YA MUME
Ili kupata mzani wa habari hiyo, baada ya kumsikia Fatma, Risasi Mchanganyiko lilimgeukia Abdallah kuhusu tukio hilo ambapo alikiri Fatma kuwa mkewe wa zamani aliyempa talaka.
“Siku hiyo mimi nilimpigia simu aje Leaders kwa kuwa mimi ni mwalimu wa timu ya watoto na wanawake. Palikuwa na bonanza, tukawa tupo pamoja pale na mtoto kwa upendo tu,” alisema Abdallah.
Jamaa huyo aliendelea kusema kuwa, ilipofika muda wa kuondoka, Fatma alitaka kuondoka naye, lakini yeye aligoma akimuahidi kwamba angeenda nyumbani kwake siku iliyofuata.
“Baada ya hapo akanianzishia vurugu na kujazia watu mpaka kufikia kile kilichotekea.
“Mimi ikabidi nimchukue mtoto wangu niondoke naye,” alisema mwanaume huyo bila kufafanua kilitokea nini baada ya mkewe huyo kumwanzishia vurugu kama anavyoeleza.

MAISHA YAO YALIKUAJE?
Fatma na Abdallah walioana Julai 31, mwaka 2015 na kuishi maeneo ya Kigogo jijini Dar es Salaam. Baadaye walifanikiwa kujenga nyumba yao maeneo ya Chanika na kuhamia huko kwa ajili ya kufanya maisha.
“Wakati ninafunga ndoa na mume wangu nilikuwa ninafanya kazi katika Kampuni ya Bia ya Serengeti.
“Baadaye tulikubaliana kwamba niache kazi ili nilee watoto. Wakati huo mwenzangu alikuwa na mtoto mmoja na mimi nilizaa naye mtoto mmoja wa kiume,” alisema Fatma.
Hata hivyo, alisema kuwa, alilazimika kuachana na mume huyo kutokana na tabia yake ya kuzua ugomvi nyumbani kila siku akiwa amelewa.
“Oktoba, mwaka jana mwenzangu (mume) alianza kubadilika. Alikuwa akinipiga kila anaporudi nyumbani. Alikuwa akinitishia kuniua wakati wowote,” alidai Fatma na kuendelea:
“Ilipofika Desemba, mwaka jana, mambo yakazidi kuwa ovyo kwenye ndoa, kuna wakati alikuwa haonekani nyumbani.
“Siku ziliposonga ndipo ‘akakauka’ nyumbani. Baada ya hapo tulipelekana kwenye taasisi mbalimbali na ndipo akakubali kutoa talaka, sasa ninashangaa wivu wa nini tena?”
Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne ili kujua kama analifahamu tukio hilo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa.
STORI: Neema Adrian, Risasi Mchanganyiko.