
MTOTO aliyejulikana kwa jina la Muddy (14), mkazi wa Yombo-Dovya, Dar amejinyonga kwa kamba hadi kufa na kifo chake kuibua mshtuko mkubwa. Tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya usiku wiki iliyopita nyumbani kwao, Yombo-Dovya ambapo chanzo kilisemekana ni kuchelewa kurudi nyumbani ndipo mama yake akamfokea.
Kutokana na kuchelewa huko, mama yake anayejulikana kwa jina la Mwamvita Selemani alihangaika sana kumtafuta, lakini baadaye alipigiwa simu na jirani yake kuwa akamchukue mwanaye. Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mama huyo wa marehemu alieleza kuwa baada ya kupigiwa simu na jirani yake alikwenda kumchukua mtoto wake hadi nyumbani na kuanza kumgombeza kwamba kitendo cha kuchelewa nyumbani si kizuri ndipo mtoto huyo alipokasirika na kuamua kujinyonga.
Mama huyo wa marehemu aliendelea kueleza kwa huzuni huku sauti ikiwa imekauka kutokana na kilio, kuwa yeye na watu wengine walishtushwa na tukio hilo kutokana na kwamba mtoto huyo alikuwa wa pekee aliyejaliwa na Mwenyezi Mungu. “Mwanangu alichelewa kurudi nyumbani na mimi kama mzazi na baba yake wa kambo tulimuuliza kwa nini anafanya hivyo ndipo akazunguka nyuma ya nyumba kwenda kukaa barazani.
“Basi, mimi na mume wangu tukapitiwa na usingizi, Muddy akaja akaanza kugonga mlango kwa kutumia jiwe akisema nimfungulie aingie ndani, nikamwambia mbona huo mlango haujafungwa? Ndipo akaingia ndani, lakini kumbe alitoka tena nje na kwenda kufunga kamba dirishani. “Nilipotoka nilimkuta na kumuuliza mbona unafunga kamba dirishani? Yeye akawa anacheka tu, nikazifungua zile kamba, baada ya hapo akaacha na mimi nikarudi kulala.
“Baada ya muda nilitoka tena ndipo nikamkuta mwanangu ananing’inia, sikuamini nilichokiona, nikamwamsha mume wangu, akatoka nje na kuita majirani ambao walikuta ameshafariki dunia,” alisimulia mama huyo huku akiangua kilio. Naye mjomba wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Salumu alisema kifo hicho kimeibua mshtuko mkubwa kwao kwani hakuwahi kufikiria kwamba mpwa wake huyo angeweza kufanya tukio kubwa kama hilo hasa ikizingatiwa umri wake ni mdogo.
“Hakuwa mtu ambaye angeweza kufanya tukio kama hili kwa sababu kama kuelekezwa na mzazi ni kitu cha kawaida, alafu kwa umri wake ni mdogo sana na isitoshe mama yake alikuwa anajitahidi kumpa kile ambacho anakihitaji,” alisema Salumu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, ACP Emmanuel Likula alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtoto huyo hakuacha ujumbe wowote. Marehemu alizikwa Septemba 20, mwaka huu katika Makaburi ya Kwa Maganga, Temeke- Mikoroshini, Dar.
STORI: Memorise Richard na Neema Adrian, DAR