
WEEEEER-AAAAA shoga yangu! Unaambiwa gari la kuazima haliwezi kukuishia mafuta na utatembea hadi umalize soli za viatu lakini huwezi kukutana na sanamu likicheka… heeee heeeiyaaaaa! Mama nipe radhi mie kuishi na watu mjini kazi, haswaaa wa jiji kama hili la Dar, upo nyonyo?
Shoga usiwe kama ngiri muda wote meno nje; akicheka hujui, akinuna hujui! Weee shangaashangaa tu wakati kwetu uswahilini hadi dawa ya mswaki ya kupima, haloooo eeeeehhhhhh! Raha ya mtihani aijuae mwanafunzi na raha ya mume aijuae kitanda, uongo shoga? Usinione kama nimekuja kwa kucheka ukaona ni mazuri, leo shoga hana tatizo, weeee! Aliyekwambia nani? Nisije na udambwidambwi aliyekwambia nani? Shuuuuutuuuuuuu! Tangu lini barafu likachemshwa?
Leo nipo na wewe mwanamke mwenzangu ambaye huna hata haya; umri umekwenda, umeingia makanisa na misikiti yote umemaliza kuomba dua na sala uolewe, leo umepata bahati hiyo unawekwa ndani unakuwa kama sanamu la michelini, inahuu? Shoga hakuna kitu kinachokera kama mwanamke kutojitambua, umeolewa lakini unataka kila kitu akusaidie mfanyakazi wa ndani kisa unamlipa! Haya bora akufanyie kwa kuwa umemuajiri, siku akiumwa? Siku akiondoka na kukuacha na mume wako?
Nikisemaga shoga huwa namaanisha ati! Juzi nimeshuhudia laivu mwanamke mzima na micheni yake mwili mzima, ameolewa lakini anajua kufua, kupika maharage, wali, makande, kutengeneza chai, chips na juisi… mwanamke mzima hajui kupika ugali, hajui hata chapati za maji zinatengenezwaje, kisamvu kinatwangwaje, jamanijamani loooo! Dunia simama nishuke, nachoka Anti mie! Sasa shoga yangu hapo tuseme mwanaume amekuoa wewe au ameoa hausigeli? Wee kupika vitu lainilaini ndiyo unaweza lakini vingine hujui sasa si bora urudi kuishi kwa wazazi wako?
Ngoja nikung’ate sikio shoga yangu, wanawake sie huwa tunaaibika sana kwa sababu wakati mwingine tunashindwa kushirikishana kwenye mambo ya msingi, sawa wengine wametoka kwenye malezi ya mboga saba, nyumbani kila kitu alikuwa akifanyiwa halafu moja kwa moja anaingia kwenye ndoa, hivyo vitu atajifunzia wapi?
Kuku mweusi tangu lini akafukuzwa usiku? Kwanza utamuona na giza lote hilo? Badilika shoga usisubiri mpaka giza limekufika ndo unashtuka hujui hata kupika au unajua mapishi malaini ambayo kesho na keshokutwa wakija wakwe unaaibika. We hujiulizi hata aliyegundua raba, naye anaogea kandambili? Ndiyo unatakiwa kujua katika maisha haya kuwa hakuna mjuaji zaidi ya mwenzake! Usiwe na aibu katika kujifunza, kama hujui kutengeneza au kupika kitu fulani basi mshirikishe ndugu au rafiki.
Tena siku hizi mmesogezewa hadi mitandao, kila kitu unachotaka kujifunza iwe kwenye kupika au kuvaa basi unauliza tu mitandao inakuanikia kila kitu. Kwa leo naomba niishie hapa shoga yangu nahisi mate yamenikauka! Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu
