
SIMANZI na majonzi yametawala katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma wakati wabunge walipokuwa wakiuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kigoma, Kasuku Bilago aliyeaga dunia Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Bilago, Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema Bilago alikuwa ni zawadi kwa wananchi wa Kigoma na Tanzania.

“Tumekusanywa hapa na Mwalimu Bilago, Bungeni alikuwa anatuchekesha, anatunyamazisha, kila alipokuwa akisimama kuzungumza kila mmoja wetu aliacha alichokuwa anakifanya na kumsikiliza, leo amenyamaza hatusikii.
“Alikuwa zawadi kubwa kwa Watanzania na watu wa Kigoma, alikuwa mwalimu na mtu wa kusamehe. Hii ni safari yetu sote,” alisema Zitto.