
TIMU ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, jana Ijumaa ilipoteza mechi kwa kufungwa mabao 3-1 na vijana wenzao wa Uganda katika mchezo wa nusu fainali wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa umri huo (Afcon U17) kwa timu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Uganda ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Abdulwahid Idd aliyefunga dakika ya nne, kabla ya Edson Mshirakandi hajasawazisha dakika ya 11.
Uganda waliamka zaidi kipindi cha pili na kujipatia mabao mawili dakika ya 72 kupitia kwa John Alou, huku bao la tatu likiwa ni la kujifunga kutoka kwa Alphonce Msanda katika dakika ya 90.

Katika matokeo ya mchezo wa awali, Ethiopia waliifunga Rwanda kwa penalti 4-2 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 2-2.
Kesho Jumapili uwanjani hapo, Uganda na Ethiopia zitacheza mechi ya fainali na bingwa ataungana na Serengeti Boys kuuwakilisha Ukanda wa Cecafa katika michuano ya Afcon U17 itakayofanyika mwakani jijini Dar es Salaam. Kabla ya hapo, Serengeti Boys na Rwanda zitacheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.
PICHA: MUSA MATEJA | GPL