
LAZIMA unaijua ile ishu kuwa dada wa msanii maarufu Bongo, Ali Salehe Kiba, Zabibu Kiba a.k.a Mrs Banda siku hizi anaishi nchini Afrika Kusini. Zabibu alihamia Afrika Kusini kwa ajili ya kuanza maisha mapya, hii ilikuwa ni baada ya kuolewa na mwanasoka maarufu, Abdi Banda. Banda ni beki na nahodha msaidizi wa Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini maarufu kama PSL.
PSL ni moja ya ligi bora barani Afrika na Zabibu amejichimbia katika Mji wa Polokwane ulio Kaskazini mwa Afrika Kusini. Mji wa Polokwane uko umbali wa kilomita 320 kutoka katika Jiji kubwa la biashara la Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Huu ni mji ulio katika Jimbo la Limpopo na kipindi cha miaka ya 1900 ulikuwa maarufu zaidi kwa mchezo wa kriketi na gofu kutokana na kukaliwa na Wazungu wengi. Gazeti la Risasi Jumamosi, halishindwi! Liliamua kufuatilia na kutaka kujua maisha ya Zabibu huko Afrika Kusini yako vipi.
Shushushu wetu, Hilaly Daudi alitua nchini humo na kufanya uchunguzi kabla ya kuwasiliana na makao makuu jijini Dar ndani ya Ofisi za Magazeti Pendwa yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers. Mahojiano live yalikuwa hivi:
HILALY: Nimefika hapa, Zabibu na Banda wanaishi katika mtaa mmoja wa ushuani, unajulikana kama Dorp.
MAKAO MAKUU: Vipi umefanikiwa kuingia ndani?
HILALY: Niko ndani mkuu, Zabibu ni mkarimu sana na ametukaribisha vizuri.
MAKAO MAKUU: Vipi mazingira hapo, maana isije ikawa Sauz, Sauz halafu kumbe…!
HILALY: Wako vizuri aisee, ukiachana na kukaa uzunguni, jamaa (Banda) kajiweka vizuri. Sehemu yenyewe si kubwa sana lakini ina mpangilio mzuri na ulinzi wa kutosha.
MAKAO MAKUU: Kuna mgambo au kuna kipi kinakufanya uone ulinzi ni maridhawa?
HILALY: Zabibu anafungua geti kwa kutumia simu. Hakuna cha mgambo wala bunduki, akifika anabonyeza simu yake kisha geti linafunguka.
MAKAO MAKUU: Vipi kuhusiana na mandhari ya ndani?
HILALY: Ndani pamekaa bomba sana, kochi la kisasa mfumo wa L. Bonge la runinga aina ya Samsung na kapeti fulani hivi la kitasha. Ukizunguka kwa nyuma, unakuta jiko na makabati fulani hivi ya kijanja.
MAKAO MAKUU: Umefa-nikiwa kuingia hadi geto?
HILALY: Mkuu kama hunitakii mema vile! Banda mwenyewe si unamsikiaga hata uwanjani mambo yake?
MAKAO MAKUU: Duh, kweli. Lakini Zabibu anasemaje?
HILALY: Kwa kweli ni mcheshi sana na anaonyesha kufurahi sana kutuona. Ametuma salamu kwenu, kasisitiza nimsalimie Imelda (Mtema). Lakini anaendelea vizuri na maisha yake ni raha mustarehe.
MAKAO MAKUU: Ahsante sana, unarejea lini?
HILALY: Kesho mkuu, ila nilitamani nibaki maana Zabibu kwa misosi, acha kabisa.
MAKAO MAKUU: Uwahi kurudi.