
GEITA: Ukiambiwa usifanye hivi ukakaidi yatakukuta tu; ndivyo ilivyokuwa kwa bwana harusi, Saayai Petro na baba mkwe wake aitwaye Kashirimu Mashimba ambao hivi karibuni walijikuta wakitiwa pingu na polisi huku binti wa miaka 14 akitajwa kuwaponza.
Mashimba na Saayai walimfanyaje mtoto huyo? Habari kutoka Kata ya Kanyara mkoani Geita zinasema, watu hao wanatuhumiwa kumwachisha masomo binti huyo (jina linalindwa) na kumwingiza kwenye ulimwengu wa maisha ya ndoa.

Inaelezwa na vyanzo vya habari kwamba, msichana huyo alikuwa amefaulu mtihani wake wa darasa la saba mwaka jana na kutakiwa kujiunga na Shule ya Sekondari Kasamwa lakini hakufanya hivyo baada ya kuamriwa na baba yake aolewe.
Uamuzi wa kumzuia mwanaye asijiunge na msomo ya sekondari unatajwa kuwa ulichochewa na mzee Mashimba kubabaikia zaidi mahari ya ng’ombe watano aliyopewa na Saayai.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kukamatwa kwa watu watatu kuhusiana na tukio hilo.
“Hadi sasa tunawashikilia watu watatu ambao ni dada wa binti, baba mzazi pamoja na kijana ambaye ndiye muoaji,” alisema Kamanda Mwabulambo.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kanyara, Augustino Kazanza amesema kuwa walibaini kuwa binti huyo ameozeshwa kutokana na kupata taarifa kwa wananchi wenye mapenzi mema na taifa nao kuliarifu Jeshi la Polisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi amelaani kitendo hicho cha kuozwa binti huyo na kuwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa dhidi ya watu ambao wanawaozesha wanafunzi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kahama, Mhandisi Modest Aporinaly amesema kuwa bado kuna changamoto ambazo zimeendelea kujitokeza kwa watoto wa kike wanaosoma.
“Moja ya changamoto kwa wanafunzi wa kike ni kuozeshwa na kupata mimba wakiwa shuleni kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuendekeza mali na kuacha kuwapa elimu wasichana wao,” alisema mkurugenzi huyo wa mji.
Stori: Joel Maduka, Amani.