
TAARIFA zilizotolewa na taasisi ya polisi wa kimataifa (Interpol) zimesema, rais wake, Meng Hongwei, amejiuzulu wadhifa wake na kumtaja aliyekuwa makamu mwandamizi wa rais, Kim Jong Yang, kukaimu nafasi hiyo
Mapema mwezi huu, mke wa Meng aliwaambia waandishi wa habari mjini Lyon, Ufaransa, kwamba alikuwa anahofia maisha ya mumewe kuwa hatarini. Kwa mujibu wa mke wake huyo ambaye alitoa taarifa ya kupotea kwa Meng kwa ofisi kuu ya Interpool nchini Ufaransa, mumewe huyo alikuwa nchini China mwezi ulopita kwa safari binafsi.
Meng mwenye umri wa miaka 64 anaishi kwenye mji wa Lyon uliopo kusini mwa Ufaransa ambao ndipo yalipo makao makuu ya Interpol na aliteuliwa kuwa mkuu wa taasisi hiyo mwaka 2016.
Muda wake wa kuongoza taasisi hiyo unaisha mwaka 2020.
Taasisi hiyo ina ofisi katika kila nchi duniani ikiwemo Tanzania na inafanya kazi zake kwa kushirikisha kila jeshi la polisi ya nchi hizo.
Moja ya kazi kubwa ya taasisi hiyo ni kuwatafuta wahalifu mbalimbali duniani, wanaotafutwa na nchi wanachama kwa kuweka picha zao katika tovuti yake.
Uteuzi wa Meng ulihisiwa na vyombo vya kutetea haki za binadamu kwamba zilikuwa ni jitihada za serikali ya China kuwasaka na kuwatafuta raia wote ambao wanaipinga serikali ya nchi hiyo.
Serikali ya Beijing imekuwa katika harakati za kushikirisha nchi za kigeni katika kuwaorodhesha raia wake ambao wengi wanatuhumiwakujishirikisha na matukio ya rushwa na ugaidi.
Kuna habari kwamba Meng yupo chini ya ulinzi nchini China tangu siku alipotua mjini Peking kutoka nchini Ufaransa.
Mtu huyo ambaye bado kiufundi anafanya shughuli zake nchini China akiwa waziri anayeshughulikia usalama wa raia, anahojiwa na kamati ya nidhamu ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Haijajulikana rasmi anahojiwa kuhusu masuala gani, jambo hilo limekumbwa na giza nene ambapo si wizara ya usalama wala ya mambo ya nje ambazo zilikuwa tayari kujibu masuali ya waandishi.
Chini ya sheria ya uangalizi na kuwekwa chini ya ulinzi, mara zote familia ya mtuhumiwa huwa inataarifiwa ndani ya masaa 24 isipokuwa kama utoaji wa taarifa hiyo utaathiri uchunguzi ambapo kwenye suala hili, familia ya Hongwei haikuwa imepewa taarifa yoyote.
Pamoja na kuwa waziri wa usalama wa raia, Hongwei mwezi Aprili mwaka huu alipoteza nafasi yake katika Kamati ya Maamuzi ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Hata hivyo, Hongwei anaweza kuwa anahusika na kitendo chake cha kutoa agizo liitwalo “Red Notice”, agizo alilolitoa mwaka 2014 la kukamatwa kwa mfanyabiashara tajiri Guo Wengui ambaye alikuwa anahitajiwa nchini China kujibu tuhuma mbalimbali za rushwa.
Ipo orodha ya raia wa China wapatao 44 ambao wanatafutwa na serikali ya China.