×

ZAMU YA LOWASSA KURUDI CCM!

DAR ES SALAAM: Tufani ya Chama Cha Mapin­duzi (CCM) kuwazoa wapin­zani bado inapiga. Duru za kisiasa zinaonesha kuwa sasa anayesubiriwa kwa hamu kurejea ndani ya chama hicho tawala ni waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

Lowassa aliyekihama chama hicho mwaka 2015 na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadaye kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopita, ame­husishwa mara kadhaa kurejea alikotoka. Chanzo cha kuaminika cha habari kutoka ndani ya CCM kililiambia Uwazi kwa sharti la kutokutajwa jina kuwa kazi ya kumrejesha waziri mkuu huyo wa zamani imefika pazuri na kwamba inachosubiriwa hivi sasa ni wakati timilifu.

Wakati kukiwa na taarifa hizo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Ba­shiru Ally aliliambia Uwazi kwa njia ya simu juzi (Jumapili) kuwa hawezi kumsemea Lowassa kuhusu nia yake ya kurejea CCM.

“Kakuambia kuwa anarudi CCM? Mimi siwezi kumsemea, la­kini nikuambie tu kwamba hayo unayoyaona yanatokea chama chetu kinatesti tu mitambo,” al­isema Dk. Bashiru bila kufafanua kutesti huko kumelenga kufanya nini kikubwa.

UPINZANI KUZIDI KUBOMOKA

Achana na wanachama wadog­owadogo wa vyama pinzani kutimkia CCM, siku za hivi kar­ibuni miamba ya siasa za upin­zani nchini kama Julius Mtatiro kutoka Chama cha Wananchi ‘Cuf’ alikiacha chama chake na kujiunga na chama tawala jambo lililowaacha wapinzani midomo wazi huku wakijiuliza “Hata Mtatiro?”

Wengine walioibua mshtuko katika siku za hivi karibuni ni pamoja na Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara, Mbunge wa Mon­duli nyumbani kwa Lowassa, Julius Kalanga na Diwani wa kata hiyo nao walimuasi waziri mkuu huyo mstaafu na kujiunga na CCM.

Kubomoka huko kwa ngome ya Lowassa iliyokuwa ngumu kuvunjika enzi za uimara wake kisiasa kumetajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni ishara ya moto wa upinzani uliowashwa na waziri mkuu huyo mwaka 2015 kuanza kuzimika.

“Monduli inafahamika miaka nenda rudi, halikuwa jambo la rahisi kwa mtu kwenda kiny­ume na kiongozi huyo, Low­assa anaheshimika, anaaminika lakini leo ukiona kuna watu wa­nakwenda kinyume naye basi yako mambo mawili, moja ni kwamba nguvu zake zimepun­gua au naye anakubaliana na hali hiyo itokee,” alisema Hus­sein Said mchambuzi wa masu­ala ya siasa aliyeko Magomeni jijini Dar es Salaam.

Tangu uvume upepo wa CCM kuubomoa upinzania alioujenga Lowassa Monduli kumekuwa na taarifa nyingi, moja ikiwa ni kuwepo kwa kundi la wanachama wa chama tawala kumuomba arudi CCM ili alinde heshima yake kuto­kana na madai kwamba siasa za upinzani zimepoteza dira.

Hata hivyo waziri mkuu huyo mstaafu amekaa kimya mara zote, akiacha uvumi wa kurejea katika chama chake cha zamani uendelee bila kupatiwa majibu sahihi.

LOWASSA ASUBIRIWA KWA HAMU

Uchunguzi uliofanywa na Uwazi umebaini kuwa pamoja na baadhi ya wabunge na wanachama kutoka vyama vya upinzani kuhamia CCM kwa wingi wao katika siku za hivi karibuni, anayesubiriwa kwa hamu kuchukua uamuzi huo ni waziri mkuu mstaafu Lowassa.

“Wapinzani wameshapoteza mwelekeo, mimi nakuambia siku ambayo Lowassa atarejea CCM nitachinja mbuzi, nak­uapia kwa Mungu kuwa hili litakuwa pigo la mwaka kwa wapinzani wetu,” alisema Mo­hamed Omary mwanachama wa CCM Temeke Kata ya 14, jijini Dar.

Mbali na wanachama wengi wa CCM kutamani Lowassa are­jee kwenye chama chake cha zamani upande wa upinzani nako hofu kwa baadhi ya wa­nachama wanaoamini nguvu zake kisiasa inazidi kutanda hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Kila mtu anajua, wingi wa kura tuliopata wapinzani ulipa­tikana kutokana na nguvu za Lowassa, hata kuna baadhi ya wabunge wetu walishinda siyo kwa sababu walikuwa wana­kubalika kwenye majimbo yao bali walisaidiwa na nguvu za Lowassa.

“Kama Lowassa atarudi CCM mimi nakuambia uchaguzi ujao mimi hata kupiga kura sitak­wenda kwa sababu ushindi wa CCM utakuwa wazi kabisa,” al­isema kijana mmoja aliyejitam­bulisha kwa jina moja la Jabir, mkazi wa Ubungo ambaye pia ni mfuasi wa Chadema.

LOWASSA NA MAGUFULI WANAELEWANA?

Miaka mitatu tangu ufanyike uchaguzi mkuu uliowaku­tanisha Lowassa aliyekuwa anagombea kupitia muungano wa vyama vya upinzani maaru­fu kwa jina la Ukawa na Rais aliyeko madarakani Dk. John Pombe Magufuli kutoka CCM, inaelezwa kwamba harakati za kuwania kiti cha urais haziku­waachia kovu wanasiasa hao na kwamba wanaelewana na kuheshimiana.

Mara kadhaa Rais Magufuli amemsifu Lowassa hadharani na kumtaja kuwa ni mwa­nasiasa mkomavu aliyeleta mchango mkubwa wa kimaen­deleo katika taifa. Lowassa na Rais Magufuli walipokutana Ikulu Januari, mwaka huu, katika kikao chao cha siri rais alisema:

““Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungum­za mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwam­bia ya kwangu, kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fu­lani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivy­osema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.”

Naye Lowassa alitoa yake ya moyo kwa kusema: “Na kwenye nchi yoyote inayoen­delea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayo­fanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakush­ukuru Mhe. Rais, you made my day.”

Ukaribu huu wa viongozi hawa, umekuwa ukitazamwa na wengi kuwa ni kichocheo cha Lowassa kuweza kuamua kurejea katika chama alicho­toka ambacho kinatajwa kuwa kimejaa marafiki zake wengi kuliko upinzani ambao ana­fanya nao kazi hivi sasa.

CCM INATOA RUSHWA KU­NUNUA WAPINZANI?

Baada ya kuwepo kwa wimbi kubwa la wapinzani kujiunga na CCM, baadhi ya viongozi wa upinzani wamekuwa wakila­lamika kwamba chama tawala kinacheza mchezo mchafu wa kuwanunua wapinzani ili kuwadhoofisha nguvu. Akijibu tuhuma hizo mara baada ya kuulizwa na Uwazi juu ya uwepo wa madai hayo, Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru alisema:

“Naomba nikuambie kuwa chama chetu hakina hela za kununua wapinzani na mimi ndiye mtendaji wa chama, sijawahi kuona fungu la hela li­natengwa kwa ajili ya kuhonga wapinzani. “Kinachotokea ni kwamba, chama chetu kimefanya mageuzi makubwa, sasa ki­naaminika, kinawavutia watu.

“Sisi tunapoona watu wanavutika na chama chetu ndiyo tunazidi kupata nguvu ya kuendelea kufanya kazi zaidi zenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo. “Tunaendelea kuwakaribisha wote wanaovutiwa nasi, na kama Lowassa anavutiwa na utendaji wetu tunamkaribisha na wenzake wote.”

WIMBI KUBWA LA WAPIN­ZANI KUHAMIA CCM

Uchunguzi uliofanywa na Uwazi umebaini kuwa kasi ya wafuasi na viongozi wa upinzani kuhamia CCM itazidi kuongezeka kuelekea uchaguzi mkuu na kwamba hiyo ndiyo mikakati ya chama tawala kujihakikishia ush­indi usiokuwa na jasho katika uchaguzi mkuu ujao. “Kama chama hatutaki kufanya makosa, kilichotokea mwaka 2015 kimetupa funzo, kazi tuliyonayo hivi sasa ni kui­marisha safu yetu ya ushindi na kusema kweli adui yako muombee njaa.

“Sisi tunapoona upinzani unabomoka tena kwa sababu ya chama chetu na Serikali yake kufanya vizuri kiutendaji hili ni jambo zuri sana, kwa sababu litaleta utulivu na maendeleo kwa ujumla,” kilisema chanzo chetu kutoka safu ya juu ya uongozi wa CCM kulichoomba kisitajwe jina.

Hata hivyo, wapinzani nao mara kadhaa wamekuwa wakilalamika kwamba mbali na kufanyiwa rafu za kisiasa watahakikisha kuwa wana­jiimarisha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kushika dola.

KUBENEA ATOA YA MOYONI

Kufuatia kuwepo kwa madai kwamba kuna baadhi ya wabunge kutoka Chadema ambao wako mguu sawa kuki­hama chama chao na kujiunga na CCM akiwepo Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, mbunge huyo ametoa ya moyoni kwa kusema hivi:

“Kwanza wanaosema narudi CCM wananikosea sana, mimi katika maisha sijawahi kuwa CCM, sifanani na watu wa CCM, sasa narudije huko. “Mimi nakuambia kamwe sitajiunga na CCM, nitabaki kwenye siasa za upinzani na kama kuna changamoto za ndani nitakabiliana nazo nikiwa humuhumu.”

Baadhi ya viongozi wali­otoka upinzani na kujiunga na CCM ni pamoja na Anna Mg­wira, Kitila Mkumbo, Juliana Shonza, Moses Mashali, David Kafulila, Maulid Mtulya, Mwita Waitara na Patrobas Katambi.