
HII ni kali ya aina yake! Watu wanane wenye ulemavu wa macho wamevamia Ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania,(Tanroads) na kujifungia kama vile wapo mahabusu kisha kugoma kuondoka wakitaka kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda awatatulie tatizo lao.
Tukio hilo la aina yake limetokea hivi karibuni baada ya walemavu hao kuvamia ofisi hizo zilizopo maeneo ya Mbezi- Mwisho jijini Dar wakiwatuhumu Tanroads kutaka kuwaondoa kwenye eneo lao walilokuwa wakifanyia shughuli zao za muziki kwa kuimba na kujipatia kipato.
Akizungumza na kwa niaba ya wenzake mwenyekiti wa walemavu hao ambaye ndiye kiongozi wa bendi yao iitwayo Excellent, Eliya Msoke alisema wamelazimika kuvamia ofisi hizo za Tanroads baada ya wafanyakazi wa ofisi hiyo kuwazuia wasifanye shughuli zao nje ya ofisi hizo.
“Tuliamua kujiunga kwa pamoja na kuunda kikundi ili tuweze kupata riziki kuepuka kwenda kuombaomba barabarani lakini leo hii mtu anakuja na kuamua kutufukuza na kuchukua vitendea kazi vyetu kama vile jenereta, mixer na kipaza sauti kwa madai kuwa tunafanya shughuli kinyume na taratibu ya eneo husika kwa kuwa halijaruhusiwa kukusanya watu.

“Sisi kikundi chetu tumeshajisajili katika sekta husika tunachofuatilia sasa hivi ni kukamilisha tu taratibu za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) tupate usajili kamili na vyote vinahitaji fedha ndio maana tunazitafuta kupitia huo muziki,” alisema Msoke.
Aliongeza kuwa, kazi yao ya muziki wanayoifanya haina wateja maalumu, wateja wao huwapata sehemu yenye mikusanyiko ya watu sasa wanasikitika kuona Tanroads wanawazuia. “Tunapofanya kazi hii ya muziki tunakodisha vifaa pamoja na gari kwa shilingi 100,000 ambayo inapatikana kidogokidogo kutoka kwa watu wanaotazama shoo zetu.
“Sasa kwa kuwa wameamua kumwaga mboga na sisi tunamwaga ugali, hatuondoki humu ndani mpaka tupate muafaka na tutajigawa wengine watabaki hapa na wengine tunatenda kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda ili aweze kutusaidia,” alisema Msoke.
Kiongozi huyo alipoulizwa na Risasi Jumamosi kwa nini wasiondoke wote kwa pamoja hadi kwa mkuu wa mkoa, alisema hawawezi kwenda wote kwa kuwa wakiondoka wote ofisi hiyo itafungwa na wao kupoteza haki na vitu vyao. Alipoulizwa kuhusu familia zao, alisema hawazijali kwa sasa, wataendelea kuishi hapo kwani wanaamini haki itakapopatikana watarejea katika familia zao.
Walemavu hao waliungana na kuunda bendi yao hiyo ambayo ina takriban miezi sita hadi sasa ambayo imekusanye wanamuziki kutoka katika sehemu mbalimbali kama vile Tanga, Geita, Kahama na Mwanza.
Kufuatia sakata hilo, Risasi Jumamosi lilimtafuta Meneja wa Tanroad kwa simu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini ili kupata ukweli ambapo alisema hawako tayari kulizungumzia suala hilo maana tayari wamelifikisha kwenye mamlaka husika.
“Sisi tumesharipoti sehemu husika kwa ofisa utamaduni wa manispaa ndio watazungumzia kuhusu suala hilo mimi siwezi kuzungumzia. “Kwa kuwa sisi ni waathirika tumesharipoti katika Jeshi la Polisi na tumeshatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya, sasa tunasubiri tuone hatua inayofuatia,” alisema meneja huyo.
Imeandikwa: Neema Andrian na Zaina Malogo.
STORI: Waandishi Wetu, Risasi Jumamosi