
UNAPOMZUNGUMZIA Nancy Abraham Sumari, hakika unataja jina la miongoni mwa kinadada ‘special’ wa taifa hili ambao wana mchango mkubwa kwenye suala zima la maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Mwanadada huyu, mwenye uzuri wa asili jina lake lilianza kupaa mbali zaidi mwaka 2005, baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania, baadaye kushika namba sita kwenye Shindano la Miss Dunia kisha kutangazwa kama Mrembo wa Bara la Afrika Kidunia.
Huyo ndiye Nancy Sumari ambaye tumekuletea leo! Ambaye mchango wake kwenye ujenzi wa nchi amewekeza kwenye habari akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bongo 5 (T) Media Group, lakini pia ni mmoja wa wakurugenzi kwenye Mfuko wa Neghesti Sumari, ambao unahusika na kutoa elimu na kuinua wajisiriamali vijana wa kike na kiume, bila kusahau kwamba anamiliki Jenga Hub, ambapo hapa anawakutanisha watoto pamoja kwenye suala zima la elimu.
NANCY KAANZIA WAPI?
Nancy alizaliwa Mererani mkoani Arusha. Ni mtoto wa tatu, kati ya watano na dada yake Nakaaya Sumari aliyeimba Wimbo wa Mr Politician, ni miongoni mwa watu wenye heshima kubwa kwenye Muziki wa Bongo Fleva.
Kuhusu elimu, Nancy masomo ya shule ya Msingi alisomea Kenya na Tanzania alikuja kwa ajili ya ngazi ya chuo pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
MASUALA YA U-MISS ILIKUWAJE?
Nancy amewahi kusimulia kupitia Startup Grind Local, warsha ambayo huwa inaandaa mikutano kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kuhamasisha na kuwaelimisha vijana wa Kitanzania kuhusu mafanikio kwamba, alianza masuala ya u-miss baada ya kukutana na mwanadada mmoja Dar es Salaam, aliyemwambia kwamba anafaa kuwa mrembo wa Tanzania.
“Ndiyo hivyo ilivyokuwa. Nilijiingiza kwenye masuala ya u-miss wazazi wangu wakiwa hawafahamu kabisa, lakini Mungu alisaidia nikafika mbali na baadaye waliweza kufahamu kwamba ninashiriki kwenye masuala hayo ya urembo,” alisema Nancy.
Kupitia masuala ya u-miss Nancy, alipata ‘experience’, kubwa iliyomjenga na kumsaidia kwa namna moja kufika hapo alipo kwa sasa.
KUHUSU MAFANIKIO
Nancy anaamini wanawake wote wanaweza na kila mmoja anaweza kufikia mafanikio yake na kuwa yeyote yule anayehitaji kuwa Tanzania. Zaidi, anaamini kupitia elimu kwa watoto na wasichana wa Kiafrika ambako pia, ameweza kuweka mchango wake mkubwa huko.
Nancy, ameandika kitabu kiitwacho Nyota Yako, ambacho ni cha mashairi kwa ajili ya kuwainua watoto kwenye masuala ya ndoto zao na namna wanaweza kuzifikia.Huyo ndiye Nancy Sumari, mama wa mtoto mmoja wa kike aitwaye Zuri. Unaweza kufanya maajabu kwenye ulimwengu wako kama Nancy, unaweza kutimiza ndoto zako pia kama mwanadada huyu wa Chuma. Ota sasa, pambana sasa. Mungu ni mwema!
Makala: Boniphace Ngumije na Mtandao