
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ametoa taarifa rasmi bungeni kuhusu kifo cha MBUNGE wa Jimbo la Buyungu, wilayani Kakonko Mkoani Kigoma kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kasuku Samson Bilago aliyeaga dunia juzi Jumamosi, Mei 26, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Spika, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson amesema kabla ya kupelekwa Muhimbili, Bilago alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya DCMC iliyopo Dodoma na hali yake ilipobadilika, ndipo akahamishwa kwa matibabu zaidi.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa Spika amepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Bilago huku akiwapa pole wabunge wote kwa msiba huo mkubwa.
Aidha kikao cha pamoja baina ya Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi ya Bunge kimefanyika leo na kukubaliana kuwa, mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Marehemu Kasuku Samson Bilago utapelekwa Bungeni jijini Dodoma, kesho Jumanne Mei 28 kwa ajili ya wabunge kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Kigoma kuzikwa.