
Manispaa ya Kinondoni imeingia makubaliano ya ujenzi wa barabara zenye thamani ya shilingi Milioni 39.062 zinazotarajia kujegwa katika Kata ya Tandale, Mburahati pamoja na Mwananyamala.
Akizungumza katika hafla ya kutiliana saini ya Mikataba ya Ujenzi baina ya serikali na wakandarasi, Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Kinondoni Aron Kagurumjuli amesema kuwa Kampuni ya CRJE East Africa Ltd na China Railway South Group Co. Ltd zimefanikiwa kushinda zabuni katika miradi hiyo.
Kagurumjuli ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hizo utakuwa katika kiwango cha Lami, mifereji, Taa, njia za watembea kwa mguu pamoja na vyoo katika Kata ya Tandale na Mburahati.
Amefafanua kuwa tayari wakazi wote wa maeneo hayo ambayo mradi huo utapita wamelipwa fidia, hivyo wakandarasi wanatarajia kuanza kazi muda wowote kuanzia sasa.
Akizungumza katika hafla hiyo Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta, amesema kuwa serikali itaendelea kuwajali wananchi wake kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara.
Sitta amaeleza kuwa serikali inatumia gharama kubwa katika kujenga mradi wa barabara, hivyo wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kiwango kinachostahili.
Hata hivyo ameishukuru serikali Kuu pamoja na Ofisi ya Rais kwa kufanikisha mradi huo.