×

WANNE WAFARIKI AJALINI KILIMANJARO

WATU  wanne wakiwemo wawili wa familia moja wamefariki dunia papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Isuzu kuacha njia na kwenda kugonga gema katika eneo la Kikelelwa wilayani Hai, Kilimanjaro.

Waliofariki wametambulika kwa majina ya Emmanuel Josephat Silayo (28) ,Viviano Silayo (35) wakazi wa Mbomai Juu, Juma Idd (20) maarufu kama Mwarabu na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Deolla.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, aliyefika eneo la tukio amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba dereva wa lori hilo lililokuwa limebeba mbao alikimbia baada ya ajali.

“Jitihada za kumtafuta dereva zinafanyika; chanzo cha ajali ni kupoteza muelekeo kwa lori hilo na baadaye kugonga gema ambapo waliokuwa wamekaa mbele walichomoka na kwenda kupigiza vichwa katika gema hilo na kupasuka,” alisema Kamanda Issah.

Kamanda Issah amesema gari hilo likiwa na shehena ya mbao lilikuwa likitokea eneo la West Kilimanjaro, eneo maarufu kwa uchanaji wa mbao na lilikuwa likielekea Rombo kupitia njia ya Rongai.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hosptali ya wilaya ya Rombo kusubiri maziko.