
Meneja Masoko wa Kampuni ya Umeme wa Jua, Seth Matemu (wa pili kushoto) akizungumza jambo.


WAPENZI wa Soka vijijini kunufaika na michuano ya Kombe la dunia mwaka huu, hii ni kutokana na Kampuni ya Star Times ambayo ina mkataba hapa nchini wa kutangaza mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA 2018, yatakayofanyika nchini Urusi kuanzia mwezi ujao, kampuni hiyo imeingia ushirikiano na kampuni ya kusambaza nishati ya jua na vifaa vinavyotumia nishati hiyo ya Mobisol, kutumia mtandao wake kuwezesha wananchi wanaoishi maeneo yasio na umeme wanaotumia nishati ya umeme wa jua nchini na nchi jirani za Kenya na Uganda kutokupitwa na mashindano hayo ya kihistoria duniani kote.
Ushirikiano huo ambao umetangazwa leo jijini Dar es Salaam unawezesha wateja wanaotumia umeme na vifaa vya Mobisol kununua vifaa maalumu vya kuboresha mawasiliano vitakavyowezesha kushuhudia mechi za kombe la dunia, sambamba na kupata chaneli mbalimbali za burudani kupitia vingamuzi vya Star Times.
Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Mobisol Tanzania, Gerald Matemu , ameeleza kuwa wateja wa Mobisol nchini, wanaweza kununua vifaa vya mawasiliano kutoka star Times vitakavyowawezesha kufurahia burudani hiyo ya soka bure na kwa wakati wote kuanzia sasa hadi mwisho wa mwezi Julai mwaka huu. Vifaa hivyo baada ya kununuliwa wanafungiwa bure popote walipo.
“Tunafurahia kuingia ushirikiano huu na Star Time, hasa kwa kuwaletea ofa maalumu wananchi wanaotumia umeme wa nishati ya jua maeneo mengi yasiyo na umeme ili kuwawezesha kupata burudani za mashindano ya Kombe la Dunia, Mobisol tutahakikisha tunaendelea kusambaza umeme kwenye maeneo yasio na nishati hiyo sambamba na kubuni vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati ya jua,”Alisema Patric Juma.
Naye Meneja Masoko wa Star Times Tanzania, David Malisa,alisema “kampuni yao inayo furaha kufanya kazi na Mobisol katika kuhakikisha familia nyingi zinazotumia umeme wa mtandao wake wanaweza kutumia ving’amuzi vyao na vifurushi maalum vitakavyowawezesha kuangalia mashindano ya Kombe la Dunia ambapo kampuni yao ndiyo yenye hakimiliki ya kutangaza mashindano haya makubwa ya soka duniani.”
Kampuni ya Mobisol imeweza kusambaza umeme wa jua wenye nguvu mpaka 10MW kwa kaya zaidi ya 500,000 katika nchi za Afrika Mashariki pia inasambaza vifaa bora na vya kisasa vinavyotumia umeme wa jua kwa gharama nafuu vyenye uwezo wa kutumia umeme wa 40W hadi 200W,vifaa ambavyo inasambaza mbali na vya kuwasha na kuchaji simu pia inasambaza vyombo vya muziki na Televisheni bapa za kisasa zenye ukubwa tofauti.