
UMESHASIKIA msemo wa: “Usipofanya utafiti huna haki ya kuzungumza?” Ukiwa bado, maana yake jifunze kupeleleza vitu kabla ya kuviongea kwa watu. Ukiupuuza msemo huo utajikuta pabaya siku moja kwa sababu unaweza kuropoka mambo ya uongo halafu yakakukosti; Ijumaa linamkasa mbichi wa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye sasa anaburuzwa kortini kwa kosa la udhalilishaji.
KUMBUKUMBU
Siku za hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa ‘klipu’ yenye sauti inayodaiwa ni ya mzazi mwenzake na Diamond aitwaye Hamisa Mobeto akipanga njama na mganga wa jadi (hajajulikana) kumroga msanii huyo ili kumlainisha amuoe.
Kumbukizi hii inafika pale klipu hiyo ilipodakwa kwa fujo na makundi ya wapenda ubuyu mitandaoni na kuifanya ishu kuwa hoti, kiasi cha kumuibua mzee baba Diamond ambapo alimuibukia kimafumbo mzazi mwenzake huyo na kumwanika vilivyo. “Unapotaka kwenda kwa mganga uniroge mimi na mama yangu unaonekana wewe hushindwi kumuua hata mama yangu,” Diamond alisema katika mahojiano na chombo kimoja cha habari
MOBETO APAGAWA
Mashambulizi ya komenti za mitandaoni zenye hukumu nzito zilipozidi kumtuhumu Mobeto kuabudu ushirikina, mwanamitindo huyo alipagawa kiasi cha kutojua la kufanya. Lakini kama Waswahili wasemavyo penye watu wengi hapaharibiki jambo, inadaiwa kuwa timu Mobeto inayoamini kuwa mwanadada huyo hakurekodi klipu hiyo, ilikuja na hoja ya kutinga mahakamani kutafuta haki.
NANI ANASHTAKIWA?
Chanzo kinasema ni mtu aliyesambaza klipu hiyo ya sauti sambamba na wale waliyoiamini akiwemo Diamond. “Mtu anayesambaza hiyo sauti ameshajulikana, lakini na Diamond naye anatakiwa kupelekwa mahakamani maana aliwaaminisha watu kuwa hiyo ni sauti ya Mobeto.
DIAMOND ATASHTAKIWA KWA KOSA GANI?
Kwa mujibu wa wanasheria, litakalomkabili Diamond ni ‘udhalilishaji’ na kwamba licha ya kwamba hakumtaja jina Mobeto lakini mazingira yanaonesha kuwa aliyekuwa anamzungumzia katika majibu yake alikuwa ni Mobeto. “Nimefuatilia kwa makini sekeseke hilo mitandaoni, Mobeto ana uwezo wa kwenda mahakamani kulalamika kudhalilishwa na waliomshambulia wote wakashitakiwa kwa kosa hilo la kudaiwa fidia.
“Kama unavyojua udhalilishaji siyo kosa la jinai, lipo kwenye Sheria za Mwenendo wa Makosa ya Madai au Civil Procedure Code ya mwaka 1966 iliyofanyiwa marekebisho mara kadhaa,” alisema alisema Hareed Mohamed ambaye ni mwanasheria wa kujitegemea wa jijini Dar.
DIAMOND KUMLIPA MOBETO MAMILIONI
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo alisema kiwango cha fidia ambacho Diamond na wenzake wanaweza kumlipa Mobeto watakaposhindwa kesi kitapimwa kutokana na kiwango cha hoja za mlalamikaji na uamuzi wa mahakama.
“Mlalamikaji ataweza kuiomba mahakamani iamuru mlalamikiwa alipe hata mamilioni. Lakini mahakama nayo itatazama madhara yaliyotokana na udhalilishaji huo, ikijiridhisha inatoa hukumu,”alisema mwanasheria huyo. Aliongeza kuwa, ukifuatilia hali ya kifedha waliyonayo watuhumiwa unaona kuwa Diamond ndiyo mwenye uwezo mkubwa na kwamba huyo ndiyo yuko kwenye hatari kubwa ya kulipa fidia itakayodaiwa na Mobeto kwa kosa la udhalilishaji.
HUYU HAPA MWANASHERIA WA MOBETO
Ijumaa lilipoambiwa kuwa Mobeto anafungua madai dhidi ya Diamond na waliomdhalilisha, lilimtafuta mtu anayetajwa kuwa ni mwanasheria anayeaminiwa na Mobeto ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini, ili kujua kama hatua za kufungua kesi hiyo zimeshachukuliwa.,“Mimi sijaona hiyo klipu na sijaambiwa chochote na Mobeto mpaka sasa, kwa hiyo sina cha kuzungumza zaidi,” alisema mwanasheria huyo kwa kifupi.
MAMA WA MOBETO ACHANGANYIKIWA
Ijumaa lilipomtafuta kwa njia ya simu Mobeto hakuweza kupatikana lakini lilipomtilia mguu mama mzazi wa mwanamitindo huyo anayeitwa Shufaa Lutigunga, alisema kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu amechanganyikiwa. Alipopigiwa simu Diamond hakuweza kupatikana na hata alipotafutwa meneja wake Hamis Taletale, ‘Babu Tale’ simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.
HISTORIA YA DIAMOND NA MOBETO
Awali walianza kujivinjari kimapenzi kwa siri lakini ujauzito ukaja kuwaumbua na kuifanya ishu kuwa wazi na kwamba wawili hao ni wapenzi na wamezaa mtoto wa kiume. Aidha baada ya mambo kuwa mengi na Diamond kugomea kutoa matunzo ya mtoto aliyezaa na Mobeto, mrembo huyo alilazimika kumburuza msanii huyo mahakamani ambapo baadaye mambo yaliwekwa sawa na kesi ikafutwa. Endapo mara hii Mobeto atachukua uamuzi huo itakuwa ni mara ya pili kufanya hivyo, safari hii akienda mahakamani kudai fidia ya kudhalilishwa ambapo chanzo kinasema kuwa amepanga kudai mamilioni ya fedha.
KESI ITAKUWA NGUMU
Katika hatua nyingine baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisheria waliozungumza na Ijumaa walisema kesi hiyo itakuwa ngumu kwa kupatiwa ufumbuzi kutokana na mazingira yake jinsi yalivyo. “Diamond hakumtaja mtu katika mahojiano yake na hata hiyo sauti inayosambaa mitandaoni haiaminiki kama ni ya Mobeto.
“Sasa ili msichana huyo aweze kushinda kesi lazima ifahamike kuwa si yeye aliyerekodiwa na kwamba watuhumiwa walitengeneza klipu, kutakuwa na mvutano mkubwa mpaka kuithibitishia mahakama ukweli usiokuwa na shaka,” alisema Martin Paul mchambuzi wa mambo ya sheria wa Ilala, Dar.
STORI: WAANDISHI WETU, IJUMAA