×

JEMBE LA MJINI HALINA MAKALI

Picha inayohusiana

SHOGA upooooo? Ni Jumatano nyingine tunakutana tena katika kona yetu hii ya kujimwayamwaya, kujiachia na kupata elimu au siyo shoga? We shangaa wenzako tunaingiza pesa siku zinakwenda! 

 

Baada ya kutumia karibu wiki mbili kuwachamba kinababa, leo nipo na nyie wadada! Jamani wanawake wenzangu kuna kipindi kinafika tunatia aibu hadi nashangaa, hivi sisi akili zetu nani katushikia? Kwa nini mambo mengine tunayafanya hadi yamepitiliza?

 

Dada hujaolewa badala utulizane ndiyo kwaaaanza kazi yako kubadili wanaume, bora basi hata ungemaliza hicho chuo, wengine wapo chuoni leo katoka na mwanafunzi mwenzake kesho na mume wa mtu keshokutwa na mwanaume wa mwenzako loooo! Nasema haya namaanisha shoga, ushahidi ninao tena kwa wanaonizunguka! Siku zote nilikuwa kimya kudili na haya mambo ya kinababa sasa leo niwachambe tu hapa mchambike!

 

Kila siku maadili ya kinadada yanazidi kuporomoka, hivi ni nani aliyewaroga ninyi au ndiyo ule msemo wa samaki mmoja akioza basi wote wameoza! Aku bibi weee miye simo! Uvunde wewe shombo utuleteee siye! Shuuuuutuuuuu! Inafika kipindi inasikitisha sana kuona baadhi ya wadada wamepanga nyumba zao na kukaribisha midume mizima waishi nayo au kuwatembelea bila kuwa hata na mshipa wa aibu kutoka kwa majirani wanaowazunguka.

 

Hivi ndiyo kusema mnapenda sana naniliu, si naongea na wewe domo umelivimbisha kama umekosa danga la kukununulia nguo za mtoko! Au ndiyo kukosa kuolewa! Yaani kama huku uswahilini ndiyo usiseme yaani dada mrembo anamuingiza mjibaba mzima chumbani kwake bila hata woga.

 

Halafu siyo dada mmoja unakuta karibia wadada wengi ambao wanaishi wenyewe, wale wanaojifanya wanajua kuishi maisha ya kujitegemea, hivi si msubiri mpelekwe kwa hao wanaume siyo kuwapeleka mnapoishi? Baadaye unaanza kulialia ohhh siolewi! Nani akuoe kama umeshachakazwa ukachakazika! Halooooo eeeehhhh nicheke miye mbavu zangu zitanuke!Tokeo la picha la AFRICAN COUPLES

Siku zote nikiongea shoga nina ushahidi, yananitokea, hili nisemalo nimeshuhudia tena kwa macho yangu huku ushuani dada mmoja kapanga juzi tuu yaani sijui kama vile yeye ndiyo kamuoa mwanaume kwa jinsi anavyomuingiza kwake kila siku.

 

Mwanaume anaishi hapo kwa mdada, asubuhi mpaka jioni hatoki, tena wengine wakitoka utakuta wanakimbilia msalani moja kwa moja! Looo! Baba weee hata aibu! Natamani sana siku moja wanawake wote tufunguliwe macho tuone hawa wanaume wanaotusaliti!

 

Kama hiyo haitoshi, hawahawa wadada kutwa kulalamika tena wengine wananifuata na kunitumia meseji kuwa hawaolewi! Akuoe nani wewe wakati umeoa au unaingiza midume mingine unalala nayo hadi asubuhi! Shoga jembe la mjini tangu lini liwe na makali? Shauri yako endelea na kuingiza midume uone kama hujawa kama jembe la mjini unafika umri wa kuolewa unakuwa umeshachina!

 

Najua maneno yangu kama sumu, usipozingatia yatakuua tu! Shoga kama huwezi kujitunza basi badilika, wanaume wa siku hizi siyo wa zamani ati! Ukiwaita katika chumba unachoishi siku ya kwanza ya pili anakwenda kwa mwingine atafanya hivyohivyo mwisho wa siku unashangaa anakuja kumuoa mtu anayeishi na wazazi wake! Upo?

Kwa leo niishie hapa, ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu!