×

VIFO AJALI YA MV NYERERE KWA JPM HAPONI MTU

AJALI ya Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza inaweza kuhusishwa na uzembe au kutowajibika kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Wakala wa Ufundi, Umeme na Elekitroniki Tanzania (Temesa) hivyo haponi mtu, imeelezwa.

 

Watu kadhaa kutoka eneo la tukio walisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa Ijumaa Wikienda katika eneo la tukio.

JPM KUANZIA HAPA

Walisema kuwa mamlaka hizo tatu ndizo zenye dhamana ya usalama wa usafiri wa majini na kwa vyovyote, katika kutafuta chanzo cha ajali hiyo, Rais John Magufuli ‘JPM’ atalazimika kuanzia hapo.“Tunaweza kusema mengi kuhusu ajali hii, lakini mamlaka zinazohusika na usalama wa usafiri wa majini ni tatu tu; Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Sumatra na Temesa. Uchunguzi lazima uanzie huko,” alisema mmoja wa watu waliokuwa katika shughuli ya uokoaji.

LAZIMA WATU WAWAJIBIKE

Alisema inavyoonekana kivuko hicho kilizidisha mzigo, maana idadi ya watu waliofariki dunia na kuokolewa ni kubwa kuliko ile inayotakiwa kusafiri kwenye kivuko hicho kwa wakati mmoja, hivyo kuna watu wanaotakiwa kuwajibishwa kutoka mamlaka hizo tatu.

JPM AGUSIA UZEMBE

Tayari suala la kivuko hicho kuzidisha idadi ya watu limegusiwa na Rais Magufuli katika kauli yake kuhusu ajali hiyo ambapo pamoja na mambo mengine, alitangaza siku nne za maombolezo ya vifo hivyo zinazoishia leo.Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kivuko hicho kilichokuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100 wanaotakiwa. Aliagiza wahusika wote wa ajali hiyo wakamatwe, akiwemo nahodha ambaye alidaiwa kuwa hakuwa kwenye kivuko wakati kikizama, badala yake alimpa mtu mwingine ‘deiwaka’ kukiendesha.

 

WOTE WAKAMATWE

“Kivuko hicho kilikuwa na uwezo wa kubeba watu 100 au 101, lakini kilibeba watu zaidi. Kuna taarifa kuwa kivuko kilikuwa kimepakia mahindi mengi, bia, soda na vifaa vingine mbalimbali.“Hata aliyekuwa akiendesha hiyo feri siyo nahodha mwenyewe, yeye hakusafiri na inadaiwa amekamatwa na wote wakamatwe,” alisema Rais Magufuli.

 

NAYE WAZIRI MKUU

Kauli ya Rais Magufuli ilithibitishwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa aliyekuwa eneo la tukio ambaye akizungumza na wakazi wa Ukerewe alisema kivuko hicho kina uwezo wa kupakia tani 25 na abiria 100 hadi 101. “Kwa hali ilivyokuwa inaonekana kilizidisha abiria na mizigo,” alisema.Wakati Rais anatoa taarifa hiyo, tayari mamlaka mbalimbali za kiserikali zilikuwa eneo la tukio kusaidia uokoaji. Rais pia aliwaonya wanasiasa kutotumia tukio hilo kisiasa badala yake waache vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake.

WAJIBU WA TEMESA

Wakala huu wa Ufundi, Umeme na Elekitroniki Tanzania chini ya mkurugenzi wake mkuu, Dk Mussa Mgwatu, unatajwa kuhusika kujibu tuhuma za ajali hiyo kulingana na majukumu yake ambayo ni pamoja na kusimamia uendeshaji wa vivuko na kutoa ushauri kwa Serikali na umma juu ya ufundi na umeme.Majukumu mengine ya TEMESA ni kutengeneza magari, pikipiki, mitambo ya Serikali, kusimika mifumo ya umeme, majokofu, viyoyozi na kutengeneza na kusimika taa za barabarani pamoja na kukodisha magari.

 

Watu kadhaa wanaamini kuwa TEMESA ingewajibika, ajali hiyo isingetokea, kwani ilikuwa na fursa ya kutoa ushauri kuhusu umeme na ufundi na kuzuia ajali hiyo kutokea.Hata hivyo, hivi karibuni iliripotiwa kuwa TEMESA mkoani Mwanza ilipitia katika wakati mgumu wa utendaji kutokana na ukata ambapo ilikuwa inazidai taasisi mbalimbali za Serikali jumla ya shilingi milioni 541.9 kwa ajili ya huduma inazozipa.

SUMATRA

Hii ni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini chini ya mkurugenzi wake mkuu, Gilliard Ngewe iliyoanzishwa Kwa Sheria ya Bunge Na. 9 ya mwaka 2001. Mamlaka hii ina wajibu wa kusimamia udhibiti wa soko la usafirishaji wa nchi kavu na majini, ikiwa ni pamoja na usalama na utunzaji wa mazingira.“Hapa Sumatra lazima pia iwajibike kwa sababu kulingana na sheria iliyounda mamlaka hiyo, Sumatra ina wajibu wa kusimamia viwango vya usalama katika sekta zinazosimamiwa na kudhibitiwa na mamlaka,” alisema afisa mmoja wa Jeshi la Polisi katika eneo la tukio.

WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALINO

Wizara hiyo chini ya waziri wake, Injinia Isack Kamwele ndiyo mlezi wa taasisi zote zinazosimamia masuala ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, hivyo ilikuwa na wajibu wa kufuatilia usalama wa vivuko na hivyo kuzuia ajali hiyo.Wengi waliozungumza na gazeti hili walisema waziri wake, anapaswa kuwajibika kwa ajali hiyo kwa kuwa hakuwa amefanya jambo lolote kuizuia.

STORI: Mwandishi Wetu, MWANZA