
AFRICAN Stars Band ‘Twanga Pepeta’ imefuLia ile mbaya! Walich-okuwa hawa-kitaki wenye be-ndi hiyo yaani ku-pi-ga sh-oo kwe-nye ku-mbi za usw-azi ndi-cho wana-cho-kifanya hivi sasa.
Waswahili wanasema: ‘Moja shika huzidi kumi nenda.’ Kwa Twanga Pepeta ya leo kupata kandarasi ya kupiga muziki hata kando ya barabara ni bora mara mia kuliko kukosa kabisa.
Twanga wamefikaje huko, wameangukaje, wametelezaje? Ni maswali ambayo majibu yake ni sawa na mmwaga mchele hachagui wapi punje zitaangukia, kila mtu anajibu kivyake.
Niliwahi kumuuliza mmiliki wa bendi hiyo Asha Baraka kwa nini dansi inakufa? Alinijibu: “Na media zinachangia, haziupi mziki wa dansi nafasi ya kusikika.”
Asha asichojua ni kwamba, media hazitengenezi habari; zinaandika habari kwa maana hiyo kitu ambacho si habari kwenye jamii huwezi kukiona kwenye gazeti, televisheni na wala hutakisikia kwenye redio.
Muziki wa dansi usipokuwa habari ya mjini upigwe kwenye redio kwa kumfurahisha nani? Twanga isipokuwa habari iandikwe magazetini isomwe na nani?
Maana ni wazi kwamba jamii ndiyo inayohitaji habari, hivyo kama bendi, msanii, mtu au kitu kimefanya jambo ambalo linahitajika kujulikana kwa watu media hulazimika kuhabarisha umma.

MAWAZO YANGU
Muziki wa dansi ambao kuanzia miaka ya 1960 hadi mwaka 2000 mwanzoni ulikuwa hot, ulijikuta ukikumbwa na dhoruba nyingi ambazo zilihitaji manahodha wenye nguvu kuweza kuhimili usiporomoke.
Nakiri kabisa katika kipindi hicho bendi za Tanzania zilipambana sana, wanamuziki wa bongo walikuwa hodari mno kuweza kuleta matokeo chanya mbele ya ujio wa muziki wa Bongo Fleva ulioonekana kuanza kupendwa na kasi ya muziki wa Kikongo ilikuwa umeteka soko.
Ni Twanga hiihii ndiyo iliouzika ufalme wa nyimbo za Kikongo za akina Pepe Kalle, Yondo Sister, Kanda Bongo Man na wengine na kuwafanya Watanzania wajivunia chao.
Wengi watakubaliana na mimi katika hilo. Lakini Twanga ufalme wake umepinduliwa, ule umati uliokuwa ukijitokeza kuangalia shoo zao unepotea, walipenda kusikiliza nyimbo zao nao siku hizi wachacheee!
TWANGA ILIUAWA
Hakuna cha media kuipa kisogo wala nini; ukweli ni kwamba bendi hii iliuawa! Walioiua siyo watu wasiopenda mafanikio yake bali waliotaka kuhamisha nyota ya Twanga ing’ae upande wao nao wapate mwanga.
Kuna wauaji wa aina mbili lakini wote walikuwa na lengo moja. Wa kwanza ni wenye fedha walioamini kuwa muziki ni biashara na kwamba wangeweza kuwekeza katika muziki na kujipatia fedha nyingi.
Watu wa pili ni baadhi ya wanamuziki nguli wa Twanga waliokuwa wamejitukuza kiasi cha kujiona kuwa wao ni maji na Twanga Pepeta ni samaki; wakasahau kuwa mtazamo wao ulikuwa kinyume chake.

Najiaminisha kabisa; kwa wakati ule Twanga ilikuwa sawa na mti mkavu uliokuwa unasaidia kuni mbichi kuwaka.
Wapenzi wengi wa dansi walipima ubora wa nyimbo za bendi nyingine kupitia ladha ya nyimbo za Twanga. Hii inamaanisha bila Twanga makundi mengine ya dansi yalikuwa hayana maana. Hapo ndipo sababu ya kifo cha Twanga ilipopatikana. Wenye fedha kama nilivyosema waliona Twanga ina hela lakini wasingeweza kuichukua ili fedha wavune wao; mmiliki ni Asha!
Wenye fedha wakageuza shilingi, wakaona kwa sababu hawawezi kumnyanganya Asha bendi Twanga ikawa yao wakawatumia wanamuzki nguli niliowataja kuihamisha kumnyang’anya Asha bendi kwa mlango wa nyuma.
Mtindo wa kuchukua wanamuziki nguli Twanga na kuwapeleka kuanzisha bendi nyingine ukaasisiwa kwa mawazo yaleyale kwamba Asha abaki na jina lakini watendaji waanzishe Twanga mpya.
Nchinga Sound, Double M, Exrta Bongo na nyingine nyingine kibao zikaanza kazi kupambana na Twanga. Lakini tangu lini samaki huishi nje ya maji? Kilichotokea umma unakishuhudia Twanga imekufa na walioiua wamekufa na dansi imezikwa.
TWANGA WAFANYE NINI?
Twanga iandae mapinduzi mapya! Kama iliweza wakati huo na ikaweza kuzalisha vipaji vya akina Ali Choki, Muumini Mwinjuma, Banza Stone (marehemu), na wengine kwa ubunifu wa soko la muziki sambamba na kizazi na wakati, njia fikra hizo zirejee kwa nguvu.
Kama ilivyokuwa Twanga Pepeta ya miaka 2000 iliyokuwa na wanamuziki waliokuwa tayari kutoa burudani kwa mashabiki wao na siyo kujipatia fedha, moyo huo unatakiwa uwepo kwa wanamuziki wapya watakaokuja kuijenga Twanga Pepeta mpya.
Mawazo ya kufikiri kuwarejesha kundini wanamuziki walioifanya Twanga iwe hot yanaweza kuirudisha kwenye mstari bendi ni kujidanganya; samaki aliyevuliwa na kufa kumrudisha majini ni sawa na kumsaidia aoze haraka au ni sawa na kulisimamisha gogo lililokatwa na kulazwa chini, litaoza tu .