×

WASIFU WA BIBI ASTERIA KAPELA, MAMA WA SHIGONGO – VIDEO


KUZALIWA KWAKE
Bibi Asteria Kapela alizaliwa Septemba 16, 1931 katika Kijiji cha Kadashi, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza. Mama yake alifariki siku ya kujifungua hivyo hakubahatika kulelewa naye wala kumuona.

 

Katika tumbo la mama yake walizaliwa watoto watatu, yeye akiwa wa mwisho. Familia yao ilikuwa kubwa baada ya baba yake kuoa mwanamke mwingine na kuzaa watoto wengi na pia kuwa na ndugu wengi (Extended family).

Wingi wa watu katika familia ilimjenga na kumfanya kuwa na tabia ya kupenda kuchangia vitu na wenzake, hata wakati mwingine kupenda wenzake wapate kabla yake (Jambo hili linaweza kushuhudiwa na mtu yeyote aliyewahi kufika nyumbani kwake, awe mlinzi, mtu mzima, mpita njia, mfanyakazi wa Global Publishers{Kampuni ya watoto wake} kwani ukiingia katika familia yake ilikuwa ni lazima upikiwe au ulazimishwe kula).

 

 

ELIMU
Bibi Asteria Kapela hakufanikiwa kabisa kupata elimu ya darasani ingawa alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kujifunza jambo na kutunza kumbukumbu za hesabu, taswira au lugha yoyote ile.
Alipenda elimu na siku zote aliwasisitizia watoto wake wasome na kufaulu masomo yao ili maisha yao yawe bora. Katika hili, wajukuu zake watakumbuka kila siku walipokwenda kumuaga kabla ya kwenda shule ilikuwa ni lazima aseme maneno “Baraka kazana kabisa kusoma, uje uwe kama baba yako na wewe uwasaidie baba na mama yako!”
Kwa kifupi ni kwamba alipenda sana elimu kitu ambacho yeye hakufanikiwa kukipata.

 

 

MAISHA YA NDOA
Akiwa na umri wa miaka 14, alihama kijijini kwao, Kadashi baada ya maisha ya hapo kuwa magumu kwenye familia ya baba yake aliyeoa mke mwingine na kuzaa watoto wengi.
Alihamia nyumbani kwa dada yake, Magdalena katika Kijiji cha Kafunzo wilayani Sengerema wakati huo ikiwa chini ya Mkoa wa Geita.

Mwaka 1945 akiwa katika Kijiji cha Kafunzo alikohamia kumfuata dada yake akakutana na kijana machachari, “handsome wa ukweli”, mwenye mbwembwe na maneno matamu kama asali aliyeitwa James Bukumbi, kikaeleweka, wawili hao wakapendana na baadaye kuoana kwa ndoa takatifu kanisani.

 

 

KAZI

Bibi Asteria Kapela hakuwahi kuajiriwa mahali popote pale zaidi ya kufanya kazi ndogondogo za ujasiriamali kama kupika vitumbua na kilimo alizozifanya kwa miaka mingi kwa ajili ya mahitaji ya familia yake akishirikiana na mume wake, James Bukumbi ambaye leo hii amekwishaungana naye na wote wana furaha Mbinguni wakishuhudia nikisoma wasifu huu wakiwa wamekumbatiana.

 

 

IMANI YAKE YA DINI
Pamoja na kutopita darasani kabisa, bibi Asteria alimpenda Mungu wake. Alikuwa ni Mkatoliki aliyebatizwa na kupewa kipaimara, dini ambayo yeye na mume wake waliingizwa vichwani mwa watoto wote.
Pamoja na kipato kidogo alichokuwanacho alipenda sana kuwekeza katika imani yake kwa kuhakikisha anatoa michango mbalimbali kanisani ili apeleke Injili mbele.

 

 

WATOTO
Katika maisha yake ya ndoa na mumewe, bibi Asteria alifanikiwa kupata watoto 11, wa kwanza alikuwa Peter ambaye yeye na mdogo wake, walitangulia mbele ya haki. Wengine ni Leah, Tabitha, Elizabeth, Joyce, Shigongo, Marsha, Jesca (marehemu), Lydia na Violeth.
Marehemu amecha wajukuu arobaini na mbili na vitukuu ishirini na tatu.

 

 

KUUGUA MPAKA KIFO
Bi Asteria alikuwa akiugua kwa kipindi kirefu, aliteseka kwa miezi mingi huku akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu ambalo lilisababisha moyo wake kupanuka.
Akiwa katika maumivu na mateso makali, aliendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, TMJ, Agha Khan, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Hospitali ya Tumbi ambapo huko madaktari na manesi walijitoa kwa nguvu zote kuhakikisha bibi Asteria anapata nafuu na kupona kabisa.

Bi Asteria alifariki dunia Siku ya Ijumaa ya tarehe 27 mwezi wa saba majira ya saa kumi na moja alfajiri akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

 

SHUKRANI
Mpaka mauti inamfikia, si jambo baya kama familia ikiwashukuru watu wafuatao kwa kuonyesha kuwa walikuwa wakihitaji sana kuona bibi Asteria akipata nafuu na kupona kabisa.
– Wauguzi na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha dharura pasipo kuwasahau Dk. Patrick, Dk. Juma Mfinanga na Dk. Upendo. Lakini pia familia ingependa kuwashukuru Dk. Victoria Muntari na Dk. Marealle waliopo katika kitengo cha mifupa hospitalini hapo.

 

 

– Wauguzi na wafanyakazi wote wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete bila kuwasahau Dk. Mlawa, Dk. Kisenge, Dk. Tulizo na Profesa Janabi ambaye ni mkurugenzi wa taasisi hiyo.
– Pia kitengo cha Neulogy (Ubongo na mishipa ya fahamu) bila kuwasahau Dk. Njenje na Dk. Brighton.

 

 

– Wauguzi na wafanyakazi wote wa Hospitali ya TMJ bila kuwasahau Dk. Kaduri, Dk. James ila pia tunawashukuru zaidi vijana waliotusaidia sana katika hospitali hii, Joseph na Martin.
– Pia familia ingependa kuwashukuru wafanyakazi na wauguzi wote wa Hospitali ya Agha Khan bila kuwasahau Profesa Mgisho, Profesa Jamal, Dk. Adebayo, Dk. Fatma.
– Familia ingependa kumshukuru Dk. Wayi ambaye ni mkurugenzi katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha kwa kuonyesha moyo wake wa kumsaidia marehemu. Familia itaendelea kumshukuru Dk. Shimwela wa Hospitali ya Megra kwa msaada mkubwa aliouonyesha kwa marehemu bibi Asteria.

 

 

Pamoja na kuwashuruku watu wote kutoka katika hospitali kadhaa hapa jijini Dar es Salaam, pia familia ingependa kuwashukuru watu wote ambao walitusaidia katika maombi ya bibi Asteria wakiwemo:
– Jumuiya ya Mtakatifu Augustino.
– Paroko wa Kanisa la Mt Martha.
– Sista Theodora wa Kanisa la St. Joseph.
– Familia ya mchungaji Dk. Huruma Nkone na washirika wake wa Kanisa la VCCT lililopo Mbezi Beach.
– Askofu Deo Rubara na waumini wake wa Kanisa la Word Alive.
– Familia ingependa kuwashuruku wafanyakazi wote wa Global Group wakiwemo Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho na Mhariri Mtendaji, Saleh Ally na wafanyakazi wote kwa kujitoa kwao.
Asanteni wote na Mungu awabariki.

VIDEO: ERIC SHIGONGO AKITOA WASIFU WA AMAREHEMU MAMA YAKE