
IKIWA zimeshatimia siku 40 tangu mtoto wake, Patrick Peter afariki dunia, msaani wa filamu nchini, Rose Alphone ‘Muna Love’ ameamua kufunguka mambo mazito kama alivyoahidi kuwa angefanya hivyo baada ya kumaliza kipindi hicho cha funga.
Katika mahojiano maalum na Ijumaa Wikienda, Muna alisisitiza kuwa sasa yuko imara tofauti na mwanzo. “Patrick amenifanya kuwa shujaa na amenibadilisha kwa kiasi kikubwa, mimi sasa siyo Muna yule wa zamani,” alisema.
MSIKIE ZAIDI
Ijumaa Wikienda: Vipi Muna, unaendeleaje sasa hivi?
Muna: Nipo vizuri sana na nina amani ya moyo wangu.
Ijumaa Wikienda: Hivi sasa nimekuwa nikikuona kwenye mambo ya kijamii zaidi, nini kimekusukuma kufanya kazi hiyo?
Muna: Kitu ninachofanya marehemu alitamani sana kukifanya huko mbele na nimeamua kumuenzi kupitia hili.
Ijumaa Wikienda: Watu wengi walijua hadi sasa ungekuwa uko ndani bado ukiwa na maumivu na wengine wanashangaa kukuona ukianza harakati hizi mapema, unawaambiaje?
Muna: Unajua wanashindwa kuelewa mimi sasa hivi nimeokoka, namjua Mungu vizuri sana, siwezi kukaa na machungu hata siku moja.
Ijumaa Wikienda: Unaweza kuwafafanulia kivipi huwezi kukaa na machungu na ni msiba wa mwanao?
Muna: Ni kwa sababu tu hawajamjua Mungu ndiyo maana wanasema hivyo, yaani Patrick amemaliza kazi yake aliyokuja kuifanya hapa duniani na yule mimi ndiye shujaa wangu maana ndiye kanibadilisha mimi nilivyokuwa na mpaka hivi sasa, amenifanya niwe mpya kabisa na siwezi kumuacha Mungu tena, mapito niliyopita ni mengi mno.
Ijumaa Wikienda: Sasa 40 ya Patrick imeshafika na kupita kama siku kadhaa, ulisema ungezungumzia kuhusu mavazi yake, viatu na vitu vingine vinavyomhusu marehemu kwamba utavipeleka wapi, mashabiki wako wangependa kufahamu hilo.
Muna: Kwanza watu wafahamu mimi sina 40, nimeokoka na mwanangu kashaenda kwa baba yake nimemaliza, ila kwa sasa mimi bado nafunga tu mpaka nielekezwe nini cha kufanya lakini nashukuru nimeshaanza kuhudumia watoto wenzake ambao tayari wameanza kupata matibabu, nashukuru sana Mungu kwa hilo.
Ijumaa Wikienda: Hujafikiri kuzaa mtoto mwingine au hata kumchukua mtoto umlee ili kuweza kuziba pengo la Patrick?
Muna: Pengo kwangu hakuna nimeshasema Patrick, kamaliza kazi yake aliyotumwa na baba na mimi sasa hivi sina mpango wa kuzaa mtoto mwingine kabisa, nafanya kazi ya baba kwanza, ninachofanya sasa hivi ni kuwasaidia watoto wenzie matibabu basi.
Ijumaa Wikienda: Kuna tetesi kuwa ulishazaa mtoto mwingine huko nyuma, lakini hujawahi kuweka wazi, unazungumziaje hilo?
Muna: Nilishakwambia shetani anafanya kazi yake maeneo mengi sana na siyo kila mtu atakupenda na mimi kwa sababu nimemjua Mungu, sipendi kubishana na mtu yoyote yule hata kama akinitia kidole jichoni.
Ijumaa Wikienda: Vipi kuhusu taarifa unataka kufunga ndoa na Joel Lwaga ndiyo maana umeingia kwenye ulokole?
Muna: Hizo taarifa siyo za kweli na pia kuna wakati mwingine inabidi uwaache watu wakuongelee wanavyojua wao.
Ijumaa Wikienda: Vipi utacheza filamu tena au ndiyo umeacha kabisa?
Muna: Nitacheza, lakini filamu za kiimani zaidi ili watu wamjue Mungu kupitia mimi.
Ijumaa Wikienda: Nakushukuru kwa ushirikiano wako.
Muna: Asante sana.
STORI: Imelda Mtema, DAR