×

Kwa Nini Wanaume Wanaongoza kwa USALITI?-2

  TUNAENDELEA na mada tuliyoianza wiki iliyopita. Ieleweke kwamba lengo langu si kuonyesha kwamba kundi moja ni bora kuliko kundi jingine, tunazungumzia hali halisi, ukweli ambao haupingiki kwamba wanaume wanasaliti zaidi kuliko wanawake.

Tulianza kwa kuangalia sababu za kitaalamu kwa nini wanaume wanasaliti zaidi kuliko wanawake na jambo la msingi nililosisitiza ni kwamba katika kila usaliti unaotokea lazima utakuwa umesababishwa na matatizo katika mapenzi au matatizo ya mhusika mwenyewe.

Hakuna mtu anayesaliti isipokuwa kwa moja kati ya sababu mbili nilizozieleza hapo juu, matatizo katika mapenzi au matatizo ya mtu binafsi. Tuliona kwamba sababu ya kwanza inayofanya wanaume wengi wawasaliti wenzi wao ni tendo la ndoa, kwamba mwanaume kama anakosa huduma hii muhimu ndani ya ndoa au ndani ya uhusiano, ataitafuta nje.

Sababu nyingine tuliona kwamba ni tabia mbaya tu ambayo mtu anakuwa nayo. Wapo wanaume ambao wameumbwa na tabia mbaya ya kutamani kila mwanamke anayepita mbele ya macho yake.

Pia tuliangalia sababu nyingine kuwa ni kukosa kujiamini, wapo wanaume ambao kila siku anaamini kwamba mwanamke aliyenaye ipo siku atamkimbia na kumuacha kwenye mataa, sasa anaamua kujihami kwa kuwa na mchepuko pembeni ili siku mambo yakiharibika, awe na wakumtuliza.

Leo tunaendelea na sababu nyingine zinazoweza kusababisha mwanaume akafikia hatua ya kusaliti ndoa au uhusiano wake na kutoka kimapenzi na mwanamke mwingine.

KURUKA STEJI

Umewahi kukutana na mwanaume mtu mzima ambaye japokuwa yupo kwenye ndoa na ana familia, pengine ana watoto wakubwa lakini bado anaendekeza kuchepuka hovyo, tena wakati mwingine na wasichana ambao anaweza hata kuwazaa? Basi kitaalamu tatizo hili huwa linaitwa ‘second adolescence.’

Nitakuja kulielezea vizuri siku nyingine maana ni mada inayojitegemea lakini kwa kifupi ni kwamba wanaume wengi huwa wanasumbuliwa na tatizo la kuruka hatua za ukuaji, matokeo yake wanakuja kufanya mambo ya kitoto wakiwa tayari ndani ya familia.

KULEGALEGA KWA MAWASILIANO

Sababu nyingine inayosababisha wanaume wengi kusaliti, ni kulegalega kwa mawasiliano kati ya mume na mke. Wanawake wengi wakishaingia kwenye ndoa, huwa wanajisahau suala zima la mawasiliano.

Hawezi kumpigia simu mumewe kumjulia hali akiwa mbali kama ilivyokuwa enzi za uchumba. Hawezi kumtumia japo meseji kumuuliza anaendeleaje na kazi, akipiga simu basi ujue nyumbani kuna tatizo.

Mwanaume wa aina hii, akikutana na mwanamke ambaye mara kwa mara anampigia simu na anamtumia meseji kumchangamsha, hujikuta akiangukia kwenye mapenzi na mwanamke huyo na mwisho huwa ni wawili hao kuangukia dhambini.

Wanawake wanashauriwa kuwa na mazoea ya kuwapigia simu waume zao mara kwa mara, wakati mwingine mpigie kumuuliza anapenda umpikie chakula gani au atarudi saa ngapi kazini. Hiyo humfanya muda mwingi awe anakuwaza na kukufikiria.

IMANI

Wapo baadhi ya wanaume ambao huwa na imani kwamba mwanaume aliyekamilika lazima awe na zaidi ya mke au mpenzi mmoja. Zipo dini ambazo zinaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja lakini zipo hatua ambazo ni lazima uzifuate na siyo kukimbilia kuchepuka kwa kisingizio kwamba dini inaruhusu.

Pia wengine wanakuwa wanafuata mila na tamaduni za maeneo waliyotoka kwamba mwanaume lazima awe na zaidi ya mke mmoja.

Jambo la muhimu ni kujua kwamba hakuna kitu kinachoumiza kama usaliti, kama kweli unampenda jitahidi kuwa mwaminifu kwake, mlinde na muoneshe kwa vitendo kwamba unampenda.