
MKURUGENZI wa Vipindi wa Televisheni ya Wasafi, Zamaradi Mketema ambaye alijizolea umaarufu kupitia Kipindi cha Take One kilichokuwa kikioneshwa kupitia Clouds TV ameibuka na kueleza kuwa, mtoto aliyemzaa juzikati si wa mwisho pamoja na kuwa ni wa tatu kwani anatarajia kuzaa watoto wengi kama wazee wa zamani.
Akipiga stori na Risasi Jumamosi, Zamaradi aliongea mambo mengi pamoja na hilo la kuongeza watoto.
Fuatilia mahojiano hapa chini;
Risasi Jumamosi: Hongera kwa kujifungua, sasa wewe ni mama wa watoto watatu je, ndio umemaliza au tutarajie mtoto mwingine?
Zamaradi: Hapana sijamaliza, nitazaa kama wazee wa zamani kwani watoto ndio faraja yangu. Kwetu tumezaliwa wachache hivyo ni lazima nitaongeza tu.
Risasi Jumamosi: Ni utofauti gani uliopo wakati unalea mwenyewe watoto wako wawili wa mwanzo kabla ya ndoa na sasa hivi mtoto huyu wa tatu
ukiwa na baba yake pembeni?
Zamaradi: Siyo kwamba kwa sababu sikuwa kwenye ndoa basi watoto wangu hawakuweza kupata mapenzi ya baba, hapana! Walikuwa wanapata kila kitu na baba yao aliwajibika vilivyo, utofauti wa sasa ni kwa sababu tuko kwenye ndoa na mwanzoni sikuwa namuweka sana baba yao mitandaoni kama ilivyo kwa mume wangu sasa hivi.
Risasi Jumamosi: Mtoto wako huyu wa tatu ameongeza nini kwenye maisha yako?
Zamaradi: Ameongeza vitu vingi vizuri kwani ni mtoto na mimi kila mtoto kwangu ni faraja ingawa mtoto wangu wa kwanza alinifanya kuwa na furaha sana kwa sababu alinifanya kuitwa mama kwa mara ya kwanza.
Risasi Jumamosi: Kwa nini mtoto wako ulimuita Salah?
Zamaradi: Kwanza baba yake anampenda sana mchezaji huyo lakini pia kwangu niliona ni jina zuri na lina maana nzuri ambayo ni amani.
Riasasi Jumamosi: Watu wengi walijua ungepata mtoto wa kike kwa jinsi ulivyokuwa ukijiweka lakini pia hata wewe ulijua ni mtoto wa kike, ilikuaje akawa wa kiume?
Zamaradi: Ni kweli kabisa nilijua ni mtoto wa kike kwa sababu niliangalia mara tatu wakani-ambia ni wa kike, mara ya mwisho naangalia naambiwa ni wa kiume, sikuamini nikasema watu wote hawawezi kukosea akapatia mmoja ndio maana nilikomaa na vitu vya kike lakini namshukuru Mungu na nimefurahi kumpata Salah.
Risasi Jumamosi: Vipi kuhusu nyaku-nyaku’ hawakupi shida kwa mumeo?
Zamaradi: Nyakunyaku ndio nini? Ninachojua hakuna nyakunyaku hata siku moja ila ukiona nyakunyaku kamchukua mumeo ujue riziki yako imeisha tu.
Risasi Jumamosi: Mumeo amekuwa akikusaidia kulea wanao hasa kucheza nao, naona pia kwa mchanga amekuwa akikusaidia hata kwa malezi, unajiskiaje?
Zamaradi: Nina furaha sana, kama nilivyokwambia nina bahati ya kupata wazazi wanaowapenda watoto wao kama ilivyokuwa kwa wa kwanza.
Stori: Imelda Mtema