×

R.I.P PATRICK… UMEACHA FUNZO!

POLE sana Rose Alphonce ‘Muna Love’ kwa kumpoteza mwanao kipenzi Patrick, salamu za ram­birambi ziende pia kwa ndugu, jamaa pamoja na Watanzania wote ambao wameguswa na msiba huu.

Ukweli ni kwamba Patrick, alikuwa ni mtoto wa taifa. Nyota yake ilikuwa imeanza kung’aa mapema, kiasi kwamba watu mbalimbali pamoja na makampuni yakaanza kumtumia kwenye matangazo na filamu.

Lakini nyota yake imezimika kwenye dunia yetu hii ya mwili wa nyama. Bila shaka, inaanza kuwaka kwenye ulimwengu wa roho na kwenye Biblia Takatifu, ambayo Patrick, aliiamini kuna sehemu inasema;

“Waacheni watoto wadogo waje kwangu kwa maana ufalme wa Mungu ni wao.” Kwa sasa tunaamini roho ya Patrick, imepumzika pamoja na baba yake wa mbinguni.

Hata hivyo kuondoka kwa Patrick kunaacha funzo kubwa kwa kila mmoja wetu, kwa namna ambavyo mtoto anaweza kubadilisha maisha ya mzazi, kuleta upendo baina ya watu na hata kuunganisha jamii kwa jumla, nakueleza zaidi;

PATRICK ALIVYOMBADIL­ISHA MAMA’KE

Nakumbuka mwishoni mwa mwezi wa Machi, mwaka huu, nilipata bahati ya ku­zungumza na Muna mambo mengi kuhusu maisha yake.

Kwanza nianze kusema kwamba nimekutana na Muna katika nyakati mbili tofauti. Wakati akiwa hajaokoka na kumpokea Yesu, na wakati ambao alikuwa ameokoka, hakika walikuwa ni watu wawili.

Muna huyu niliyekutana naye siku hii alikuwa mwa­nadada mpole na aliye­zungumza taratibu. Hata mavazi yake yalikuwa ni tofauti na namna alivyovaa huko nyuma.

Kutokana na mabadiliko hayo niliyoyaona sikusita kumuuliza nini kilimsibu mpaka akaamua kuokoka na alikuwa na muda gani kwenye wokovu. Alinijibu hivi;

MUNA: Nina miezi mitano. Aliyenisababisha hasa niokoke ni mwanangu Patrick.

IJUMAA: Kivipi Patrick ame­sababisha uokoke?

MUNA: Unajua Patrick aliugua kwa muda mrefu miguu. Na ugonjwa wake ulianza kama utani. Tuliamka siku moja akawa hatembei. Anatambaa tu. Nilijua anatania lakini hali ikaendelea kuwa siriasi. Nikam­peleka Hospitali ya Agha Khan, akafanyiwa vipimo nikaelezwa ana maumivu tu baadaye atakuwa sawa. Lakini bado hakupona.

Nikampeleka tena Kliniki ya Sanitarian akafanyiwa uchunguzi ndipo wakani­ambia nimpeleke Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Muhim­bili baada ya kumchunguza walimfanyia oparesheni na kumuwekea vyuma kwenye mapaja huku wakiniambia anatakiwa kuongezewa madini ya ‘Calcium.’

Lakini baada ya muda vile vyuma vikawa vinatunga usaha. Ikabidi wafanye oparesheni ya pili na baadaye ndipo wakafanya oparesheni ya tatu na kumuwekea madini hayo. Madaktari wakaniambia baada ya kuangalia maendeleo yake, atatakiwa tena kufanyiwa oparesheni ya nne na ya mwisho ambayo ndiyo ingemsaidia akarudi kwenye hali yake ya kutembea lakini ingegharimu milioni 25 mpaka 50.

IJUMAA: Aisee pole sana. Enhee ikawaje?

MUNA: Nilihisi kuchanganyikiwa. Zilikuwa ni pesa nyingi ambazo nilifahamu kuzipata kwa haraka ulikuwa ni mtihani mzito. Lakini jambo la kush­angaza wakati mimi ninau­miza kichwa juu ya fedha hizo, mtoto yeye kila mara alikuwa ananiambia tu kwamba mama ukiokoka basi mimi ninapona.

Aliendelea kuniambia hivyo kwa siku kadhaa na kuna

wakati hata kina mama niliokuwa nao pale hospitalini walikuwa wakiniambia usiku nikipitiwa na usingizi Patrick alikuwa anazungumza peke yake na kudai kwamba anazungumza na malaika.

IJUMAA: Uliwahi kumuuliza juu ya hilo?

MUNA: Ndiyo. Alisema hivyo­hivyo na kunisisitiza niokoke. Baada ya kuona ananisisitiza zaidi niliamua kuokoka kweli. Nilitafuta mchun­gaji akaja Muhimbili na kutuombea. Nikatubu na kuokoka.

ALIKUWA MTOTO WA JABU

Muna, kwenye mazun­gumzo yetu alisimulia mengi na alizidi kueleza kwamba baada ya kuokoka mtoto wake alipata nafuu. Msikie mwenyewe;

MUNA: Alipopa­ta nafuu kiuk­weli nilimshukuru Mungu kwani hata oparesheni ya nne haikuweza kufan­yika. Madaktari waliniam­bia niende naye nyum­bani lakini niishi naye kwa uangalifu mkubwa na hakuna anaruhusiwa kukanyaga chini.

IJUMAA: Ana miaka mingapi na ungeweza kuishi naye vipi bila kukanyaga chini?

MUNA: Patrick ana miaka saba. Na suala la kuishi naye bila kukanyaga chini hata mimi lilinipa shida sana. Lakini kuna machuma walimfungia ambayo yalim­said­ia kuwa juujuu.

IJUMAA: Kikaendelea nini mpaka akapona?

MUNA: Baada ya kurudi ny­umbani, nikiwa sipo, nikirejea nyumbani msaidizi wa kazi alikuwa ananiambia kwamba nikitoka Patrick naye anatoka kwenye machuma na kutembea. Ilinishangaza na nikawa mkali kidogo katika hilo, lakini siku moja aliniambia nikimpeleka kanisani atapona kabisa na alini­sisitiza sana. Nikaamua kufanya hivyo. Nikampeleka kwenye Kanisa la Dokas. Tulivyofika pale kanisani alipoiona tu picha ya Yesu, akaanza kutembea. Na huo ndio ukawa uponyaji wake.

 

MUNA ABADILIKA

Baada ya mwanaye kupona Muna alinieleza kwamba ali­badilika moja kwa moja, kuanzia utaratibu wa maisha yake ya kila siku, hakuwa anakwenda tena kwenye sehemu za starehe kama ambavyo ilikuwa awali, hakuwa anakunywa pombe na wala hakuwa ana­jichanganya pamoja na marafiki wale aliozoea nao mara kwa mara.

AZIDIWA, AFARIKI

Hata hivyo akiwa anafurahia maisha hayo ya wokovu, hivi karibuni mwanaye Patrick aliz­idiwa na kupe­lekwa kwenye matibabu Nai­robi, Kenya, alikobainika kwamba alikuwa na uvimbe kwenye ubongo, Jumanne usiku, alifariki dunia. Pumzika kwa amani Patrick.

FUNZO KWA KILA MMOJA WETU

Maisha ya Patrick kwa ujumla ni fundisho kwa kila mmoja wetu nchini. Unaweza kuona namna ambavyo Patrick amebadilisha maisha ya mama yake, namna ambavyo ameunganisha watu.

Wema na Muna walikuwa ha­wapatani, lakini kwenye kipindi hiki cha matatizo wameweza kuungana. Jamii imekaa pamoja na kushirikiana kupigania uhai wake, huu ni mshikamano ambao kwa namna moja au nyingine kupitia Patrick, tunaji­funza kwamba ulitakiwa kuwepo toka awali.

Yapo mengi ambayo tunaweza kuzungumza kupitia mtoto huyu. Lakini itoshe kusema kwamba; ‘Patrick was the best!’ Tutamkumbuka sana, kwa heri mtoto wa taifa!