
Taasisi ya Wazalendo nchini kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa na Fahamu (MOI) jana waliendesha zoezi la uchangiaji wa damu kwa hiyari ambapo mamia ya vijana wazalendo walijitokeza katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichopo Mlimani kujitolea damu.

Katika zoezi hilo Taasisi ya Wazalendo ilikusanya vijana wenye moyo wa kizalendo kutoka sehemu mbalimbali na kuwashirikisha madaktari MOI katika zoezi la kuwatoa damu vijana hao.

Kabla na baada ya zoezi hilo madaktari hao waliwapa ushauri waliojitolea damu na kuwapa cheti maalum cha uchangiaji wa damu ambapo cheti hicho kitawawezesha kupata msaada wa damu ya dharura bure katika hospitali yeyote ya serikali endapo watapatwa na dharura inayohitaji kuongezwa damu.

Akizungumza katika zoezi hilo Mwenyekiti wa Taasisi ya Wazalendo, Allain Seth aliwashukuru wote waliojitolea damu zao kwa moyo wa kizalendoi wa kuwasaidia wamama wajawazito, majeruhi na wahitaji wengine wa damu ya dharura.
HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS